Robertinho: Kwanini Kibu tu?

LEO kwenye muendelezo wa mahojiano na kocha wa Simba, Robert Oliveira ‘Robertinho’ anaendelea kuchimba mambo mbalimbali ndani ya timu hiyo lakini kuna historia ya nyuma anatukumbushia alipoanza ukocha.


KUHUSU SAMBA LOKETO

Soka ambalo Simba inalicheza tangu aje Robertinho limepewa jina la Samba Loketo na anaeleza maana ya hilo jina na muunganiko wake.

“Unajua sisi Wabrazil tunaamini kuwa timu yako inapokuwa na mpira hakuna tatizo litakalokupata kutoka kwa wapinzani, kama una kipaji haitakuwa ngumu kwenu kuwa na umiliki mzuri wa mpira, neno samba ni kutoka kwetu Brazil tukiamini kwamba unapopiga pasi moja au mbili kisha mkafanya kwa timu yenu mzima hiyo sio samba.

“Nafurahi kuona hata wachezaji wangu hapa Simba nao wanacheza samba lakini hili Loketo sijui maana yake na sijui kwanini walikuja kuongeza hili neno,” anaeleza Robertinho huku akicheka.


KWANINI KIBU?

Baadhi ya mashabiki wa Simba wamekuwa hawakiamini moja kwa moja kiwango cha mshambuliaji wao Kibu Denis lakini Robertinho hakubaliani nao.

“Huwa naona watu wanakasirika kuhusu Kibu lakini ukiwa kocha huwezi kufanya uamuzi kwa makelele ya mashabiki, tunaheshimu mashabiki wetu kwa kuwa tunafanya kazi kwa ajili yao, mimi kama kocha najua mchango wa Kibu.

“Nitakwambia mfano mzuri, angalia nidhamu ya beki wetu wa kulia Shomari Kapombe mara nyingi ndio mtu anayepanda juu na kutengeneza krosi nyingi sijui kama watu wanaona Kibu anavyorudi kuja kuziba pale Kapombe anapoondoka.

“Ukiacha hilo Kibu ana nguvu ya kupanda na kurudi kuja kusaidia katikati lakini pia ana uwezo wa kupiga mashuti, hiki ndio tunapambana nacho sasa kuhakikisha awe anapiga mashuti, yatatumiwa na kina Baleke na wengine. Kitu ambacho tunakazana kukiondoa sasa ni kupunguza presha huwa anapoteza kujiamini kwa kuwa mashabiki wamekuwa wakimuandama, unajua Kibu ni kijana mdogo,” anasema.


AMEKUTANA NA SHIDA YA NIDHAMU SIMBA?

“Nadhani sasa hali iko vizuri juu ya nidhamu sijakutana na hiyo changamoto ya nidhamu kwa wachezaji, namshukuru Mungu, nidhamu kwangu mimi ni sawa na kuwa profeshno, ukiwa profeshno una nafasi kubwa ya kuwa na nidhamu kwa kuwa utakuwa umefuata misingi yote ya mambo ambayo unatakiwa kuyafanya kwa wakati, ukiwa huna nidhamu wewe sio profeshno.”

“Tunatumia muda wa saa moja na nusu kwenye uwanja wa mazoezi, nadhani huwa mnakuja mnaona, tukiwa pale hakuna mambo ya kuchekeana ni kazi tu, tunafanya mazoezi kwa jumla ya saa saba au sita na zaidi lakini kwenye mechi tutacheza kwa saa moja na nusu pekee kwahiyo muda mwingine tutautumia kupumzika na kufurahi lakini mazoezini ni sehemu ya kazi.”


KUCHEZA NA ROMARIO YULE MWENYEWE

Wengi hawajui hili. Kuna mtu anaitwa Romario de Souza Faria pale Brazili. Kwa sasa ni Mwanasiasa lakini ametamba sana kwenye soka la nchi hiyo mpaka kuweka rekodi duniani. Alikuwa straika aliyefunga zaidi ya mabao 700 na ni miongoni mwa mastaa wachache duniani kutupia mabao 100 ndani ya muda mfupi akiwa na klabu tatu tofauti.

Sasa msikie Robertinho; “Mimi nimecheza na Romario katika dakika za mwisho za uchezaji wangu, Romario alikuwa anacheza kama mshambuliaji na mimi nikiwa winga bahati mbaya sikucheza naye sana nikaacha na kwenda kusomea ukocha, nakumbuka mwaka 2002 aliyekuwa kocha wa timu ya taifa ya Brazil, Scolari (Philippe) alimuacha Romario katika kikosi cha taifa kikiwa kinakwenda katika Kombe la Dunia na badala yake akaenda Ronaldinho.

“Uamuzi ule ulitushtua wengi na raia wakamwambia akienda ole wake asirudi na kombe, unajua watu tulikuwa tunampenda sana Romario, sawa Ronaldinho alikuwa na kipaji kikubwa lakini tuliamini kwamba bado hajakomaa kwenda kutupa mafanikio bahati nzuri walichukua ubingwa na mimi mwaka huohuo nilikuwa naifundisha Fluminense.

“Tulitwaa ubingwa wa ligi na Fluminense tukaanza maandalizi ya kwenda kucheza mashindano makubwa ya Copa Libertadores (ambayo ni sawa na Ligi ya Mabingwa) kwa bara la America, nikiwa pia nimechukua zawadi ya kocha bora wa ligi, baada ya hapo rais wa klabu wakati huo akanifuata na kuniambia kwanza wanataka kuniongeza mkataba tukakubaliana na kuongeza.

“Baadaye akaniambia anataka kuiongezea timu nguvu kwa kumleta mchezaji mkubwa mwenye uzoefu, aliponiambia Romario nikasema sawa kwa kuwa nilikuwa namjua kwa kucheza naye, nakumbuka siku ya kwanza Romario anakuja kufanya mazoezi kwa mara ya kwanza uwanja ulijaa mashabiki kama zaidi ya elfu sita kuja tu kumuona Romario.

“Nikasema kwa uamuzi wa Romario nikaamua kumpa unahodha wa klabu kabisa ili awaongoze vizuri vijana wengine ambao walifurahi sana kucheza naye, tulipocheza mchezo wetu wa kwanza wa mashindano hayo makubwa pale Maracana uwanja mzima ulijaa tulishinda 3-0 na mabao yote alifunga Romario, sasa alipofunga bao la tatu alinifuata na kunipiga busu mashavuni mara tatu akaniambia kila busu ni zawadi kwangu kwa kukubali aje ajiunge na timu, hii ni historia kubwa kwangu ambayo sio rahisi kuja kuisahau.”