Serikali yatoa mbinu kuwainua wajasiriamali, wafanyabiashara nchini

Naibu Waziri Wizara ya Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe (wapili kushoto) akipita katika mabanda ya wajasiliamari, wakati wa ufunguzi wa maonesho ya viwanda na biashra za wanawake na vijana jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), Mwajuma Hamza. Picha na Michael Matemanga
Muktasari:
- Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, azielekeza taasisi za Serikali kuwasaidia wajasiriamali na wafanyabiashara ili kukuza uchumi na kuongeza ajira.
Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, amezielekeza taasisi za Serikali kuwasaidia wafanyabiashara na wajasiriamali ili wazidi kukua, kwani ni faida kwao na Taifa kwa ujumla.
Amesema mchango wa wajasiriamali katika uchumi wa nchi ni mkubwa, si Tanzania tu bali duniani kote.
Waziri Kigahe amesema hayo leo Jumatatu, Machi 3, 2025, kwenye ufunguzi rasmi wa maonyesho ya viwanda na biashara za wanawake na vijana yaliyoandaliwa na Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), katika viwanja vya Mlimani City.
Maonyesho hayo, yenye wajasiriamali zaidi ya 300 kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, ni sehemu ya maadhimisho kuelekea kilele cha Siku ya Wanawake Machi 8.
"Kote duniani, wajasiriamali ndiyo wanaozalisha kwa wingi bidhaa mbalimbali, ambazo ni za mwisho kwenda kwa walaji pamoja na bidhaa za kati zinazoenda kwenye viwanda vingine vya juu.
“Ombi langu kwa wajasiriamali, tuendelee kutumia fursa zilizopo zilizowekwa na Serikali, pia tutumie taasisi zetu zilizo chini ya wizara na nyingine za Serikali," amesema.

Naibu Waziri Wizara ya Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe (wapili kushoto) akipita katika mabanda ya wajasiliamari, wakati wa ufunguzi wa maonesho ya viwanda na biashra za wanawake na vijana jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), Mwajuma Hamza. Picha na Michael Matemanga
Amesema wakiwezeshwa wakazalisha kwa tija na ubora, watauza kwa soko la ndani na nje, sambamba na kuongeza ajira nchini.
"Muhimu zaidi, tunataka tupunguze uagizaji wa bidhaa kutoka nje, kuepusha matumizi ya fesha za kigeni. Mmeona mafuta kula, ya kupaka, sabuni, tulikuwa tukiagiza kutoka nje kwa wingi; sasa tunataka fedha zetu ziagize bidhaa nyingine ambazo hatuwezi kuzalisha," amesema.
Aidha, ametoa rai kwa Watanzania kupenda bidhaa za ndani kwa sababu zikinunuliwa, uchumi utakua na wajasiriamali watanufaika, kutaondokana na dhana ya kukosekana kwa ajira.
"Tunawahakikishia wajasiriamali wanawake, vijana, na wote kuwa Serikali iko bega kwa bega nanyi kuhakikisha mnatimiza lengo lenu na kuwa chachu ya maendeleo ya nchi yetu kama sehemu ya sekta binafsi," amesema Kigahe.
Rais wa Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara (TWCC), Mercy Sila, amesema wamefungua dirisha la vijana kutoka miaka 15 hadi 35 katika kuongeza ushiriki ili kwa pamoja nchi ijengwe.
Naye, Mkurugenzi wa TWCC, Mwajuma Hamza, amesema wafanyabiashara wanachagia katika biashara na pato la Taifa na kuzalisha ajira, hivyo hawana budi kuinuliwa.
Akizungumza, Ofisa Sheria Mwandamizi kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), Anneth Mfinanga, amesema kwa sasa kuna fursa za wafanyabiashara na wajasiriamali wakubwa na wadogo, hivyo wanachokifanya ni kuwasaidia kurasimisha biashara zao.
"Katika kuwasaidia kuwakuza, tunatoa elimu na kuwasaidia kurasimisha, kwani kigezo kikubwa ni kuwa na namba ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), ili walinde jina la biashara sambamba na kupata mikopo kutoka taasisi za kifedha," amesema.