Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Migogoro ‘nyumba intobhu’ yazisumbua mahakama Mara

Mariam Wankyo mkazi wa Kijiji cha Matongo-Nyamongo ambaye amewahi kukutana na masahibu ya ndoa za aina hii. Picha na Dinna Maningo.

Muktasari:

Ni kutokana na jamii hizo kutofahamu kuwa sheria haitambui ndoa ya jinsi moja.

Tarime. Licha ya kukiri kwamba mila za jamii ya Wakurya inayojulikana kama Nyumba Intobhu inakiuka sheria, inaonekana kama Serihaifahamu pa kuanzia kuidhibiti hali hiyo na hivyo kuzidisha mkanganyiko wa uhalali wake.

Nyumba Intobhu ni mila ambayo humruhusu mwanamke (mara nyingi mtu mzima) ambaye hakuwahi kupata mtoto, ‘kumuoa’ binti mdogo, kisha kumtafutia kijana wa kuzaa naye, lakini watoto hao wakishazaliwa huwa mali ya mwanamke aliyelipa mahari na siyo kijana ambaye ni baba halisi wa mtoto au watoto husika.

Katika jamii ya Wakurya, mmiliki wa watoto huwa ni yule aliyelipa mahari kwa hiyo wanawake wa Nyumba Intobhu wana haki hizo kwani wao ndiyo walipaji wa mahari kwa mabinti ambao huwachukua na kuishi nao.

Ndoa hizo husababisha migogoro ambayo imekuwa ikifikishwa mahamani ambako mahakimu hutumia muda mwingi kuwaelimisha wahusika wanaovutana badala ya kuendesha kesi.

Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ya Nyamwigura wilayani Tarime, Bhoke Kubyo anakiri kwamba mara kadhaa amekutana na kesi za nyumba intobhu ambazo uamuzi wake ni mgumu, hivyo hulazimika kutumia muda mwingi kuelimisha.

Anasema miongoni mwa mwa mambo ambayo yamekuwa yakifikishwa katika mahakama ni suala la umiliki wa watoto, lakini siyo kwa wingi. “Pengine wengi hawafiki mahakamani kutokaana na kutofahamu masuala ya sheria kuhusu umiliki wa watoto. Kama wangekuwa na elimu, wangefika mahakamani kudai watoto wao,” anasema Kubyo na kuongeza kuwa baadhi yao wanaogopa kukiuka taratibu za kimila.

Kubyo anatoa mfano wa kesi ya mwanamke wa umri wa miaka 79 ambaye alioa binti mwenye miaka 20. “Binti huyo aliolewa tu kwasababu kwao walikuwa wanamdhihaki kuwa amekosa mume hata wa nyumba intobhu, hivyo aliamua kuolewa na bibi huyo,” anasema hakimu huyo.

“Kwa hiyo baada ya kuolewa katika nyumba intobhu kwa kutolewa mahari, alikaa kwenye ndoa hiyo kwa mwezi mmoja tu, halafu akapata mwanaume akaolewa.”

Hakimu Kubyo anasema mama aliyekuwa amemwoa alikwenda kudai mahari, lakini baba mzazi wa binti akakataa kwa maelezo kwamba wao walishampatia ‘mke’ hivyo kama anahitaji ng’ombe aliowatoa kama mahari, basi amrejeshe binti aliyekabidhiwa.

“Kwahiyo huyo mama alifika mahakamani na katika shauri hilo ilibidi niwaelimishe kwamba sheria haitambui ndoa ya nyumba intobhu. Kwa hiyo baba wa binti alikubali kurejesha ng’ombe wa yule mama na mambo yakamalizika kwa amani wakifahamu kabisa kwamba ndoa hiyo si halali,” anasimulia Kubyo.

Elimu muhimu

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Tarime, Odira Amworo anasema kisheria hakuna ndoa za watu wa jinsia moja na kwamba hata mwanaume na mwanamke wanapooana na kutotenda tendo la ndoa, hiyo pia siyo ndoa kwani maana ya ndoa ni kila mmoja kupata haki yake.

Amworo anasema kuwa sheria ya ndoa sura ya 29 kifungu cha 63 inasema ni jukumu la mume kumtunza mke wake, akiolewa na mwanamke hapati haki ya kutunzwa na kwa sheria hiyo kifungu cha 64 kinampa haki mwanamke kukopa kwa kutumia jina la mmewe, hivyo akiolewa na mwanamke hiyo haki ataikosa.

“Hii ndoa inatakiwa itokomezwe watu waelimishwe kuwa inasababisha mtoto kulelewa na mzazi mmoja hata makuzi yao yanakuwa ya mashaka. Mama hatakuwa na uwezo wa kumudu maisha labda awe na kipato kikubwa! Kwa kuwa sheria haitambui ndoa hiyo, jamii yenyewe haina budi kubadilika na Serikali ichukue hatua,” anasema Amworo.

Hakimu huyo anasema elimu inaweza kuanza kwenye dini ambako watu hujengwa kiimani kwani hadi sasa hakuna dini inayotambua ndoa ya jinsi moja. Kiongozi wa Answar Sunnah ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Tarime), Ustadh Muhsin Maulid Idd anasema wao wametoa mchango mkubwa wa kupambana na mila potofu kwa lutpa elimu kwenye vijiji vingi.

“Tumegundua kwamba tunaweza kufanikiwa, lakini lazima tujue kwamba watu hawatakiwi kulazimishwa kuacha, bali kuelimishwa ubaya wa mila hizo na jambo la msingi ni kwenda nao taratibu, wataacha tu,” anaema Ustaadh Idd.

Serikali yakemea

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, John Henjewele anasema Serikali inaendelea kukemea ndoa hizo kutokana na ukweli kwamba ni kichocheo cha maambukizi ya maradhi kama Ukimwi na magonjwa mengine ya zinaa.

“Serikali ina jukumu la kukemea mila hizi kwani haihusiki kabisa na mila, maana kwa kabila la Wakurya huruhusiwi kukosoa mila yako hata kama ni mbaya na kwa kutambua nafasi hiyo Serikali inaendelea kukemea,” anasema Henjewele.

Anasema katika mazingira ya sasa ipo haja ya kutungwa kwa sheria ya kuwalinda watoto ambao huwakosa wazazi halali kwa sababu tu ya taratibu za kimila.