Aliyekuwa mteule wa Rais Congo atangaza kuanzisha kundi la waasi

Muktasari:
- Mhalifu wa kivita aliyetiwa hatiani, Thomas Lubanga ametangaza kuanzisha kundi jipya la waasi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Ituri. Mhalifu wa kivita aliyetiwa hatiani na ICC kwa makosa mbalimbali, ametangaza kuunda kundi jipya la waasi lenye lengo la kuiangusha Serikali katika Jimbo la Ituri, lililopo Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
DRC imekuwa ikikabiliwa na tishio la kiusalama katika mikoa ya mashariki ambapo makundi ya waasi hususan ni muungano wa waasi wa AFC/M23 waliotangaza kuishikilia miji ya Goma, Bukavu, Nyabibwe na Walikale.
Hata hivyo, uamuzi wa Thomas Lubanga ambaye ni mzaliwa wa Ituri nchini DRC na anayeishi Uganda, kutangaza kuanzisha kundi la Convention for the Popular Revolution (CPR) unaongeza hofu ya machafuko nchini humo wakati huu ambao Serikali ya Rais Felix Tshisekedi inatafuta maridhiano na M23.
Shirika la Habari la Reuters, limeripoti leo Jumanne Aprili Mosi, 2025, kuwa Lubanga ambaye ni mzaliwa wa Ituri, alihukumiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) mwaka 2012 kwa makosa ya kuwasajili watoto kama askari na akapewa kifungo cha miaka 14 gerezani.
Aliachiliwa mwaka 2020 na Rais Felix Tshisekedi akamteua kuwa sehemu ya kikosi kazi cha kuleta amani Ituri.
Hata hivyo, mwaka 2022 alitekwa nyara kwa miezi miwili na kundi la waasi, tukio analodai lilipangwa na Serikali, na sasa anaishi nchini Uganda.
Katika majibu ya maandishi kwa Reuters, Lubanga alisema kwamba CPR ina sehemu zote za kisiasa na kijeshi, ikiwa na wanamgambo katika maeneo matatu ya Ituri.
Alisema: “kuleta amani katika eneo hilo kunahitaji mabadiliko ya haraka ya uongozi na Serikali,” ingawa aliongeza kuwa kundi lake bado halijaanza operesheni za kijeshi.
Haijulikani ni wapiganaji wangapi Lubanga anawaongoza. Wataalamu wa Umoja wa Mataifa (UN) mwaka jana walimtuhumu kwa kuhamasisha wapiganaji kusaidia kundi moja la wanamgambo wa kienyeji pamoja na M23.
Ikulu ya DRC ilipotafutwa na Reuters haikutoa maoni yoyote kuhusiana na taarifa ya Lubanga kutangaza kuanzisha kundi hilo.
Ituri imekuwa ikikumbwa na machafuko kutoka kwa kwenye makundi mbalimbali ya waasi kwa miongo kadhaa.
Wiki iliyopita, Madaktari Wasio na Mipaka walielezea kuongezeka kwa ukatili uliosababisha vifo vya zaidi ya raia 200 na kuwalazimu karibu watu 100,000 kukimbia makazi yao tangu mwanzo wa mwaka huu.
Wanajeshi wa Uganda wako Ituri kusaidia Serikali kupambana na kundi la Allied Democratic Forces (ADF), ambalo lina uhusiano na Islamic State (IS) na limekuwa likitekeleza mashambulizi mabaya dhidi ya raia wasiyo na hatia wanaoishi maeneo ya vijijini.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika ya Habari.