Prime
Fadlu atoa amri kambini kukwepa vita nje ya uwanja

Muktasari:
- Simba itavaana na Berkane kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Manispaa ya Mji wa Berkane, ikiwa ni mechi ya mkondo wa kwanza wa fainali hiyo kabla ya kuja kurudiana nao wiki ijayo kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar uliotangazwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) badala ya Kwa Mkapa.
SIMBA imeingia siku ya tatu ikiwa Morocco, ikianza kwa kutua Jiji la Casablanca kisha jana ilisafiri kwenda Berkane, kwa ajili ya mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane, huku kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids akitoa amri nzito kambini ili kukwepa vita nje ya uwanja.
Simba itavaana na Berkane kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Manispaa ya Mji wa Berkane, ikiwa ni mechi ya mkondo wa kwanza wa fainali hiyo kabla ya kuja kurudiana nao wiki ijayo kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar uliotangazwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) badala ya Kwa Mkapa.
Hata hivyo, Simba imewatuliza mashabiki wa klabu hiyo, wakiwataka wajikite katika mechi ya kesho kabla ya kupewa taarifa rasmi juu ya pambano la marudiano litakalopigwa wikiendi ijayo, licha ya kwamba tayari barua ya CAF juu ya kuhamisha mchezo ilishasambaa tangu jana mtandaoni.
Ukiachana na ishu ya mechi ya marudiano kupelekwa Zanzibar, kama ilivyo kwa mechi ya kwanza ya nusu fainali dhidi ya Stellenbosch, huku kambini Morocco iliyokuwapo Pullman Mazagan Royal Golf& SPA, moja ya hoteli ya kishua, Kocha wa Simba, Fadlu Davids amekuwa mkali na kutoa amri ya kuzuia wasiohusika na timu kuingia ovyo au kuhudhuria mazoezi ya timu.
Fadlu aliyezoeleka kwa hulka ya upole na mara nyingi kuwa mtu wa watu, juzi alionyesha rangi yake halisi kwa kuwa tofauti katika kambi ya timu hiyo hapa Morocco, kwa kuzuia wasiohusisha na timu hata kushuhudia mazoezi ya awali yaliyofanyika kuanzia saa 11:00 jioni kwa saa za Morocco sawa na saa 1:00 usiku kwa muda wa Tanzania.
Fadlu alizuia mazoezi hayo ya kwanza kuhudhuriwa na kundi kubwa la watu, ikiwamo waandishi na mashabiki wengine waliosafiri na timu kuja Morocco kwa kuhitaji usiri mkubwa kwa kile kilichoelezwa kutotaka kuwapa mwanya wapinzani kuiba mbinu kabla ya kuvaana nao kesho huko Berkane.
Ni idadi ndogo ya viongozi ndio walioruhusiwa kutazama mazoezi hayo huku wakikatazwa kuchukua kwa video programu za mbinu na ufundi ambazo alikuwa akizitoa.
Wachezaji hao wa Simba walianza na mazoezi ya kunyoosha miili na baadaye kufanya mazoezi ya mbinu.
Sababu ya Fadlu kuzuia mazoezi hayo kuhudhuriwa na idadi kubwa ya watu ni kuzuia uwezekano wa mbinu na mipango yake kwa ajili ya mechi dhidi ya RS Berkane kuvuja.
Simba na Berkane zitaumana kesho kuanzia saa 4 usiku ikiwa ni mechi ya tatu kwao kukutana katika michuano ya Kombe la Shirikisho, kwani mwaka 2022 walikutana makundi na kila moja ilishinda mechi ya nyumbani, Wamorocco wakishinda 2-0 kabla Wekundu kulipa kisasi cha 1-0 Kwa Mkapa.
Simba imetinga hatua hiyo kwa kuitoa Stellenbosch ya Afrika Kusini katika mechi ya nusu fainali wakati Berkane iliwatoa CS Constantine ya Algeria, huku ajabu timu zote hizo nne zilizokuwa katika nusu zilitokea makundi mawili ya A na B na Simba na Berkane ndizo zilizopenya fainali hiyo.
Timu hizo zitarudiana wiki ijayo kwenye Uwanja wa New Amaan Zanzibar, kama hakutakuwa na mabadiliko mengine baada ya CAF kutoa taarifa ya kuhamisha mechi hiyo kutoka Benjamin Mkapa.