Wazanzibar wengi hawana mpango wa kustaafu

Ukosekana kwa elimu ya kujiandaa kustaafu, mfumo wa elimu usiomuandaa mtu kujiajiri na uwepo wa pensheni inayotolewa na Serikali kwa wazee zimetajwa kuwa miongoni mwa sababu ya asilimia 47 ya watu wa Zanzibar wenye umri wa miaka 55 kushuka chini kutojua nini watafanya baada ya wakistaafu.

Kiwango cha watu wasiokuwa na mipango ya nini watafanya watakapostaafu Zanzibar, ni kikubwa ikilinganishwa na asilimia 28 ya kitaifa, kwa mujibu wa Ripoti ya Finscope Zanzibar ya mwaka 2023 iliyozinduliwa mapema mwezi huu.

Loading...

Loading...

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kiwango cha watu wasiojua cha kufanya wakistaafu kimeongezeka kutoka asilimia 39 mwaka 2017 hadi kufikia kilipo sasa huku idadi ya watu wanaofikiria kuwekeza katika kilimo na ufugaji ikipaa kutoka asilimia 2 mwaka 2017 hadi asilimia 4 mwaka jana.

Utafiti huo pia unafafanua kuwa, kiwango cha watu wanaopanga kutumia akiba walizonazo watakapostaafu kimeongezeka kutoka asilimia 13 mwaka 2017 hadi asilimia 17 mwaka jana huku wanaotaka kumiliki biashara wakitoka asilimia 10 hadi asilimia 13 katika kipindi hicho.

Pamoja na wengi kutokuwa na mpango lakini moja ya jambo la kufurahisha ni namna watu hao wamepunguza utegemezi kwa watoto wao kwani waliokuwa wanadai kuwa watatunzwa na watoto ajira zao zitakapokoma wamepungua kutoka asilimia 25 mwaka 2017 hadi asilimia 13 mwaka jana.

“Waajiriwa wengi wanaamini zile fedha ni kwa ajili ya kujenga, ila changamoto ukishatoka kazini hakika kama hauna akili ya kujishughulisha mapema hata hizo fedha hujui nini cha kuzifanyia,” anasema Mmoja wa wastaafu katika utumishi wa jeshi, Mwidini Mwinyishekha.

Mwinyishekha anasema hilo linatokana na uhalisia kuwa watu wengi wanapokuwa kazini hawana mawazo ya kufanya kazi nyingine za kuwaingizia kipato.

Licha ya kutokuwa na shughuli nyingine za kuwaingizia kipato, ripoti hii inaonyesha kuwa watu wengi walio katika umri wa kustaafu au chini yake wanayo elimu juu ya mifuko ya hifadhi ya jamii lakini wanaotumia ni wachache.

Loading...

Loading...

Sensa ya watu na Makazi ya mwaka 2022 inaitaja Zanzibar kuwa na idadi ya watu 1,889,773 huku kati yake wakiwa ni wale wenye umri wa kati ya miaka 20 hadi 59 wakiwa 833,773.

Umri huo ambao huenda ndiyo wakawa na uwezo wa kuajiriwa katika sehemu tofauti ambazo Zanzibar huzitumia kama kitega uchumi ikiwemo uvuvi, kilimo na hata utalii

Uelewa

Mbali ya kuwa katika shughuli tofauti za uzalishaji mali, Finscope inasema asilimia 56 wanaelewa juu ya mifuko ya pensheni lakini wanaoitumia ni asilimia 7 pekee huku uwepo wa pensheni inayotolewa na Zanzibar kwa wazee kuwa sababu ya kiwango hicho kuwa chini.

Si hivyo tu, ripoti hiyo unaeleza kuwa watu wa eneo hilo bado ni wazito katika kuchangamkia njia tofauti za uwekezaji ikiwemo hatifungani za serikali.

