Prime
Mkongo unavyoipa jeuri TTCL katika biashara ya mawasiliano
Muktasari:
- Kwa mujibu wa Marwa, hata kampuni za simu ambazo ni washindani wake wa karibu, hutegemea mkongo wa TTCL kwa kiwango kikubwa ili kuwezesha huduma zao licha ya kuwa wakati mwingine wanakuwa na nguvu kubwa katika usambazaji.
Dar es Salaam. Wakati Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) linaonekana kutofanya vizuri sokoni katika huduma za simu, bosi wake ametaja kitu kinacholipa jeuri ya kuendelea kuwepo sokoni likiwa na matumaini ya kujiendesha kwa faida.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Moremi Marwa, anasema nguvu kubwa ya shirika hilo ipo kwenye mkongo wa taifa, ambao ndio uti wa mgongo wa mawasiliano ya kisasa nchini.
“Eneo ambalo tuna nguvu kubwa ni mkongo wa mawasiliano. Kwenye intaneti hakuna yeyote anayeweza kushindana na sisi kwa sababu tunamiliki mkongo wa taifa. Dunia sasa inaelekea kwenye mawasiliano ya kasi kupitia faiba na si redio,” anasema Marwa.
Anafafanua kuwa, tofauti na huduma za mawasiliano zinazotegemea redio, teknolojia ya faiba ina uwezo mkubwa wa kusafirisha data kwa kasi na kwa uhakika zaidi. Hivyo, wateja wanaotumia njia hiyo hupata uzoefu bora wa intaneti ukilinganisha na wale wanaotumia mitandao ya redio.
Kwa mujibu wa Marwa, hata kampuni za simu ambazo ni washindani wake wa karibu hutegemea mkongo wa TTCL kwa kiwango kikubwa, ili kuwezesha huduma zao, licha ya kuwa wakati mwingine wanakuwa na nguvu zaidi katika usambazaji.
“Hawa wengine wote wanakodisha kutoka kwetu iwe ni kwa miaka mitatu, mitano au hata kumi. Wanatumia huo mkongo kupeleka huduma kwenye minara yao na pia kuuza faiba kwa wateja wao,” anaeleza.
Katika kulinda na kupanua soko lake, TTCL imebadili mbinu ya utoaji huduma. Zamani walikuwa wanatumia teknolojia ya ‘point to point’, lakini sasa Marwa anasema wamehamia kwenye mfumo wa kisasa zaidi wa GPON (Gigabit Passive Optical Network).
Kupitia teknolojia hiyo, shirika linajenga miundombinu kwanza kabla ya wateja kujiunga, kinyume na ilivyokuwa awali ambapo mteja alipaswa kuomba huduma ndipo miundombinu ijengwe.
“Kwa mwaka huu hadi Juni tunatarajia kufikisha maunganisho 280,000. Mwaka ujao tunalenga 400,000 na baada ya hapo kufikia zaidi ya milioni 1.5,” anasema.
Anakiri kuwa sekta binafsi inaweza kuwa na kasi kubwa ya kusambaza huduma kutokana na nguvu ya mtaji, lakini TTCL sasa imejipanga kuhakikisha changamoto ya mtaji haizuii ukuaji wake.
Hata hivyo, alisema sehemu muhimu ya mkakati wa TTCL ni kusambaza huduma ya majumbani (FTTH), ambapo nyaya za faiba zinafikishwa moja kwa moja kwa wateja.
Kwa sasa, shirika linafanya utekelezaji wa awamu ya kwanza katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Arusha, Unguja, Mbeya, Mwanza na Iringa.
Ushiriki katika uchumi wa kidijitali
Moremi, ambaye amewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), anasema shirika hilo lina wajibu mkubwa katika kufanikisha uchumi wa kidijitali, jambo ambalo ni rahisi kwao kwa kuwa wanamiliki mkongo wa taifa, kituo cha data cha taifa na miundombinu mingine muhimu ikiwemo minara.
Anasema mchango wa TTCL katika uchumi wa kidijitali ni kuhakikisha kuna mtandao na mpaka sasa mkongo wa taifa umefikia mikoa yote na asilimia 82 ya wilaya zote nchini (wilaya 121 kati ya 139). Wanatarajia kuwa kufikia Desemba 2026 watakuwa wamefikia wilaya zote.
“Kufikisha mkongo wa taifa maana yake umewezesha kasi ya mawasiliano, kasi ya kupitisha data na kasi ya watu kupata huduma kwa haraka sana, ikiwemo elimu na hospitali, huduma ambazo zinahitaji intaneti isiyo na mkwamo,” alisema.
Anafafanua kuwa intaneti yenye kasi inatokana na teknolojia mbalimbali. Redio imefikia kwenye 5G na sasa watu wanaongelea 6G. Katika eneo hilo, wateja wanaweza kupata 5G kupitia ‘roaming’, lakini faiba ina kasi kubwa kuliko hata 5G ya redio.
Kuhusu mtandao wa uhakika nchini
Kuhusu usalama na uhakika wa mawasiliano ya kimataifa, Marwa anasema TTCL imejipanga kuhakikisha hakuna kukatika kwa huduma hata panapotokea hitilafu.
Alisema kwa sasa TTCL haina mpango wa kurusha satelaiti yake, isipokuwa Serikali, kutokana na maelekezo ya Rais, kupitia Wizara ya Mawasiliano inaandaa utaratibu wa kurusha satelaiti ya nchi. Pia, suala la nyaya za baharini si eneo la biashara wanayolifikiria kwa sasa.
Kutokana na mipango iliyotekelezwa, alisema hivi sasa kukatika kwa mawasiliano ya baharini (fiber cut) hakuwezi kuwa na athari kubwa, kwani kwa Dar es Salaam wamechukua mkongo kutoka kampuni tatu EASSy, SEACOM na 2Africa, ili mmoja ukikatika mawasiliano yapatikane kutoka kwa mwingine.
“Lakini mwaka jana tuliamua kuchukua mawasiliano kutoka Mombasa, ambapo kuna nyaya za mawasiliano baharini nane zinazoingia pale na kuunganishwa na mkongo wetu kupitia Horohoro, Tanga. Hii inahakikisha kwamba mawasiliano hayapotei hata kukiwa na hitilafu,” aliongeza.
Maono yake kwa TTCL
Anasema shirika linahitaji kufanyiwa mabadiliko, na hilo ndilo wanalofanya kwa sasa ili liweze kutoa huduma na kujiendesha kibiashara kwa kuweka mifumo endelevu hata akija kiongozi mwingine.
“Nikiondoka hapa nikaacha shirika linatoa huduma lakini linajiendesha kibiashara kwa muda mrefu, nitaona tumefanya mabadiliko mazuri. Shirika linapaswa kuongeza mapato na kupunguza matumizi ili liendelee kufanya vizuri,” alisema.
Alisisitiza kuwa TTCL inapaswa kuendelea kuwa kiwezeshi muhimu cha uchumi wa kidijitali, akisema ni miongoni mwa ajenda muhimu za mpango wa Taifa wa mwaka 2050 pamoja na mkakati wa Tanzania wa uchumi wa kidijitali.
Kuhusu madeni ya taasisi za Serikali, alisema ni sehemu ya kawaida ya biashara, lakini hayapaswi kuwa makubwa kiasi cha kukwamisha uendeshaji wa shughuli kwa sababu ya kutolipwa.
Aliongeza kuwa wanapobaini mteja anaenda kinyume na mkataba na mazungumzo yameshindikana, huchukua hatua ya kusitisha huduma. “Zipo nyingi tumezisitishia huduma za Serikali na hata za kampuni binafsi,” alisema.