Wadau uhamiaji wasema mfumo, vishoka vinawaumiza

Unguja. Licha ya Serikali kuanza kutumia mfumo wa kielektroniki katika kushughulikia vibali idara ya uhamiaji, wadau wa uhamiaji wamesema bado ipo changamoto kubwa hususani uimara wa mtandao na kusababisha kazi hiyo kuingiliwa na vishoka.
Hivyo wameiomba Serikali kuwekeza zaidi kwenye masuala ya intaneti kwa kutafuta watoa huduma wengi badala ya kutegemea mtu mmoja ambao mara kwa mara huzidiwa na kukwamisha kazi.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu Novemba 21, 2022 katika mafunzo maalumu baina ya watendaji wa idara ya uhamiaji na wadau wa uhamiaji wa Tanzania nzima uliofanyika Unguja Zanzibar yenye lengo la kujadili fursa na changamoto katika idara hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya wadau wengine, Ofisa mwajiri na Mkuu wa Uhusiano wa Serikali kutoka Taasisi ya Aga Khan Heath Services Tanzania, Juma Dossa amesema hiyo ndio changamoto kubwa inayowakwaza kiutendaji.
“Tunashukuru kwa sasa kuna mambo ya elektroniki, lakini kuna changamoto ya mtandao, mara nyingi unapotoa maombi ya vibali vya ukaazi unategemea ndani ya wiki moja uwe umeshakamilisha lakini unaambiwa system ipo chini kwenye malipo,” amesema
Kwa mujibu wa Dossa wanakumbana na vishoka ambao amesema wakati mwingine wanasababishwa na changamoto hiyo wakiamini wataweza kushugulikiwa haraka hivyo kuiomba mamlaka kuwapatia vitambulisho maalumu wanaoshughulika na uhamiaji kumaliza tatizo hilo.
Naye Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Tanzania, Dk Anna Makakala amesema mifumo imerahisisha huduma ikilinganishwa na kipindi cha nyuma ambapo kwasasa taasisi ambazo mifumo yao imeunganishwa na mifumo ya uhamiji akija mgeni hawana haja ya kuomba tena nyaraka.
Kuhusu suala la intaneti alisema linasababishwa na kuwa na mtoa huduma mmoja ambapo hata hivyo wanaendelea kupata ufumbuzi.
Naye Waziri wa Mambo ya Ndanii, Hamad Masauni amesema Serikali inatumia mamilioni ya fedha kugharamia mifumo lakini wapo watendaji wasiokuwa waaminifu wanaoichezea makusudi kwa ajili ya kutengeneza mazingira ya rushwa.
“Hili jambo halikubaliki na tutachukua hatua. Hata wapo wengine wanashirikiana na vishoka tena unakuta ofisi zao zipo karibu na ofisi za uhamiji, nimeshaagiza na ninaagiza tena mambo haya yashghulikiwe,” amesema