Ni asilimia 13 pekee ndiyo inayofahamu juu ya hatifungani na amana za serikali wanazoweza kuzitumia katika uwekezaji na nyinginezo lakini hakuna anayezitumia, asilimia 5 wanafahamu kuhusu Mfuko wa Dhamana ya Uwekezaji (UTT) lakini hakuna aliyewekeza, asilimia 9 wanafahamu kuhusu sarafu mtandao lakini hakuna anayetumia huku asilimia 3 ikijiwekeza katika ufugaji.

kuhusu kukosekana kwa madirisha maalumu kwa ajili ya waislamu katika maeneo tofauti inatajwa kuwa sababu ya wao kushindwa kufikia baadhi ya sehemu za uwekezaji kutokana na kuwapo kwa riba ambayo katika dini ya Kiislamu

Mwanasaikolojia John Ambrose anasema watu wanapaswa kufahamu kuwa kustaafu siyo tukio bali mchakato ambao unapaswa kufanyika kati ya miaka 10 hadi 15 kabla.

Katika kipindi hicho, moja ya hatua ambayo mstaafu anatakiwa kuifanya akiwa bado kazini ni uwezo wa kutunza fedha na kuhakikisha mshahara wake wa mwezi uliopita unakutana na unaofuata.

“Ukistaafu katika umri wa utu uzima lazima mtu utakuwa na changamoto nyingine zinazohusiana na afya yako, msongo wa maisha, nguvu, magonjwa hivi vyote lazima mtu ajiandae navyo,” anasema Ambrose.

Anasema badala ya mtu kupanga vitu atakavyofanya pekee pia ni lazima awe na mpango wa lishe kulingana na umri aliopo ili kuuandaa mwili ipasavyo.

 “Endapo hili halijafanyika kikamilifu, watu wanakuwa na msongo wa maisha ambao unasababisha matatizo makubwa, pia ni vyema kutambua kuwa mtu unatakiwa uanze kufanya kitu kabla ya kujikita katika biashara hiyo,” anasema Ambrose.

Wakati yeye akiyasema hayo, Mhadhiri wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Idara ya Uchumi na Usimamizi wa Kodi, Dk Talib Salum Zahor anasema watu kutokuwa na mpango wa kustaafu inatokana na mwamko wao.

Hatahivyo, ametaja kukosekana kwa elimu ya kujiandaa kustaafu kuwa sababu huku akisema hali hiyo hufanya wengine kugushi umri ili waendelee kuwa kwenye utumishi kufanya kazi wakiogopa kwenda kuanzisha biashara mtaani.

“Lakini kwa upande wa Serikali mfumo wa kuhudumia wastaafu, bado haujawezeshwa kuwafanya wastaafu kujikimu na michakato ya maisha baada ya kustaafu,” anasema Dk Zahor.

Anasema kukosekana kwa elimu hiyo pia kumewafanya wastaafu kuamini kuwa uwekezaji unahitaji utayari wa kupokea hasara na walio wengi wanaamini kuwa ukiwekeza utapata mapato ya haraka kiwango cha kulingana na yale aliyokuwa anayapata kwenye ajira.

“Kuna mstaafu anaweza kumuona mwenzake amefeli, kwahiyo na yeye bila kujua akaamua kwamba nami sifanyi biashara kwasababu fulani alifeli na badala yake anaenda kuwekeza kwenye daladala au bodaboda,” anasema Dk Zahor.

Ili kumudu jambo hilo, Dk Zahor anashauri mtu kujipanga tangu mapema ili aweze kufahamu ikiwa anaweza kumudu au vinginevyo.

Mtaalamu mwingine wa masuala ya uchumi, Hashim Khamis anasema kinachokosekana ni mipango thabiti kwenye kujipanga badala yake wanategemea kiinua mgongo.

“Kwahiyo madhara ya kutegemea kiinua mgongo ndio hayo, hakitoshi sasa wakati ukifika mtu ndio anaaza kujipanga kwa wakati huo muda unakuwa hautoshi tena ndio pengine unakuta watu wanaugua na kupta msongo wa mawazo,” anasema Khamis.


