Bei ya mafuta ilivyochochea matumizi ya gesi asilia kwenye magari
Muktasari:
- Kwa sasa, kituo cha kujaza gesi asilia kwenye magari kinachomilikiwa na TPDC kinajaza kwenye magari wastani wa futi za ujazo milioni 2.3 za gesi asilia kwa siku, kutoka futi za ujazo milioni 1.3 zilizokuwa zikitolewa kabla ya kupanda kwa bei za mafuta katika soko la dunia.
Dar es Salaam. Kuongezeka kwa idadi ya Watanzania wanaohamia kwenye matumizi ya gesi asilia iliyoshindiliwa (CNG) kama mbadala wa petroli, kumechochea kituo cha Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) cha kujaza gesi kushuhudia ongezeko kubwa katika kuhudumia magari.
Kwa sasa, kituo hicho kinajaza kwenye magari wastani wa futi za ujazo milioni 2.3 za gesi asilia kwa siku, kutoka futi za ujazo milioni 1.3 zilizokuwa zikitolewa kabla ya kupanda kwa bei za mafuta katika soko la dunia.
Pia, idadi ya magari yanayohudumiwa imeongezeka kutoka takribani magari 500 hadi karibu magari 1,000 kwa siku, jambo linaloonesha mwitikio mkubwa wa wananchi katika kutumia nishati hiyo mbadala kutokana na gharama zake kuwa nafuu.
Akizungumza jana Julai 9, 2026 katika Maonyesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), mhandisi wa mitambo wa Kampuni ya Gasco, Daudi Enock inayosimamia uendeshaji na matengenezo ya miundombinu ya CNG ya TPDC, amesema mahitaji ya gesi hiyo yameongezeka kwa kasi katika miezi ya hivi karibuni.
“Zamani tulikuwa tunahudumia takribani magari 500 kwa siku, lakini sasa tunapokea karibu magari 1,000 kila siku. Matumizi yameongezeka kutoka futi za ujazo milioni 1.3 hadi milioni 2.3 kwa siku, hali inayokifanya kituo hiki kukaribia uwezo wake wa juu,” amesema Enock.
Amesema ongezeko hilo limechangiwa na kupanda kwa bei za mafuta duniani, kuongezeka kwa kampuni zinazobadilisha magari kutumia CNG na hatua ya Serikali kuondoa baadhi ya kodi kwenye vifaa vya kubadilisha mifumo ya magari kutoka petroli kwenda gesi.
Kuanzia Julai mosi 2026, Serikali ilianza kutoa vivutio mbalimbali vya kikodi katika sekta ya gesi na umeme, ikiwamo msamaha wa kodi kwenye vifaa vinavyotumika kubadilisha magari kutoka mfumo wa matumizi ya mafuta kwenda matumizi ya gesi na umeme, pamoja na vifaa vya miundombinu ya gesi.
Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi na mbadala nchini, huku ikipunguza utegemezi wa mafuta yanayoagizwa kutoka nje ya nchi.
Meneja wa banda la TPDC katika maonyesho hayo, Hassan Temba amesema gesi asilia imeendelea kuwa nafuu licha ya mabadiliko ya bei ya mafuta katika soko la dunia.
“Kabla ya matukio ya hivi karibuni ya Mashariki ya Kati, petroli ilikuwa ikiuzwa kwa takribani Sh2,800 kwa lita, lakini sasa imefikia zaidi ya Sh4,100 kwa lita. Wakati huohuo, gesi asilia inaendelea kuuzwa kwa wastani wa Sh1,550 kwa kilo,” amesema Temba.
Kwa mujibu wa TPDC, gari lenye injini ya ukubwa wa CC1,500 linaweza kusafiri kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma kwa kutumia kilo 11 za gesi asilia inayogharimu takribani Sh17,000, ikilinganishwa na zaidi ya Sh50,000 zinazohitajika kwa safari hiyo hiyo kwa kutumia petroli.
Temba amesema hadi sasa zaidi ya magari 15,000 nchini tayari yamebadilishwa na kutumia CNG, huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka zaidi kufuatia uamuzi wa Serikali wa kuondoa kodi kwenye vifaa vya kubadilisha magari kutumia gesi asilia katika Bajeti ya mwaka 2026/27.
Amesema pia idadi ya kampuni zinazotoa huduma za ubadilishaji wa magari imeongezeka kutoka kampuni moja au mbili miaka michache iliyopita hadi zaidi ya 15 hivi sasa, hatua inayorahisisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi.
Kutokana na ongezeko la mahitaji, TPDC inaendelea kupanua miundombinu ya CNG nje ya Dar es Salaam kwa kujenga vituo katika mikoa ya Morogoro, Dodoma, Tanga, Kilimanjaro na Arusha.
Katika hatua za awali, gesi hiyo itasafirishwa kwa kutumia malori maalumu kabla ya kufikishwa kwenye miundombinu ya mabomba katika maeneo hayo.
Licha ya ongezeko la mahitaji, Temba amesema Tanzania ina akiba ya kutosha ya gesi asilia kuhimili ongezeko la matumizi.
“Tuna gesi ya kutosha kukidhi mahitaji. Kipaumbele chetu sasa ni kupanua miundombinu ili Watanzania wengi zaidi waweze kupata nishati hii nafuu,” amesema.
Mmoja wa wananchi, Neema Lazaro amesema maonyesho ya mwaka huu yamekuwa fursa ya kuona teknolojia na ubunifu mbalimbali unaofanyika nchini.
“Tunatarajia kuona ubunifu zaidi na bidhaa nyingi zinazoweza kutatua changamoto za wananchi na kupunguza gharama za maisha,” amesema.