Profesa Mkenda: Tuwajengee vijana ujuzi tuvutie uwekezaji

Muktasari:
- Kabla ya kampuni kuwekeza nchini moja ya jambo ambalo wanaangalia ni upatikanaji wa rasilimali watu mbali na kuwapo kwa sera zinazotabirika, usalama na amani pamoja na miundombinu inayochochea shughuli za uzalishaji.
Dar es Salaam. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema uwepo wa vijana wenye ujuzi wanaoweza kuajiriwa katika miradi ya uwezekaji unaofanywa na wageni ni moja ya jambo ambalo linaweza kuvutia wengi kuweka mitani yao Tanzania.
Profesa Mkenda amesema unapozungumzia mazingira mazuri ya biashara yanajumuisha mambo manne ambayo ni usalama wa nchi, uwekezaji katika miundombinu inayochochea shughuli za kiuchumi, sera na sheria zinazotabirika na rasilimali watu jambo ambalo halizungumzwi saba.
Ameyasema hayo leo Ijumaa ya Julai 12, 2024 katika mkutano wa mwaka wa wachumi uliofanyika jijini hapa akimuwakilisha Makamu wa Rais Dk Philip Mpango.
Profesa Mkenda amesema kampuni kama ya Apple inayozalisha bidhaa ambazo zinatumiwa na watu wengi wa pato la kati haziwekezi nchini China kwa sababu kuna nguvu kazi ya bei ya chini lakini zinawekeza huko kwa sababu kuna watu wenye ujuzi.
Amesema vitu vingi vinavyonunuliwa kutoka nje kama kompyuta na magari, kama nchi itahitaji uzalishaji huo ufanyike nchini haitoshi kuwavutia kwa msamaha wa kodi na sera zinazotabirika bali pia kuwapo kwa nguvu kazi.
“Hiyo ndiyo itafanya waje hapa kuwekeza kama ambavyo wanakimbilia nchini China, tukiwekea katika ujuzi itasaidia kuongeza uwekezaji kwa sababu wanajua pindi watakapoweka fedha zao watapata na watu wa kusaidia katika uzalishaji wa bidhaa zao,” amesema Profesa Mkenda.
Amesema hali hiyo itafanya watu wanapokuja kuwekeza Tanzania watakuwa na uhakika wa kupata wafanyakazi.
“Siyo wanakuja halafu wanaanza kutafuta wafanyakazi nje halafu wakienda ofisi ya kazi wanaambiwa waajiri watanzania…. ambao hawana ujuzi,” amesema Profesa Mkenda.
Amesema ni matumaini ya kila mtu kuona fursa zinapokuja nchini zisaidie kupunguza idadi ya vijana ambao hawana ajira katika maeneo ya mijini.
Amesema kama Serikali tayari imeshaanza kuchukua hatua kuhakikisha inazalisha nguvu kazi yenye ujuzi kwa kufanya mapitio ya mtaala kama ilivyokua agizo la Rais Samia Suluhu Hassan.
Mbali na mapitio hayo pia upo mkakati wa kujenga shule 100 za mkondo wa amali ambazo zitakuwa zikiwapika vijana ili wawe na ujuzi unaohitajika sehemu mbalimbali.
Akizungumza katika mkutano huo Mbunge wa Masasi Mjini, Godfrey Mwambe amesema wakati akifanya kazi Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kama mtu wa kutoa vibali vya ajira kwa wageni alikuwa akiumia kuona orodha ya watu wengi ambao wanapaswa kuajiriwa.
“Unakuta Wahindi watano, Wafaransa saba, unajiuliza kwamba hapa ndani hatuna watu wenye sifa unaambiwa kwa sifa hizi huwezi pata mhitimu kutoka Udom (Chuo Kikuu cha Dodoma) ana sifa hizo,” amesema Mwambe.
Akitoa mfano mwingine wa moja ya hoteli iliyopo jijini Arusha amesema kama nchi ilisaidia kujenga hadi ilipokamilika lakini ilipofika katika kuajiri Mkuu wa Kitengo cha masoko alikataliwa kupata kibali.
“Wakataka tumuambie (mmiliki) aajiri mtu wa kitengo hicho kutoka Tanzania, ikabidi nikae na Kamishna wa kazi. Mkuu wa kitengo cha masoko katika hoteli hiyo alitamiwa kuwa anaishi Marekani kutafuta wateja, wale Wazungu wanaokuja wametafutwa huko, sasa yule kamishna wa kazi anasema kuna watu wamemaliza UDOM, UDSM lakini huwezi,” amesema Mwambe.
Amesema hali hiyo inaonyesha kuwa vijana wengi wanaomaliza vyuo bado hawafikii vigezo vya soko hivyo ni vyema hatua zaidi zikaendelea kuchukuliwa ili kutomuongezea mwekezaji gharama za kumpatia mafunzo ili mwajiriwa mpya aweze kuendana na kile anachokitaka kwa sababu hakuwa amepikwa vizuri.