Kikokotoo nacho shida

Kukosekana kwa mipango juu ya nini watakwenda kufanya watakapostaafu inahusishwa pia na kiinua mgongo kiduchu anachopewa mtumishi wa umma muda wake wa utendaji unapokoma.

Dk Zahor anasema licha ya kuwa jambo hilo si zuri ila wakati mwingine labda serikali huona watu hawajawa na uelewa wa kuwekeza kwenye maisha ndiyo maana ikaja na mpango wa kuwapatia fedha kidogo kidogo.

“Lakini kile kidogo wanachopewa hakiwezi kuwakimu kutokana na gharama za maisha kupanda huku hawana mbadala wa fedha na hawajajifunza kuwekeza na hajawaweza kuhimili kutoa gharama zinazoendana na maisha,” anasema Dk Zahor.

Suala la kikokotoo linaungwa mkono na Mtaalamu wa Uchumi na Biashara kutoka Chuo kikuu cha Dar es salaam (USDM), Profesa Abel Kinyondo anayesema suala la kumpa mtu kiwango kidogo cha mafao yake inaweza kumfanya ashindwe kufanya kitu cha maana katika maisha yake baada ya utumishi huku fedha kiduchu anayopewa ikiishia katika kula.

“Kuna nchi za wenzetu mtu kusataafu si lazima afike miaka 50, watu wanastaafu wakiwa na umri mdogo kutokana na marupurupu anayopata na fedha anayopewa lakini kwetu mtu anastaafu anaanza kuomba kazi ya mkataba wa miaka miwili miwili,” anasema Profesa Kinyondo.

Suala la Kikokotoo bado limeendelea kuwa kaa la moto kwa Serikali huku wabunge kwa nyakati tofauti wakiitaka Serikali iangaliwe upya ili kuwasaidia wastaafu kwa kile wanachoeleza kuwa ni watumishi kupewa fedha kidogo baada ya kulitumikia Taifa kwa Miaka mingi.


Mkwamo uko wapi?

Wakati kukosekana kwa elimu ya kujiandaa kustaafu kukitajwa kuwa sababu, Profesa Kinyondo anasema watu wanashindwa kufikiria chochote kabla ya kustaafu kwa sababu ya elimu iliyopo inafundisha watu kuajiriwa.

Anasema hali hiyo imekuwa ikiwafanya kushindwa kufikiria nje ya boksi na hata wanapokosa kazi hubaki kuwa wasiokuwa na ajira.

“Kubadili mtaala na kutengeneza watu ambao wanaweza kuajirika ndiyo suluhisho kama inavyofanyika ili wakikosa ajira waweze kujiajiri, lakini kwa sasa tunatengeneza watu wanasubiri kuajiriwa wawe na kazi na si kinyume chake,” anasema Profesa Kinyondo.

Anasema Tanzania ndiyo nchi pekee ambayo pia miezi sita kabla ya kustaafu ndiyo mwajiri anamwandikia barua mwajiriwa wake kutaka ajiandae huku akisema hiyo ni tofauti na nchi nyingine ambazo watu huanza kuandaliwa tangu siku ya kwanza kazini.

“Hivi vitu inabidi umuandae mtu, kwani kadri watu wanavyofanya kazi huwa wanajisahau na si lazima kustaafu kuna kufukuzwa kazi, kupata ajali na mambo mengine yanaweza kutokea yanayoweza kukufanya usiendelee na kazi hivyo wenzetu wanachofanya huwa ni kitu endelevu,” anasema Profesa Kinyondo.


Nini kifanyike

Ili kukabiliana na jambo hilo, Dk Zahor anasema watu wapewe elimu mapema sio kusubiri miaka mitano anakaribia kustaafu ndio anapewa elimu.

Pia washawishiwe kutengeneza vipato mbadala na waaminishwe kwamba mifumo ya uhifadhi wa jamii bado haijaweza kuhifadhi jamii kwa kiwango ambacho kinachotakiwa bali inampatia kiasi kidogo tu cha kuishi.

