Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yaanza safari ya kuondoa uchimbaji wa kubahatisha

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde (kushoto), wakati akipokea Ripoti ya Mapendekezo ya Kuwaendeleza Wachimbaji Wadogo wa Madini nchini. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Hatua hiyo inatarajiwa kuwezesha sekta ya madini kuchangia zaidi katika ukuaji wa uchumi wa Taifa kupitia uzalishaji wenye msingi wa taarifa, teknolojia na uwekezaji wa kisasa

Dar es Salaam. Serikali imesema imeanza hatua za kuondoa uchimbaji wa kubahatisha nchini kwa kuweka mfumo utakaowezesha asilimia 10 ya makusanyo ghafi ya mapato ya madini, kubaki kwenye sekta ya madini kwa ajili ya kugharamia utafiti na uwekezaji.

Hatua hiyo inalenga kuboresha tija ya uchimbaji, hususan kwa wachimbaji wadogo kupitia upatikanaji wa taarifa sahihi za kijiolojia, teknolojia na upatikanaji wa mitaji.

Akizungumza wakati wa hafla ya kupokea Ripoti ya Mapendekezo ya Kuwaendeleza Wachimbaji Wadogo wa Madini nchini mwishoni mwa wiki, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema uamuzi huo ni sehemu ya mageuzi makubwa ya Serikali katika sekta ya madini.

Mavunde amesema changamoto kubwa inayowakabili wachimbaji wadogo si kukosa juhudi, bali kufanya kazi bila taarifa za uhakika kuhusu maeneo yenye madini hali inayosababisha gharama kubwa na kupunguza uwezekano wa kupata mikopo.

Amesema Serikali kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27, itaweka mfumo wa Mfuko wa Utafiti wa Madini, ambao asilimia 10 ya makusanyo ghafi ya mapato ya sekta hiyo itatumika moja kwa moja kugharamia utafiti na uwekezaji.

“Utafiti ndiyo msingi wa uchimbaji wenye tija. Unamwezesha mchimbaji kujua mahali pa kuchimba, kupanga uwekezaji na hata kupata taarifa zinazoweza kumsaidia kukopesheka,” amesema Mavunde.

Ameongeza kuwa, Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisikiliza changamoto za wachimbaji na wadau wa sekta hiyo na uamuzi wa kurejesha sehemu ya mapato katika utafiti unaonesha dhamira ya Serikali ni kuhakikisha rasilimali za madini zinawanufaisha Watanzania kwa mapana zaidi.

Mavunde ametoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo iliyopokewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo, Profesa Mkumbo amesema wachimbaji wadogo ni sehemu muhimu ya sekta ya madini nchini, wakichangia takriban asilimia 40 ya mapato ya sekta hiyo na kutoa ajira kwa maelfu ya Watanzania, wakiwamo vijana na wanawake.

Hata hivyo, amesema wachimbaji hao bado wanakabiliwa na changamoto za mitaji, teknolojia, gharama kubwa za utafiti, upatikanaji mdogo wa taarifa za kijiolojia, masoko na huduma za kifedha.

Amesema ripoti hiyo ni muhimu kwa wakati huu, kwa sababu Serikali inaendelea kuweka mazingira yatakayosaidia wachimbaji wadogo kuongeza tija na hatimaye kukua kutoka uchimbaji mdogo hadi wa kati na mkubwa unaomilikiwa na Watanzania.

Kwa upande wake, Mavunde amesema Wizara ya Madini inaendelea kutekeleza Dira ya Madini 2030 “Madini ni Maisha na Utajiri,” inayolenga kuongeza eneo lililofanyiwa utafiti wa kina kutoka asilimia 16 ya sasa hadi kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.

Amesema Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (Stamico) na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), imeendelea kutoa huduma za utafiti na uchorongaji kwa wachimbaji wadogo, ikiwamo matumizi ya mitambo 15 ya kisasa.

Ripoti iliyozinduliwa imependekeza kuimarishwa kwa mifumo ya kifedha kwa wachimbaji wadogo, kuongeza ushiriki wa taasisi za fedha, kupanua upatikanaji wa taarifa za kijiolojia, matumizi ya teknolojia ya kisasa na kuimarisha masoko ya madini.

Pia, imependekeza kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Madini utakaosaidia wachimbaji wenye maeneo yenye uwezo lakini wasio na dhamana au mitaji kupata mikopo, pamoja na kuimarisha nyaraka za kitaalamu zinazohitajika kwenye taasisi za fedha.

Mavunde amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha uaminifu kati ya wachimbaji na taasisi za fedha kupitia elimu ya biashara ya madini, utunzaji wa kumbukumbu, uchimbaji salama na matumizi ya taarifa sahihi za kijiolojia.

Amesema pia Serikali inaendelea na hatua za kuboresha sekta hiyo ikiwamo uratibu wa uanzishwaji wa benki ya wachimbaji wadogo ili kuongeza upatikanaji wa mitaji na kuimarisha uchimbaji wenye tija.

Hatua hiyo inatarajiwa kuondoa uchimbaji wa kubahatisha na kuwezesha sekta ya madini kuchangia zaidi katika ukuaji wa uchumi wa Taifa kupitia uzalishaji wenye msingi wa taarifa, teknolojia na uwekezaji wa kisasa.