Dully Sykes na Bongo Fleva

Muktasari:

  • Wengi walitoweka kimuziki kwa tabia mbaya na kutojitunza kisanaa. Wakajali muonekano na sauti. Wakasahau moyo safi. Heshima. Na nidhamu ya kazi

Dar es Salaam, Ni mtoto wa mjini tena siyo wa kuiga. Kazaliwa Ilala na kukulia Ilala. Utu uzima akiupatia mitaa ya Mnazi Mmoja. 
 
Wengi walitoweka kimuziki kwa tabia mbaya na kutojitunza kisanaa. Wakajali muonekano na sauti. Wakasahau moyo safi. Heshima. Na nidhamu ya kazi.
 
Dully  Sykes anazeeka na game. Kwake sauti ni dili ndiyo maana hajaichosha kwa moshi na pombe. Ushasikia msanii fulani akimlalamikia Dully? Kwa kazi? 

Ukiweza iga tabia zake na siyo kunyoa kiduku au kuvaa vipuri kama yeye. Kwake muonekano ni biashara na tabia ni silaha. Dully ni baba wa familia tangu na tangu.
 
Anakuonesha kuwa muonekano na tabia kwake ni Simba na Yanga. Haviendani kamwe. Alikiba, Blue, Benz na wasanii wengi wenye makuzi ya Ilala na Kariakoo. Wamepita katika mikono ya Dully…
 
Kipaji ni jambo moja. Kujisimamia ni jambo lingine kubwa zaidi. Vijana wa umri wake wengi walipotea kwa dawa za kulevya na ulevi mwingine.

Unachotakiwa kujua Dully aliyeupenyeza muziki huu unaowapa pesa kina Mondi, katikakati ya muziki wa kufokafoka (hip hop). Akiitwa mwanasesere na majina mengi ya dhihaka. Akakomaa nao.
 
Dully kafika hapo siyo kwa bahati mbaya. Anastahili heshima…