Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Idadi waliokufa kwenye tetemeko Myanmar yafika 2,700

Muktasari:

  • Mwanamke aokolewa kwenye kifusi cha jengo lilianguka baada ya kufukiwa kwa saa 91, Myanmar inaendelea na maombolezo.

Mandalay. Jamii nchini Myanmar imeendelea na maombolezo ya waliopoteza maisha katika tetemeko kubwa la ardhi ambalo hadi sasa limesababisha vifo vya watu zaidi ya 2,700 wakiwemo watoto 50 waliokuwa katika Shule ya awali karibu na Jiji la Mandalay.

Kati kati ya tukio hilo, dara ya zimamoto nchini Myanmar ilisema waokoaji walimuokoa mwanamke wa miaka 63 kutoka kwenye kifusi cha jengo siku ya Jumanne, zikiwa zimepita saa 91 tangu kutokea tetemeko hilo.

Hata hivyo, mamlaka zilisema uwezekano wa kupata manusura wengine ni mdogo.

Katika  hatua nyingine maofisa wa Polisi na Jeshi la nchi hiyo walikaa kimya kwa dakika moja ili kuwakumbuka waliopoteza maisha katika janga hilo.

Kwa mujibu wa CNN, mashirika ya misaada yamesema jamii zilizoathiriwa vibaya na tetemeko hilo zinahangaika kupata mahitaji ya msingi ikiwemo chakula, maji na makazi.

Tetemeko hilo lenye kipimo cha ritcher 7.7, lililotokea Ijumaa mchana na linadaiwa kuwa tetemeko lenye nguvu zaidi kuwahi kuikumba nchi hiyo ya Kusini Mashariki mwa Asia katika kipindi cha zaidi ya karne moja, likiangusha majengo ya kale na mapya.

Kiongozi wa kijeshi wa Myanmar, Jenerali Mkuu, Min Aung Hlaing, katika hotuba yake kupitia  televisheni leo Jumanne, Aprili Mosi 2025, amesema idadi ya vifo imefikia 2,719 na inaweza kuzidi 3,000.

Amesema watu 4,521 wamejeruhiwa huku zaidi ya 441 hawajulikani walipo.

Watu wasiopungua 20 pia wamekufa katika nchi jirani ya Thailand.

Katika tetemeko hilo, eneo la  katikati mwa Myanmar limeathirika zaidi, milio ya ving’ora ilisikika saa 6:51 mchana Jumatatu, muda halisi ambao tetemeko lilitokea, na kuwalazimisha wakazi kusimamisha shughuli zao ili kuwakumbuka waliofariki.

Nje ya jengo la Sky Villa, mojawapo ya maeneo yaliyoathirika vibaya, waokoaji walisimama kwenye mistari, mikono yao ikiwa nyuma wakitoa heshima kwa waathiriwa.

Maofisa na wahudumu walisimama nyuma ya uzio wa usalama, wakiangalia ndugu wa waathiriwa wa tetemeko kwa mbali huku bendera ya Myanmar ikipepea nusu mlingoti, kutoka kwenye mlingoti wa mianzi uliofungwa kwenye hema la uokoaji.

Wakazi wa jiji hilo wamesema wanakesha nje kwa siku ya nne mfululizo, kwani nyumba zao ziliharibiwa na wanaogopa kutokea kwa matetemeko mengine ya wakati wowote.

“Sijihisi salama. Kuna majengo yenye ghorofa sita au saba karibu na nyumba yangu ambayo yameegemea, na yanaweza kuporomoka wakati wowote,” amesema Soe Tint, ambaye ni fundi saa.

Baadhi ya manusura wana mahema, lakini wengi wakiwemo watoto wachanga na watoto wadogo wanalala juu ya mablanketi katikati ya barabara, wakijaribu kukaa mbali na majengo yaliyoathirika.

Vita yatajwa ugumu kuwafikia waathiriwa

Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Myanmar, ambako jeshi lilitwaa madaraka kupitia mapinduzi mnamo 2021, pia vimeathiri juhudi za kuwafikia walioumia na waliopoteza makazi kutokana na tetemeko hilo kubwa.

Mwandishi wa Al Jazeera, Jessica Washington, akiripoti kutoka Bangkok, Thailand, alisema familia nyingi katika maeneo yaliyoathirika zina matatizo ya kukidhi mahitaji ya msingi.

“Hawana mawasiliano, hawana umeme. Watu wanahangaika. Bado wanalala nje. Katika hospitali moja mjini wagonjwa wanatibiwa nje, wakikabiliwa na joto kali. Upatikanaji wa maji pia ni changamoto,” amesema mwandishi huyo.

Kumekuwa pia na ripoti kadhaa za mashambulizi yanayotekelezwa na jeshi dhidi ya makundi yenye silaha yanayopinga utawala wake licha ya uharibifu uliotokea.

“Kwenye mji ulio karibu zaidi na kitovu cha tetemeko, Sagaing, upatikanaji umekuwa mgumu sana. Tunajua kuna kikosi kutoka Malaysia kilicho kwenye eneo hilo kikisaidia juhudi za uokoaji katika shule iliyoporomoka,” amesema mwandishi huyo.

“Lakini vikosi vingine vya uokoaji vinasema vimezuiwa na wanajeshi na wanamgambo wanaounga mkono utawala wa kijeshi, wakiwazuia kufikia maeneo yanayohitaji msaada wa dharura.”

Wakati huohuo, Shirika la Amnesty International limesema jeshi linapaswa kuruhusu misaada kufikia maeneo yasiyo chini ya udhibiti wake.

“Jeshi la Myanmar limekuwa likizuia misaada kufika maeneo ambako kuna vikundi vinavyopinga utawala wake,” amesema Joe Freeman, ambaye ni mtafiti Amnesty International nchini Myanmar.

“Lazima liruhusu mara moja ufikiaji usio na vikwazo kwa mashirika yote ya kibinadamu na liondoe vizuizi vya kiutawala vinavyochelewesha tathmini za mahitaji,” amesema.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada ya Kibinadamu (OCHA) limesema miongoni mwa waathiriwa wa tetemeko hilo ni watoto 50 na walimu wawili waliouawa wakati shule yao ya awali ilipoanguka karibu na Mandalay.

Gazeti la serikali, Global New Light of Myanmar, pia liliripoti kuwa waumini wa Kiislamu wapatao 500 waliuawa nchini humo baada ya tetemeko kupiga wakati walipokuwa wakiomba kwenye misikiti siku ya Ijumaa.

Katika Bangkok, waokoaji bado walikuwa wakipekua kifusi cha jengo moja la ghorofa ambalo lilikuwa halijakamilika kwa dalili zozote za kupata mtu ambaye yuko hai.

“Kuna miili kama 70 chini ya kifusi … na tunatumai kwa miujiza mmoja au wawili bado wako hai,” alisema Bin Bunluerit, ambaye ni kiongozi wa kikundi cha waokoaji wa kujitolea, akiwa kwenye eneo la tukio.

Naibu Gavana wa Bangkok, Tavida Kamolvej, amesema mashine za Skana zimebaini uwepo wa miili sita yenye umbo la binadamu, lakini hakukuwa na ishara zozote za kuwa wako hai. Alisema wataalamu wa ndani na wa kimataifa sasa wanatafuta njia salama ya kuwafikia.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika ya Habari