Prime
Waarabu wataka mwingine Yanga

Muktasari:
- Lakini mambo yakiwa hivyo, sasa inadaiwa, kiungo Duke Abuya ambaye amekiwasha sana, ameingia anga ya JS Kabylie ya Algeria iliyoanza mazungumzo naye na kama mabosi ya Yanga hawatashuka mapema na kufanya kazi basi huenda ikamkosa mchezaji huyo raia wa Kenya.
WAARABU ni kama wamenogewa na mastaa wa Yanga. Wameanza na Stephane Aziz KI. Kiungo mshambuliaji huyo ametajwa kuwindwa na Wydad Casablanca mwishoni mwa msimu. Kisha Clement Mzize naye kutajwa kuwindwa na timu kadhaa za Kiarabu.
Lakini mambo yakiwa hivyo, sasa inadaiwa, kiungo Duke Abuya ambaye amekiwasha sana, ameingia anga ya JS Kabylie ya Algeria iliyoanza mazungumzo naye na kama mabosi ya Yanga hawatashuka mapema na kufanya kazi basi huenda ikamkosa mchezaji huyo raia wa Kenya.
Matajiri wa JS Kabylie inaelezwa wameanza kufanya mazungumzo na kiungo huyo aliye kwenye moto, wakitaka kufanya biashara ya haraka ya kumsajili.
Abuya aliyeichezea Yanga dakika 1,299 msimu huu mkataba alionao na Yanga unamalizika mwisho wa msimu huu mara Ligi Kuu Bara itakapomalizika na baada ya hapo atakuwa huru na kurahisisha kubebwa na klabu yoyote bure kabisa.
Yanga ilimsajili kwa mwaka mmoja, ikinunua msimu mmoja uliosalia katika mkataba aliokuwa nao na Singida Black Stars ambayo awali ilimsajili kwa miaka miwili akitokea Polisi Kenya, huku akiwa amewahi kukipiga timu kadhaa kama Nkana ya Zambia, Kariobangi Sharks na Mathare za Kenya.
Yanga inaumiza kichwa kwa sasa baada ya awali kumwona kama kiungo wa kawaida, lakini moto aliouwasha mara baada ya kuumia kwa Mganda Khalid Aucho umewashtua mabosi wa timu hiyo na sasa wanapiga hesabu mpya za kutaka kumbakisha kikosini kwa muda mrefu zaidi.
“Tunataka kuanza naye mazungumzo haraka, hizo taarifa za JS Kayblie tunazijua awali walitutafuta wakijua kama bado ana mkataba na sisi hawakujua kama unamalizika mwisho wa msimu huu,” alisema bosi huyo wa juu wa Yanga na kuongeza.
“Unajua shida ni namna alivyocheza vizuri hasa hili duru la pili la ligi, mzunguko wa kwanza tulipata shida kumwelewa lakini huku mwishoni amefanya mambo makubwa.”
Katika eneo la kiungo mkabaji mtihani mkubwa unaoiandama Yanga ni viungo wote watatu wanatakiwa kuondoka mwisho wa msimu huu akiwemo Khalid Aucho, Mudathir Yahaya na Abuya ambao wanamaliza mikataba, huku Aziz Adambwile akimalizia mkopo wake wa mwaka mmoja akitokea Singida BS.
Abuya amehusika katika mabao manne akifunga maao mawili na asisti mbili, ana uwezo wa kutumika maeneo tofauti akimudu kucheza kama kiungo mshambuliaji wa kati au hata kushambulia akitokea pembeni, kitu kilichoivuitia JS Kabylie iliyowahi kunolewa na kocha aliyeifundisha Simba kwa muda mfupi, Abdelhak Benchikha.