Chombo cha kusimamia miundombinu ya michezo kuanzishwa

Muktasari:
- Katika kukabiliana na changamoto ya miundombinu ya michezo nchini, Serikali imekuja na mwarobaini wa kukabiliana na hilo.
Serikali imeanza mchakato wa kuanzisha chombo maalumu cha usimamizi wa miundombinu ya michezo katika kukabiliana na changamoto za uendeshaji wa miundombinu ya michezo nchini.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi leo Mei 7, 2025 wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara yake kwa mwaka 2025/26.
Profesa Kabudi amesema chombo hicho kitakuwa na mamlaka ya kusimamia uendeshaji, ukarabati na matunzo ya miundombinu yote ya michezo nchini.
“Hivyo, ni matumaini yetu kwamba kuwapo kwa chombo hiki kutapunguza changamoto za usimamizi wa miundombinu na kutaongeza thamani ya miundombinu ya michezo nchini,” amesema Profesa Kabudi.
MAANDALIZI YA AFCON 2027
Wakati Tanzania itaandaa fainali za soka za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 kwa kushirikiana na Kenya na Uganda, Profesa Kabudi amesema kuwa wizara imeendelea na ukarabati mkubwa wa Uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo ukarabati huu umejumuisha maeneo ya vyumba vya wachezaji (dressing rooms) na maeneo ya waandishi wa habari (media tribune and press conference).
“Maeneo mengine ni kufunga viti vipya na kuondoa vya zamani ambapo hadi kufika Aprili 2025 jumla ya viti 40,000 vimewasili na vinaendelea kufungwa. Kukarabati eneo la mchezo wa riadha kwa kuondoa na kuweka taa mpya,” amesema.
Ametaja maeneo mengine yanayokarabatiwa ni mifumo ya viyoyozi, mifumo ya mtandao wa intaneti, mifumo ya majitaka ikiwamo vyoo, kupaka rangi sehemu mbalimbali na kuondoa na kufunga taa mpya ambapo jumla ya taa 352 zimefungwa.
Mengine ni kuondoa na kufunga milango mipya, kukarabati jukwaa la viongozi na kuondoa na kupanda nyasi mpya sehemu ya kuchezea.
Profesa Kabudi amesema kwa ujumla ukarabati wa uwanja huu umefikia asilimia 80.
Kuhusu Uwanja wa Uhuru, Profesa Kabudi amesema ukarabati mkubwa wa uwanja huo umefikia asilimia saba.
Amesema maboresho yanayofanyika katika uwanja huo yanajumuisha eneo la kuchezea (pitch), kuweka viti, mfumo wa maji, mfumo wa umeme, Tehama na upakaji rangi.
“Ujenzi na ukarabati wa viwanja hivi haulengi tu mashindano ya AFCON 2027 na CHAN 2024, bali una faida kubwa kwa Taifa letu katika maeneo mbalimbali. Uimarishaji wa miundombinu ya michezo utasaidia kuendeleza vipaji vya vijana wetu,” amesema.
Amesema wanapokuwa na viwanja bora na vya kisasa, vijana wetu wanapata fursa ya kufanya mazoezi katika mazingira salama na ya kisasa jambo litakalosaidia kukuza vipaji vyao.