Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Makali ya bei za mafuta duniani kuendelea kwa siku zaidi 

Muktasari:

  • Bei za mafuta duniani tayari zimepanda kwa zaidi ya asilimia 25 tangu vita hivyo kuanza, hali inayosababisha gharama za mafuta kupanda kwa watumiaji duniani

Dar es Salaam. Vita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran vinaweza kusababisha bei za mafuta kupanda kwa muda mrefu zaidi duniani, hata kama mzozo huo uliodumu kwa wiki moja utamalizika haraka, kutokana na uharibifu wa miundombinu, kuvurugika kwa usafirishaji na hatari kubwa kwa meli zinazobeba mafuta.

Matarajio hayo yanaweka shinikizo kwa uchumi wa dunia na pia yanaweza kuwa changamoto ya kisiasa kwa Rais wa Marekani, Donald Trump hasa kuelekea uchaguzi wa katikati ya muhula, wakati wapigakura huwa makini kwenye gharama za nishati na mara nyingi hupinga kuhusika kwa nchi yao katika migogoro ya nje.

Kwa mujibu wa Reuters, wachambuzi wa Benki ya Uwekezaji JPMorgan Chase wamesema katika ripoti ya utafiti Ijumaa iliyopita kuwa, soko la mafuta sasa linaanza kukabiliana si tu na hatari za kisiasa bali pia na athari halisi za kiutendaji.

“Soko linaondoka kwenye kukadiria hatari za kisiasa pekee na sasa linakabiliwa na usumbufu wa moja kwa moja wa shughuli huku kufungwa kwa baadhi ya mitambo ya kusafisha mafuta na vikwazo vya usafirishaji vikianza kuathiri uchakataji wa mafuta ghafi na mtiririko wa usambazaji wa kikanda,” wachambuzi hao wamesema.

Mzozo huo tayari umeathiri takribani asilimia 20 ya usambazaji wa mafuta ghafi na gesi asilia duniani, baada ya Iran kulenga meli katika Mlango Bahari wa Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji wa nishati kati ya pwani zake na Oman, pamoja na kushambulia miundombinu ya nishati katika eneo hilo.

Bei za mafuta duniani tayari zimepanda kwa zaidi ya asilimia 25 tangu vita hivyo kuanza, hali inayosababisha gharama za mafuta kupanda kwa watumiaji duniani.

Kufungwa karibu kabisa kwa Mlango Bahari wa Hormuz kumelazimisha wazalishaji wakubwa wa mafuta wa Saudi Arabia, Falme za Kiarabu (UAE), Iraq na Kuwait kusitisha usafirishaji wa hadi mapipa milioni 140 ya mafuta, sawa na mahitaji ya dunia kwa takribani siku 1.4.

Kutokana na hali hiyo, hifadhi za mafuta na gesi katika vituo vya Ghuba ya Mashariki ya Kati zinaanza kujaa haraka na kulazimisha baadhi ya visima vya mafuta nchini Iraq na Kuwait kupunguza uzalishaji. Wachambuzi wamesema huenda UAE nayo ikafuata hatua hiyo.

“Muda si mrefu kila mtu atalazimika kusimamisha uzalishaji ikiwa meli hazitafika kuchukua mafuta,” kimesema chanzo kimoja kutoka kampuni ya mafuta inayomilikiwa na Serikali katika eneo hilo, kama kilivyonukuliwa na Reuters.

Kwa mujibu wa Amir Zaman wa kampuni ya utafiti wa nishati ya Rystad Energy, visima vya mafuta vitakavyolazimika kufungwa katika Mashariki ya Kati kutokana na kuvurugika kwa usafirishaji vinaweza kuchukua muda kurejea katika uzalishaji wa kawaida.

Ikulu ya Marekani imehalalisha mashambulizi dhidi ya Iran kwa kusema nchi hiyo ilikuwa tishio la haraka kwa Marekani, ingawa haijatoa maelezo ya kina. Rais Trump pia amesema ana wasiwasi kuhusu juhudi za Iran kutafuta silaha za nyuklia.


Hatari iliyopo Hormuz

Kumalizika kwa haraka kwa vita kunaweza kutuliza masoko ya nishati, lakini kurejea kwa usambazaji na bei katika viwango vya kabla ya vita kunaweza kuchukua wiki au hata miezi, kutegemea na kiwango cha uharibifu wa miundombinu na usafirishaji.

“Kwa sasa hatujaona uharibifu mkubwa wa kudumu katika miundombinu kutokana na mashambulizi ya Iran, ingawa hatari bado ipo kadiri vita vinavyoendelea,” amesema Joel Hancock, mchambuzi wa nishati wa Natixis Corporate & Investment Banking.

Swali kubwa kwa sasa ni lini na kwa kiwango gani mlango Bahari wa Hormuz utakuwa salama tena kwa usafirishaji wa meli za mafuta. Trump ameahidi kutoa ulinzi wa kijeshi kwa meli za mafuta pamoja na msaada wa bima ya Marekani kwa meli zinazopita katika eneo hilo.

Hata hivyo, wataalamu wa kijeshi na kiintelijensia wanasema usalama katika njia hiyo muhimu ya majini unaweza kuwa mgumu kupatikana kwa haraka, kwa kuwa Iran ina uwezo wa kuendeleza mashambulizi ya ndege zisizo na rubani dhidi ya meli kwa miezi kadhaa.

Aidha, mgogoro huo unaweza kuzisukuma nchi mbalimbali kuongeza akiba zao za kimkakati za mafuta baada ya vita kuisha, hatua itakayoongeza mahitaji ya mafuta duniani na kuendelea kuhimiza bei kupanda.