Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kibagha, mila ‘inayomjengea’ mwanamume ujasiri

Vijana waukoo waWanyamongo waliofanyiwa tohara Desemba mwaka jana wakiwa na mwandishi wa makala haya( wa kwanza kushoto aliyeketi) . Na mpigapicha wetu.

Muktasari:

Mila za makabila hayo nyingine tumezizoea kwa muda mrefu. Kwa mfano; hakuna wa kuwashangaa Wazaramo kwa ustadi wao katika ngoma au Wamakonde kuchanja nyuso zao.

Katika taifa lenye zaidi ya makabila 120, si ajabu kuona mila  tofauti nyingine zikiwa na mambo yanayoshangaza.

Mila za makabila hayo nyingine tumezizoea kwa muda mrefu. Kwa mfano; hakuna wa kuwashangaa Wazaramo kwa ustadi wao katika ngoma au Wamakonde kuchanja nyuso zao.

Lakini kwa kabila la Wakurya, kuna jambo la kushangaza. Kwao kijana jasiri ni yule anayetahiriwa kwa kisu bila kuweka ganzi.

 Kibagha

Mila hiyo inayojulikana kwa jina la ‘Kibagha’ inaaminiwa kuwa ndiyo humfanya mwanaume aonekane jasiri, tofauti na anayetahiriwa hospitali ambaye huonekana ni mwoga.

“Wanaume wanaotahiriwa hospitali tunawaita ni wanawake wajawazito wanaokwenda kliniki kupima, utaendaje hospitali kwani wewe mgonjwa,” hayo ndiyo maneno ya vijana wa Tarime, mkoani Mara.

Vijana hao wanaeleza sifa za kutahiriwa jandoni kwa kisu na kusema kuwa inawaondoa woga.

“Ni mila na inaondoa woga. Kwa Mkurya aliyetahiriwa kwa kisu, haogopi kukatwa panga wala kisu. Ikitokea amekatwa huona kama amejikwaruza kwa wembe,” anasema Mwita Marwa.

Yanayofanyika

“Ukienda jandoni, wakati wa kutahiriwa huruhusiwi kutikisika, wala kushituka. Unatakiwa usimame wima, hata kama akitokea nyoka mbele yao akasogea kwenye miguu yako, hupaswi kutikisika, wacha akuume ”anaeleza Marwa.

Anasema kuwa unapotikisika unahesabiwa kuwa tayari umelia na ukilia ndiyo jamii itakudharau.

Anaeleza kuwa kijana anayelia jandoni, akikutana na wenzake hudharaulika hivyo heshima kupungua.

“Utadharauliwa hata na watoto na wasichana, pia hutazawaidiwa kwa kuwa umelia wakati ulipotahiriwa,”anafafanua Marwa.

Je, ni kweli wavulana hulazimishwa kwenda kutahiriwa porini badala ya hospitali?

Mwikwabe Mwita, mkazi wa kijiji cha Matongo, Nyamongo anasema kuwa wapo wavulana wanaokwenda kutahiriwa porini kwa hiari yao lakini pia wapo wanaolazimishwa.

“Kwa kweli wavulana wengi wanapenda wenyewe kwenda kutahiriwa kwa kisu porini. Lakini kwa huku, kijana wa umri kuanzia miaka 12 hawezi kukubali kwenda kutahiriwa hospitali, kama ni mtoto atatahiriwa hospitali, akikua na kujitambua anataka kwenda porini kwa kuwa huko kuna heshima yake,”anasema Mwita.

Anaongeza: “Wapo wazazi wanaolazimisha watoto wao kwenda kutahiriwa porini, lakini mimi nashangaa, sijui eneo wanakotahiri huwa kumewekwa nini, kwani unaweza kukuta mtoto nyumbani ni mwoga nawe ukasema huyu akienda kwenye kisu atalia, lakini akifika huko anakuwa jasiri, wala halii.”

Mkazi wa Kijiji cha Nyarero, Matiko Paul(24) anasema ni vigumu utamaduni wa kutahiri wavulana porini kukoma, kwani kila msimu wa tohara wavulana wengi hupelekwa huko.

“Idadi ya chini ni wavulana wanaopelekwa porini kwa tohara kwa wakati ni 100 na wakati shule zinapofungwa, idadi huongezeka hata kufikia wavulana 200 wakitoka koo mbalimbali,”anasema na kusisitiza:

“Mwandishi, mimi nakwambia wavulana wanapenda tohara ya porini, msimu huu wa tohara kuna mvulana wa miaka minane alitoroka akaenda jandoni na kumwomba ngariba amfanyie tohara.

