Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mchele wa Mbeya hatarini kupoteza soko

Muktasari:

Yaelezwa ni kutokana na mafuta kuupunguzia sifa kimataifa.

Mbeya. Wakati wafanyabiashara wengi wa mchele nchini wakiunadi wa Mbeya kwa ubora, hususan ule wa wilayani Kyela, wataalamu wa ubora wa vyakula wamesema uko hatarini kukosa soko la kimataifa kutokana na kupakwa mafuta.

Mchele huo unadaiwa kupakwa mafuta ya alizeti katika mazingira machafu kwa kutumia miguu kuuchanganya kwenye chumba ambacho mazingira yake ni hatari.

Mtalaamu wa usindikaji wa nafaka kwa kuzingatia ubora wa bidhaa za Tanzania, Ladislaus Ikombe kutoka Taasisi ya Staple Value Chain Activity inayoshughulika na kilimo cha mazao ya nafaka chini ya udhamini wa Usaid, alisema juzi kuwa mchele mwingi nchini unachafuliwa baada ya kukobolewa kwa kuupaka mafuta kwa kutumia miguu na kuuweka kwenye vifungashio duni.

Ikombe alisema katika viwanda vingi vya kukoboa mchele mkoani Mbeya, huumwagia mafuta yanayodaiwa kuwa ya kula, tofauti na kanuni za usindikaji bora wa vyakula na kuzingatia afya ya walaji. “Wenye mchele wanadai wanaweka mafuta kwa ajili ya kuung’arisha na kuondoa ukungu, lakini kitendo hicho ni cha hatari kwa vile mchele ukipimwa ili uingie soko la kimataifa unaweza kukosa sifa kwa vigezo vingi, ikiwamo kuonekana kwa mafuta yasiyo ya kawaida,” alisema.

Alisema usindikaji bora wa nafaka za kuuza nje ya nchi lazima uzingatie masuala ya afya na uwe na maelezo ya ubora pamoja na vifungashio vyake kuonyesha lini ulifungwa, ubora wake, utadumu muda gani bila kuharibika na anwani ya wazi kwa wanaoweza kulalamikia ubora.

Mmoja wa wauzaji wa mchele katika Soko la Sido mjini hapa, Rose Tweve alikiri kuwapo tabia ya kupaka mafuta mchele iliyoanza kwa matakwa ya wateja wanaotoka Pemba na Somalia.

Naye Jabir Mwakisole ambaye ni muuzaji wa mchele alithibitisha kuwa hupaka mafuta mchele kwa lengo la kuung’arisha na kuuondolea vumbi.

Katibu wa Wamiliki wa Viwanda Vidogo vya Kukoboa Mpunga jijini Mbeya, Julius Ngallawa alisema wanaamini upakaji mafuta mchele ni uchafu na walishapiga marufuku tabia hiyo.

Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Rodney Alananga alisema ni makosa kupaka mafuta mchele.

Alananga alisema mamlaka hiyo inakabiliwa na upungufu wa wafuatiliaji wa mazingira na ubora wa vyakula.