Kutokana na suala hilo, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) kwa sasa unalipa mafao ya wastaafu kila baada ya siku 14 ili waweze kujikimu kadri mtu alivyojipangia kuzitumia.

Mbali na hilo, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Zanzibar imekuwa ikimpatia kila mzee mwenye miaka 70 pensheni kila mwezi ili ziwasaidie kukabiliana na changamoto za Maisha.

Ili kufanikisha hilo, wazee wamepatiwa vitambulisho ambavyo vitawasaidia sehemu mbalimbali za huduma ikiwemo kwenye vyombo vya usafiri.

Alipokuwa akiwasilisha mpango huo, Mkuu wa Divisheni Pensheni Jamii, Aisha Abass Seif amesema mpango huo umegusa shehia zote 388 za Unguja na Pemba na usaili hufanyika kuanzia ngazi ya Shehia wanazoishi wazee hao.


Loading...

Loading...

Wengi bado matumizi ya huduma za kifedha

Wakati asilimia 84 ya Wazanzibar wakitajwa kupokea malipo yao kwa fedha taslimu na asilimia 49 wakitunza akiba zao ndani ya nyumba, makato makubwa na kukosekana kwa elimu ya matumizi ya huduma za kibenki zimetajwa kuwa sababu.

Takwimu hiyo ni kwa mujibu wa Ripoti ya Finscope Zanzibar ya mwaka 2023 iliyotolewa Machi mwaka huu na Rais Dk Hussein Ali Mwinyi.

Licha ya kuwa ulipwaji ujira kwa fedha taslimu bado upo kwa kiwango kikubwa lakini umeshuka kutoka asilimia 89 iliyokuwapo mwaka 2017 huku kuongezeka kwa matumizi ya huduma za kifedha kupitia simu za mkononi yakitajwa kuwa sababu.

Matumizi ya huduma za kifedha kupitia simu za mkononi yameongezeka hadi kufikia asilimia 4 kutoka asilimia 1 mwaka 2017 huku wanaotumia benki nao wakifikia asilimia 11 mwaka jana kutoka asilimia 6 mwaka 2017.


Wanakotunza akiba

Namna wanavyopokea ujira wao ndivyo namna pia inavyowashawishi kutunza fedha zao, kwa mwaka jana asilimia 49 ya Wazanzibar wanatunza fedha zao ndani ya nyumba ikiwa ni ongezeko kutoka asilimia 35 mwaka 2017.

Matumizi ya huduma za kifedha kupitia simu za mkononi yamesaidia kwa kiasi kuongeza utunzaji fedha kwani ulikua kwa asilimia 37 mwaka jana huku asilimia 17 pekee ndiyo wakitumia benki kutunza akiba zao.

“Ukiweka Sh100,000 benki hauipati yote lazima kutakuwa kuna makato na pengine sio malengo yako, lengo langu ni kuweka hiyo fedha niichukue nikamilishe mipango yangu, sasa ninapokwenda kuchukua Sh95,000 nahisi kama jambo langu limepungua,” anasema Salma Abdi Badrul mkazi wa Zanzibar.

Salma anasema changamoto kubwa ni makato kwa sababu wanahisi kupeleka fedha benki hawezi kuipata yote kama alivyoipeleka hivyo inawaharibia hesabu zao.

Mbali na makato, kukosekana kwa elimu juu ya masuala ya fedha ndiyo sababu ya wengi kuweka fedha zao ndani huku Thabit Makame Issa akisema jambo hilo limekuwa ni utamaduni kwa watu kuamini kwamba benki kuna usumbufu.

“Wakati mwingine wanaambizana kwamba ukienda benki unakuta foleni kwa hiyo anaona kwa nini fedha yake mwenyewe imtese kwenye foleni bora atunze ndani akiitaka atatoa na kutumia,” anasema Issa.