Ngariba akamwuliza kama ombi lake ni la dhati, mtoto akasisitiza kutaka atahiriwe, akasimama kwa ujasiri mbele yake bila kutikisika, ngariba akamtahiri na kijana akauliza; umemaliza? Watu waliokuwepo walimshangilia mtoto huyo kwa ujasiri na kumzawadia fedha nyingi.”

Mkoani Mara tohara ya porini kwa wavulana ni jambo linalothaminiwa kwa vitendo hata na vijana wenyewe.

Mkazi wa Mtaa wa Ronsoti Tarime, Mariamu Chacha anasimulia kwamba mtoto wa kaka yake aliyetahiriwa hospitali akiwa na umri wa miaka 11, alipofikisha miaka 16 akaenda kwa ngariba porini kudai atahiriwe upya.

Tohara ya porini kwa wavulana imekuwa ikiendelea, licha ya Serikali na asasi mbalimbali zikiwamo za kidini kutoa elimu juu ya umuhimu wa kutahiriwa hospitali, kuepuka madhara yanayoweza kutokea kwa kutahiriwa porini kutokana na ukweli kwamba vifaa vinavyotumika havina ubora kiafya.

Taasisi hizo pia zimekuwa zikitoa elimu kwa wasichana ili wasikeketwe.

Katibu wa mila koo 13 za jamii ya Wakurya wilayani Tarime, Boniface Meremo anasema kuwa tohara ya porini ni kudumisha mila na kwamba umri wa wavulana kutahiriwa ni kuanzia miaka 16, ingawa siku hizi imekuwa tofauti. “Siku hizi unakuta wavulana wadogo wanang’ang’ania kutahiriwa porini, japo umri wao hauruhusiwi. Lakini inabidi wamtahiri,”anasema.

Anasema kuwa baada ya tohara wavulana hufanyiwa sherehe ambapo watu hula nyama kwa wingi na kunywa, huku mvulana husika akizawadiwa.

“Mimi kijana wangu alitahiriwa porini akazawadiwa zaidi ya Sh1 milioni, ng’ombe watatu na mbuzi 28. Huoni hapo tayari anakuwa amepata mali itakayomwezesha hata kuoa?

Fedha hizo ni yeye mwenyewe ataamua azifanyie nini, haziguswi na mtu mwingine,”anasema Meremo.

Akitetea tohara hiyo, Meremo anasema hufanyika kwa umakini mkubwa, hivyo hakuna maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwa kuwa kila kijana hutahiriwa kwa kutumia kisu chake na anatakiwa kuwa na glovu kwa ajili ya ngariba kuvaa wakati anapofanyia tohara.

Athari za tohara ya porini

Licha ya jamii hiyo kuthamini tohara ya porini, imebainika kuwa na madhara yakiwamo vijana kuvuja damu nyingi, wengine kupoteza fahamu.

Umbali inapofanyikia tohara pia ni mateso kwa vijana kwani hulazimika kutembea kilometa tatu hadi sita, kwenda na umbali kama huo kwa kurudi.

Chacha Mwita ni miongoni mwa vijana waliotahiriwa porini ambaye anasema:

“Unaondoka nyumbani saa 11 alfajiri, unatembea umbali wa zaidi ya kilomita tano kwa miguu, unatahiriwa na unarudi kwa miguu jumla ya kilometa 10.

Mbaya zaidi unarudi kwa miguu, huli kitu chochote. Mimi nilivuja damu nyingi, nikashindwa kutembea, nikabebwa kwenye pikipiki. Lakini sikulazimishwa kutahiriwa porini, nilipenda mwenyewe.”

Katibu wa afya wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Sufiani Mageta anasema kuwa tohara ya porini ina athari kiafya kwa kuwa hospitali zimekuwa zikipokea vijana waliotahiriwa huku wakiwa na hali mbaya.

“Wengine waliletwa wakivuja damu nyingi, wengine wakiwa wametahiriwa vibaya na kukatwa mishipa,”anasema.

Anasema kuwa tohara ya hospital ni salama kwa kuwa hakuna uvujaji wa damu nyingi, lakini pia hufanyika kitaalamu ikiwamo kutoa dawa ya ganzi ambayo husaidia kumpunguzia maumivu kijana anapofanyiwa tohara.

Mageta anaitaka jamii kubadilika na kuwapeleka watoto wao kufanyiwa tohara hospitali.

Je, tohara ya porini inaruhusiwa kisheria?

Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Patric Muhere, anasema kuwa hakuna sheria inayozungumzia utaratibu au aina ya tohara kwa wanaume.