NBS yawabana wazalishaji wa takwimu nchini

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damasi Ndumbaro akipokea ripoti za utafiti wa sheria kutoka kwa Tume ya Marekebisho ya Sheria (LRCT) katika mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Muktasari:
- Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), imewataka wakusanya takwimu binafsi kuziwakilisha kwao kabla ya kuzitunza na kuzisambaza.
Dodoma. Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) imekabidhi ripoti ya utafiti ya Sheria ya Takwimu, lengo likiwa ni kuiwezesha Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kuweka mfumo utakaowezesha wazalishaji wote wa takwimu rasmi kuwasilisha takwimu zao katika ofisi hiyo.
Mwenyekiti wa LRCT, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Winfrida Korosso amesema hayo leo Jumatatu Machi 24, 2025 wakati wakikabidhi ripoti za utafiti kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro.
Pamoja na ripoti ya Sheria ya Taifa ya Takwimu, LRCT imekabidhi utafiti kuhusu mfumo wa sheria zinazosimamia vyama vya ushirika nchini.
Akizungumza kabla ya kukabidhi, Jaji Winfrida amesema mapitio ya Sheria ya Takwimu yalitokana na ombi la NBS yanayolenga kuwezesha kuwekwa kwa mfumo utakaowezesha wazalishaji wote wa takwimu rasmi kuwasilisha takwimu zao katika ofisi hiyo.
“Kwa sababu ofisi hiyo (NBS) ndio chombo chenye mamlaka ya kusimamia, kuratibu na kuhifadhi takwimu rasmi nchini na kurahisisha utaratibu ama mfumo wa upatikanaji wa takwimu kutoka kwenye mamlaka husika moja kwa moja,”amesema.

Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria (LCRT) Jaji wa Mahakama ya Rufani, Winfrida Korosso akizungumza wakati akiwasilisha ripoti za utafiti wa sheria katika Ofisi ya Wizara ya Katiba na Sheria katika mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Amesema mfumo huo ni badala ya njia inayotumika sasa ambayo kila mzalishaji wa takwimu rasmi, anazitunza na kuzisambaza bila kuziwasilisha NBS.
Jaji Winfrida amesema lengo la mabadiliko hayo ni kuifanya NBS kuwa chimbuko la takwimu zote hapa nchini, pia ndio inayoongoza na kutoa miongozo mbalimbali kuhusu takwimu rasmi za Serikali.
“Tume imebaini kuna changamoto za kisera, kisheria na kiutawala zinazochangia kukosekana kwa mazingira wezeshi ya uwasilishaji wa takwimu rasmi kwenye ofisi hiyo ambayo ndiye anasimamia kanzidata za Taifa, mratibu na msimamizi wa takwimu rasmi,”amesema.
Akizungumza baada ya kupokea ripoti hizo, Dk Ndumbaro ameiagiza tume hiyo kutengeneza utaratibu unaoeleweka wa utunzi na marekebisho ya sheria, ambao utatumika na kila mtu ambaye anataka kutunga ama kufanya marekebisho ya sheria nchini.
“Na katika utaratibu huo Tume ya Kurekebisha Sheria ndio anakuwa controller (mwongozaji), tusikilize maelezo ya wadau na mahitaji yao lakini tufanye utafiti, ulinganifu na sheria nyingine, nchi nyingine na mambo mengine ya Katiba na ndipo tutakuja na sheria,”amesema.
Amesema haipendezi Serikali kupeleka muswada bungeni unagonga mwamba na kurudi serikalini kwa sababu chombo cha kufanya utafiti wa sheria ambacho ni tume hakikutumika.