Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Samia atangaza msamaha wa viza kwa watalii wa Angola

Rais Tanzania, Samia Suluhu Hassan akipokelewa na mwenyeji wake Rais wa Angola João Manuel Gonçalves Lourenço mara baada ya kuwasili katika Ikulu ya Luanda leo Jumanne Aprili 8, 2025.

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan ametangaza kuwa Tanzania imetoa msamaha wa viza ya kitalii kwa raia wa Angola wanaotaka kutembelea nchini.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametangaza kuwa Tanzania imetoa msamaha wa viza ya kitalii kwa raia wa Angola wanaotaka kutembelea nchini humo.

Hatua hiyo inatajwa kuwa itaongeza tija katika sekta ya usafiri, uwekezaji na biashara kati ya mataifa hayo mawili.

Rais amesema hayo leo, Jumanne Aprili 8, 2025, baada ya majadiliano na Rais wa Angola, João Lourenço, ikiwa ni sehemu ya ziara hiyo inayolenga kukuza na kuimarisha zaidi mahusiano ya kihistoria na kindugu kati ya Tanzania na Angola.

“Nina furaha kutangaza juu ya msamaha wa viza ya kitalii kwa raia wa Angola wanaotaka kutembelea Tanzania,” amesema.

Rais Tanzania, Samia Suluhu Hassan akipokelewa na mwenyeji wake Rais wa Angola João Manuel Gonçalves Lourenço mara baada ya kuwasili katika Ikulu ya Luanda leo Jumanne Aprili 8, 2025.

Aidha, amebainisha kwamba wamekubaliana na Rais João Lourenço kuwa Julai 2025 atafanya ziara ya kiserikali nchini Tanzania, ili kuimarisha zaidi uhusiano wa nchi hizo mbili.

“Tumekubaliana mwaliko huu utakuwa Julai, atafanya ziara ya kiserikali sambamba na kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba yanayofanyika jijini Dar es Salaam,” amesema Rais Samia.

Amesema wamekubaliana kubadilishana maarifa na uzoefu katika sekta nyingine kama madini, mafuta na gesi, katika kutengeneza nafasi za ajira kwa vijana wa nchi hizo.

“Hata vyombo vyetu vya ulinzi vilivyopambania uhuru wa nchi hizi vimeendelea kuwa na uhusiano wa karibu, ambao umeanzishwa tangu harakati za uhuru,” amesema.

Amesema katika mazungumzo yao amemweleza kuhusu hali ya kisiasa na kiuchumi iliyopo Tanzania, huku wakijadili namna ya kuongeza ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, hasa eneo la kiuchumi.

Akizungumzia historia ya nchi hizo, Rais Samia amesema hata baada ya uhuru, nchi hizo zimeendelea kuwa na uhusiano wa karibu kama ilivyo sasa.

Amesema kwa sasa nguvu zinaongezwa kwenye kukuza jitihada za kupanua wigo wa kibiashara na uwekezaji kati ya mataifa hayo mawili.

Ziara ya Rais Samia inalenga kuendeleza uhusiano wa nchi hizo mbili ulioasisiwa na waasisi ambao ni hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, na hayati Rais António Agostinho Neto, waliokuwa na maono ya pamoja ya kuikomboa Afrika na watu wake.

Baadaye, Rais Samia atahutubia Bunge la Angola, kisha kesho, Jumatano, atahitimisha ziara yake kwa kutembelea kiwanda cha kusafisha mafuta cha Luanda Oil Refinery.

Rais Samia amealikwa na Spika wa Bunge la Angola, Carolina Cerqueira, amekuwa Rais wa kwanza mwanamke kutoka barani Afrika kuhutubia Bunge hilo.