Nyimbo za Kabaka ni darasa tosha la muziki

Kati ya wanamuziki maarufu ambao waliteka masikio ya wapenzi wa muziki wa Kenya katika miaka ya 60 ni Daudi Kabaka Masika, maarufu kama Mtoboa Siri kutokana na tungo zake zilizokuwa na vituko vya kusema ukweli.

Daudi kabaka alizaliwa Kyambogo Uganda mwaka 1939. Baba yake alimpa jina la Daudi Kabaka kutokana na jina la Kabaka Daudi Chwa aliyekuwa mfalme wa Wabaganda aliyefariki mwaka 1939. Mwaka 1950, Daudi alihamia Nairobi kumfuata baba yake aliyekuwa mfanya kazi wa shirika la reli na akajiunga na shule ya msingi ya St. Peter Clavers Primary Alipokuwa na umri wa miaka 12 baba yake akawa anaishi jirani na vijana waliokuwa na magitaa hapo ndipo akaanza kupata elimu yake ya muziki iliyokuja kumfanya aje kujulikana Afrika ya Mashariki yote. Kabaka alijifunza gitaa na miaka miwili tu baadae akiwa na umri wa miaka 14 alirekodi wimbo wake wa kwanza  ulioitwa Mie Kabaka Naimba.  Mwaka  1959 alianza kufanya kazi Equator Sound Studio na muda si mrefu akawa mwanamuziki wa  bendi ya studoi iliyoitwa Equator Sound Boysambayo ilikuwa na mabingwa wengine kama Nashil Pichen, David Amunga, Charles Sonko, Frida Sonko, na Fadhili William.  

Sauti ya Daudi Kabaka na gitaa lake vilisikika katika nyimbo maarufu kama Malaika na Taxi Driver za Fadhili William, Pole Musa akiwa na Peter Tsosi na Nashil Pichen, na alikuwemo pia katika wimbo maarufu wa Lunch Time wa marehemu Gabriel Omolo.

Daudi Kabaka alitunga nyimbo nyingi sana za twist kiasi cha kupewa sifa ya kuitwa Mfalme wa Twist. Siku moja aliwahi kusema  wimbo wa Mmarekani Chubby Checker  Let's Twist Again, ndio uliomfanya aanze kutunga nyimbo kwa mtindo huo.  Kati ya nyimbo zake za twist zilizokuwa maarufu sana ni Bushbaby Twist ambapo aliimba akisema hata wanyama wa mwituni wanapenda kucheza twist, pia alitunga African Twist, Bachelor Boy TwistTaita Twist na nyinginezo nyingi. Twist ulikuwa ndio mtindo wa vijana katika miaka ya sitini na ulionekana ni mtindo wa uchezaji wa kihuni ambao ulisababisha vijana wengi kupata adhabu kwa kukutwa wanacheza twist.Hakika Kabaka alikuwa na nyimbonyingine nyingi ambazo hazikuwa twisti na kati ya hizo nyimbo,kama Ambulance Mlangoni, Sisi wanaume, Msichana wa sura nzuri zilikuwa zikiongea mambo ambayo yalikuwa si rahisi kuongea hadharani na hivyo kumpa jina la Mtoboa Siri

Wimbo wa Kabaka ulioitwa Haramba Harambe ulikuwa maarufu sana Kenya kwani ulikuwa kama wimbo wa vijana wakisifia Taifa lao na kwa miaka mingi ulipigwa kila siku katika redio ya Taifa hilo na kujulikana na kila mtu.  Mwaka 1967 kundi la Uingereza la The Tremeloes lilichukua kipande cha kibwagizo cha wimbo Helule Helule wa Daudi Kabaka, na kuurekodi, wimbo huo ukapata umaarufu na kufikia namba 14 katika Top Ten za Uingereza, miaka mingi baadae Kabaka alisema hakupata hata senti kutokana na mirabaha ya mauzo ya wimbo huo, japo alipewa fedha za awali kwa ajili ya kutumia tu wimbo huo.

Mwaka 1972 Kabaka na wenzie wakaiacha Equator Sound na kuanzisha kampuni yao ya muziki walioiita African Eagles Recording, Ltd, wakaunda bendi ya studio waliyoiita African Eagles Lupopo ambayo pamoja na kutoa nyimbo kadhaa ilifanya ziara katika nchi za  Zambia, Malawi na Uganda.  African Eagles Recording, Ltd hatimae ikafa na Daudi aliamua kupumzika kidogo. Kutokana na uzoefu wake wa miaka mingi katika muziki  mwaka 1995, Chuo Kikuu cha Kenyatta, kilimtunukia mkongwe huyu tuzo ya  Kenyatta University's Distinguished Service Award.  Na kutokana na historia yake, Kabaka alipata kazi ya kufundisha kama Creative Arts instructor katika chuo hicho kwa miaka kadhaa iliyofuata. Kabaka alipata tena ari ya kufanya maonyesho akawa anafanya maonyesho kadhaa na wakongwe wenzie akina Fadhili William, John Nzenze katika onyesho waliloliita Oldies Nite. Kabaka pia akaanzisha kundi lililokuwa na vijana wadogo aliloliita Wazalendo Eagles Band.  Urithi wa Kabaka unaendelea hata hapa kwetu Tanzania,bendi kadhaa bado zinapiga nyimbo za Daudi Kabaka jukwaanina watu bado wanaendelea kufurahia tungo za mkongwe huyu.

Kwa mwanamuziki mtunzi au anaetaka kujifunza kutunga moja ya shulenzuri ni kusikiliza nyimbo za Kabaka kuanzia miaka ya 50 mpaka kifo chake. Alitoa mafunzo, ushauri, alichekesha, alifundisha uzalendo, na nyimbo zake ziliwezakusikilizwa na kuchezwa na watu wa rika zote bila kuwa na ukakasi.

Daudi Kabaka alifariki tarehe 26 Novemba 2001 zikiwa zimebaki siku mbili aweze kutimiza umri wa miaka 62. Akazikwa  nyumbani kwake Muhudu, Tiriki Magharibi ya Kenya tarehe 15 Disemba 2001. Inasemekana mzee alifariki akiacha watoto 47.