Hashim Awadh Mzee anasema ni vyema taasisi za fedha zitoe elimu kwa wananchi ambayo itakwenda sambamba na kupunguza makato yao ambayo ni kikwazo.

“Bila elimu hatuwezi kufika lakini makato yanakwaza watu, kwenye Sh10,000 ukiambiwa unakatwa Sh300 huoni kama utakuwa umepoteza lakini ukiambiwa unakatwa Sh1,200 unaona ni kubwa sana kwa hiyo unaona ya nini kupoteza fedha yangu,” anasema Awadh.

Fatma Abdallah Mussa anasema kupeleka benki ni nzuri kwani wanapata usalama ila elimu ya benki ndiyo wanayokosa hivyo kuwafanya wahisi zinakatwa.

“Kile unachokatwa tofauti na unavyoweka ndani kwa sababu ndani inaweza kuibiwa au nyumba kuwaka moto lakini ikiwa benki hata ikifilisika lazima haki yako utaipata kwa sababu unajulikana kiasi fulani na hiyo ndio raha ya benki,” anasema

Katika hilo, Mtaalamu wa Uchumi na Biashara, Profesa Abel Kinyondo anasema hela kuwa na mzunguko nje ya taasisi za fedha inafanya watu kushindwa akufikia fursa mbalimbali zinazotolewa na taasisi hizo ikiwemo mikopo.

“Ili benki iweze kutoa mikopo kuna kiwango cha amana ambacho inatakiwa kuwa nacho, kama kikifikiwa kinafanya watu kuwa na uwezo wa kikopeshwa kwa wanaotaka kufanya biashara watafanya lakini hela kuwa nje ya taasisi za kifedha fursa hizi zinakosekana,” anasema Profesa Kinyondo.

 Anasema umefika wakati wa taasisi za kifedha kuangalia kwa nini watu wanaona kuweka hela nyumbani ni chaguo sahihi licha ya kuwapo kwa athari zinazoweza kutokea kama nyumba kuungua au kuibiwa.

“Ni gharama kuweka hela benki kwa sababu unahitaji vitu vingi pia ukiweka hela unakuwa unakatwa kila baada ya muda, ukitoa utakatwa na makato ni makubwa,” anasema Profesa Kinyondo.

Mlolongo huo ndiyo unamfanya mtu kuamua kukaa na fedha nyumbani ili anapoihitaji aipate kwa wakati huo na akitaka kukopa aombe kwa ndugu na yeye akiombwa atoe ndani anakuwa amekwepa gharama.

Alichokisema Profesa Kinyondo, kinaoneka pia katika ripoti hii kwani takwimu zinaonyesha kuwa kwa mwaka jana, asilimia 80 ya Wazanzibar walipohitaji fedha walikopa kutoka kwa familia na marafiki.

Kiwango hicho kimeongezeka kwa asilimia 3 kutoka asilimia 77 zilizokuwapo mwaka 2017 katika utafiti uliotangulia.

Katika hilo asilimia 11 ya Wazanzibar ndiyo wanakopa katika vikundi vya akiba na mikopo vinavyotoa riba na masharti nafuu huku chini ya asilimia 4 ndiyo wanaoweza kufikia mikopo ya benki na chini ya asilimia 1 wakikopa kutoka mitandao ya simu.

 “Lazima tujiulize nini kifanyike katika sekta ya fedha ili watu wavutiwe kuweka fedha kule,” anasema Profesa Kinyondo.

Akizungumzia suala hilo, Waziri wa Nchi, Fedha na Mipango Dk Saada Mkuya anasema mwelekeo wa serikali kwa sasa ni kuhamasisha matumizi ya mifumo ya fedha badala ya fedha taslimu.

“Katika kuliendea jambo hilo, kwa sasa hakuna malipo yoyote ya serikali yanayotolewa kwa fedha taslimu badala yake ni kutumia mifumo ambayo alikiri bado ilikuwa hajaeleweka kwa watu wengi lakini elimu tayari imeanza kutolewa.