Shilole atoa somo kwa vijana

Muktasari:

  • Shilole ameeleza kuwa wakati anatoa wimbo huo mwaka 2013, kuna mambo mengi yalikuwa yakizungumzwa dhidi yake ambayo ameyaimba kwenye wimbo huo

Dar es Salaam, Mwanamuziki na mwigizaji Zuwena Mohamed ‘Shilole’ amefunguka kuwa alichoimba kwenye wimbo wake uitwao ‘Nakomaa na Jiji’ ulikuwa na uhalisia wa aliyokuwa akipitia kipindi hicho.

Shilole ameeleza kuwa wakati anatoa wimbo huo mwaka 2013, kuna mambo mengi yalikuwa yakizungumzwa dhidi yake ambayo ameyaimba kwenye wimbo huo.

“Wakati natoa ‘Nakoma na Jiji’ mengi yalikuwa yakizungumzwa, wengi walisema nirudi kwetu Igunga kwa sababu huu mji nimeushindwa, nilichoimba kwa wakati huo ulikuwa ni ukweli mtupu ilifika kipindi nilikuwa ninazungumza na Mungu wangu tu, yatima mimi ambaye kutafuta sijachoka, Mungu alinijalia sikuweza kuanguka,”ameeleza

Hata hivyo, ameeleza kuwa kutokana na hali ilivyokuwa kwa kipindi hicho hakuna aliyeweza kuamini kama angeweza kufungua mgahawa wa chakula.

“Nani aliamini kwa kipindi kile nitaweza kufungua migahawa ya chakula mkubwa na kufanya vizuri kila kona. Jiulize ni watu wangapi maarufu walianzisha biashara na wakashindwa kusimamia?",ameeleza. 

Aidha kutokana na hayo ametoa somo kwa vijana kujitahidi kuwa watu wema na kuachana na dhana ya kuwa mtu mwenye makalio makubwa ndiye kafanikiwa.

“Kwa wadogo zangu, na watoto wangu, nani aliwadanganya kuwa na makalio makubwa ndiyo kufanikiwa? nani aliwadanganya kufanya mambo ambayo hayampendezi maulana ndiyo kufanikiwa?”, ameeleza na kuongezea. 

“Somo langu kubwa kwa wadogo zangu na watoto wangu, hii dunia imejaa kila aina ya watu jitahidi uwe moja kati ya watu wema, uwe hadithi nzuri siku ukiondoka, mimi ni hamasa kwa kundi kubwa la Wanawake wenye ndoto wale wanaopitia magumu sana, Wale wanaotoka hali ya chini sana,” ameeleza.