Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vuguvugu la mgomo wa malori

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa tangazo la mpango wa mgomo, huduma za usafirishaji mizigo kupitia malori zinatarajiwa kusitishwa kuanzia Julai mosi, 2026, kuishinikiza Serikali ifanyie kazi masilahi ya madereva na kuboresha barabara ili kuepusha ajali.



Dar es Salaam. Vuguvugu la kusimama kwa shughuli za usafirishaji wa mizigo mikoani na nje ya nchi kwa malori linanukia nchini, baada ya madereva kutangaza kusudio la kugoma kushinikiza Serikali kutatuliwa kwa changamoto zao.

Kwa mujibu wa tangazo la mpango wa mgomo huo, huduma za usafirishaji mizigo kupitia malori zinatarajiwa kusitishwa kuanzia Julai mosi, 2026, kuishinikiza Serikali ifanyie kazi masilahi ya madereva na kuboresha barabara ili kuepusha ajali.

Hata hivyo, tayari Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), imesema imebaini tetesi za mgomo huo na inafanya juhudi za kuhakikisha inakutana na uongozi wa madereva kwa mazungumzo ya kutafuta mwafaka.

Taarifa ya mpango wa mgomo huo, zimesambazwa katika makundi mbalimbali sogosi ya WhatsApp wiki hii, zikiambatanishwa na kaulimbiu ya: “Sauti ya Dereva Isikike, Haki Yetu Itendeke.”

Alipotafutwa leo Jumatatu, Juni mosi, 2026, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa kuhusiana na suala hilo, amesema ndio kwanza analisikia na kuomba apewe muda kulifuatilia.

"Ndio kwanza nakusikia ukiongelea suala hilo, naomba nipe muda nifuatilie niweze kujua ukweli wake," amesema Msigwa.

Waziri wa Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, alipopigiwa jana Jumapili, simu yake ilita bila kupokewa na hata alipoandikiwa ujumbe mfupi hakujibu.

Wakati kwa Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, simu yake haikuwa ikiita kabisa licha ya kupigiwa kwa nyakati tofauti.

Naibu wake, David Kihenzile simu yake iliita bila kupokewa.


Taarifa ya mgomo

Kwa mujibu wa taarifa hiyo yenye anwani ya Mkombozi Driver Africa Group, madereva wamechoka kusubiri utekelezaji wa uamuzi uliofikiwa katika mikutano mbalimbali kati yao na Serikali.

“Baada ya juhudi kubwa za muda mrefu za kuwasilisha kero na madai yetu, ikiwamo kukutana na mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye alitoa maelekezo ya kuundwa kwa Kamati Maalumu ya kushughulikia matatizo ya madereva.

“Mpaka sasa maelekezo hayo hayajatekelezwa na hakuna majibu ya kuridhisha yaliyotolewa licha ya makumbusho mbalimbali,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Kutokana na hali hiyo, kundi hilo limetangaza rasmi kusitisha huduma za usafirishaji wa mizigo nchi nzima kuanzia saa 12:00 asubuhi ya Julai mosi, 2026.

Iwapo mgomo huo utatekelezwa, unaweza kuathiri kwa kiwango kikubwa mnyororo wa usafirishaji wa bidhaa nchini na katika nchi jirani zinazotegemea Bandari ya Dar es Salaam kwa usafirishaji wa mizigo.


Madai ya madereva

Katika tangazo hilo, madereva wamewasilisha madai saba wanayotaka yashughulikiwe, ikiwamo kuongeza kiwango cha chini cha mshahara kutoka Sh350,000 hadi Sh1 milioni kwa mwezi.

Lingine, wanataka masharti ya uhuishaji wa leseni yarahisishwe, huku madereva wenye uzoefu wa zaidi ya miaka 15 wakitaka kuondolewa baadhi ya masharti wanayoyaona kuwa mzigo usio wa lazima.

Tatu, wanapinga gharama za mafunzo ya leseni zinazofikia Sh375,000, wakisema kiwango hicho ni kikubwa ukilinganisha na mishahara wanayopokea.

Nne, wanataka Bandari Kavu (ICD) zote zilizopo ndani ya Jiji la Dar es Salaam zihamishiwe Kwala, wakiamini hatua hiyo itapunguza msongamano mkubwa wa magari unaoendelea kushuhudiwa jijini.

Tano, wanataka Serikali iboreshe miundombinu ya barabara wanazodai kuwa chanzo kikubwa cha ajali zinazohusisha magari makubwa.

Sita, wanataka kuwepo kwa mfumo bora zaidi wa kusikiliza na kutatua changamoto za madereva kwa wakati.

Dai la saba ni kuhoji uwepo wa maofisa wa Latra barabarani, wakitaka mamlaka hiyo ijieleze kuhusu msingi wa kisheria wa baadhi ya shughuli zake za ukaguzi.


Vyama vya madereva

Ingawa vyama vya madereva wa malori waliozungumza na Mwananchi vimedai hawautambui mgomo huo, kwa upande mwingine baadhi yao wamekiri kuwepo kwa changamoto zilizoorodheshwa na kwamba zimekuwa zikijadiliwa kwa muda mrefu.

Katibu wa Chama cha Wafanyakazi Madereva Tanzania (Tadwu), Ally Kimaro amesema changamoto inayowakabili ni utekelezaji hafifu wa mikataba ya ajira licha ya kuwepo kwa makubaliano yaliyofikiwa kati ya wadau na Serikali.

Amesema baadhi ya waajiri wamekuwa wakikiuka masharti ya mikataba huku usimamizi ukiwa dhaifu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Madereva wa Mabasi na Malori ya Masafa Marefu Tanzania (TLDTA), Shabani Dede amesema changamoto nyingi zilizotajwa katika tangazo hilo ni za kweli, lakini suluhisho lake si mgomo bali mazungumzo.

Dede, amesema madai mengi yaliwasilishwa serikalini tangu Juni mwaka jana, lakini mchakato wa kuyafanyia kazi ulipungua kasi kutokana na shughuli mbalimbali za kitaifa, ikiwamo uchaguzi mkuu.

Ametaja masuala ya masilahi, mikataba ya ajira na ubovu wa miundombinu kuwa miongoni mwa changamoto kuu zinazowagusa madereva wengi nchini.

“Kuhusu mshahara, tulipendekeza madereva walipwe kwa dola kwa sababu sehemu kubwa ya safari wanazofanya zinahusisha matumizi ya fedha za kigeni. Mapendekezo yetu yalikuwa dereva alipwe angalau Dola 500 kwa mwezi,” amesema.

Aidha, amesema chama hicho kilipendekeza malipo ya safari yaongezwe kutoka Sh700,000 hadi Dola 800 za Marekani, huku posho za kuchelewa njiani (overstay) zikiongezwa ili kuendana na hali halisi ya gharama za maisha.


Latra yasema inafuatilia

Kaimu Ofisa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa Latra, Fungo Augustus amesema mamlaka hiyo ipo tayari kusikiliza hoja za madereva na kuchukua hatua kwa yale yatakayobainika kuwa ndani ya mamlaka yake.

“Makundi ya madereva yapo mengi na waliotoa tamko hili si chama kinachotambulika rasmi. Hata hivyo, tutawatafuta ili tuwasikilize. Yapo madai yanayohusu Latra na mengine yanayohusu taasisi nyingine za Serikali,” amesema.

Kuhusu madai yanayoihusisha Latra, Augustus amesema mamlaka hiyo inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na kwamba hatua zinazochukuliwa dhidi ya baadhi ya magari mara nyingi huhusiana na ukiukwaji wa masharti ya ajira au matumizi ya madereva wasio na sifa zinazotakiwa.


Mtazamo mbadala

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Malori Tanzania (Chawamata), Nuhu Mgodo amesema pamoja na kutounga mkono mgomo huo, baadhi ya malalamiko yaliyotolewa yana mantiki.

Hata hivyo, amesema chama chake hakikubaliani na hoja ya kupinga mafunzo ya madereva.

“Ukweli ni kwamba kazi yoyote inafanyika vizuri zaidi ikiwa mhusika amepewa mafunzo stahiki. Tabia ya zamani ya kupata leseni bila mafunzo ya kutosha imechangia baadhi ya matatizo tunayoyaona barabarani,” amesema.

Kuhusu madai ya kuondolewa kwa Latra barabarani, Mgodo amesema mamlaka hiyo ipo kwa mujibu wa sheria na ina wajibu wa kusimamia sekta ya usafiri.

Pia, amesema changamoto za miundombinu hakiwezi kuwa sababu pekee ya kusitisha huduma kwa kuwa baadhi ya maeneo yana barabara nzuri na madereva wanapaswa kuendesha kwa kuzingatia hali ya eneo husika.

“Mimi naamini jambo la msingi zaidi ni kuboresha masilahi ya madereva. Hilo ndilo linalowagusa wengi moja kwa moja. Mambo mengine yanahitaji elimu zaidi na ushirikiano wa wadau mbalimbali,” amesema.


Wamiliki wa malori waonya

Rais wa Chama cha Wasafirishaji Tanzania (TAT), Omari Kiponza amesema chama chake hakijapokea taarifa rasmi za mgomo huo na kimeziona taarifa hizo kupitia mitandao ya kijamii kama wananchi wengine.

Hata hivyo, ameonya kusimamishwa kwa huduma za usafirishaji wa mizigo akisema kunaweza kuleta madhara makubwa kwa uchumi wa nchi, hasa ikizingatiwa nafasi ya sekta ya usafirishaji katika kuhudumia biashara za ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

“Sekta hii ndiyo uti wa mgongo wa mnyororo wa usambazaji wa bidhaa. Kusimama kwake kunaweza kuathiri biashara, viwanda na shughuli za bandari,” amesema.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori ya Kati na Madogo Tanzania (Tamstoa), Chuki Shabani, amesema chama chake hakijapokea malalamiko rasmi kutoka kwa madereva wala taarifa ya kusudio la mgomo.

“Hatuna taarifa rasmi kutoka kwa wanachama wetu. Tunachokiona kwa sasa ni taarifa zinazozunguka kwenye makundi ya mitandao ya kijamii. Ni muhimu hoja hizi zikashughulikiwe kupitia njia rasmi za mazungumzo,” amesema.