Maxime azipigia hesabu dakika 180

Muktasari:
- Maxime alisema katika kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa ameamua kutoa likizo fupi ya wiki mbili kwa mastaa wa timu hiyo kabla ya kurejea mapema mwezi ujao kujiandaa na mechi hizo za kufungia msimu akisala pointi zitakazowaweka salama katika kuangukia play-off ya wenyewe kwa wenyewe.
KIPIGO cha mabao 5-0 ilichopata Dodoma Jiji kutoka kwa Azam FC ni kama kimemshtua kocha Mecky Maxime, aliyeliambia Mwanaspoti kwamba kwa sasa anajipanga kiufundi ili kukuhakikisha anazitumia mechi mbili zilizosalia ambao ni sawa na dakika 180 kujiokoa kucheza play off.
Maxime alisema katika kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa ameamua kutoa likizo fupi ya wiki mbili kwa mastaa wa timu hiyo kabla ya kurejea mapema mwezi ujao kujiandaa na mechi hizo za kufungia msimu akisala pointi zitakazowaweka salama katika kuangukia play-off ya wenyewe kwa wenyewe.
Dodoma Jiji imesaliwa na mechi dhidi ya Singida Black Stars utakaopigwa Juni 18 kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma kisha kumalizia kwa kuifuata Yanga jijini Dar es Salaam Juni 22, kwani kwa sasa imecheza mechi 28 na kuvuna pointi 34 ikishika nafasi ya saba katika msimamo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Maxime alisema wamepoteza mechi dhidi ya Azam, lakini wanasahau kwa vile ni sehemu ya mchezo na akili zote wanazielekeza katika michezo miwili ijayo na kwamba wanarudi kufanyia kazi upungufu uliojitokeza Azam Complex, ili mambo yawe mazuri kwao.
“Kutakuwa na mapumziko ya siku chache kutokana na ligi kusimama kwa muda kupisha Kombe la Shirikisho (FA) mara baada ya kurudi tutakuwa na maandalizi ya mechi mbili ngumu kutokana na aina ya timu tunazokutana nazo,” alisema Maxime na kuongeza;
“Singida Black Stars ni timu nzuri ina wachezaji wengi bora lakini pia tutamaliza na bingwa mtetezi ambaye anapambania kombe alilo lishikiria haitakuwa rahisi tunahitaji kusawazisha makosa ili kupunguza idadi ya mabao tunayofungwa lakibni pia sisi pia tushinde.”
Maxime alisema alisema mzunguko huu ni wa lala salama wakikosea wanaadhibiwa kama ilivyotokea katika mechi ya Azam, huku akikiri kwamba wachezaji wa Dodom walikosa umakini dakika 30 za kipinzi cha kwanda udhaifu ambao wapinzani wao waliutumia.
“Tunahitaji umakini na utulivi hasa kwenye mechi mbili zilizobaki kwani bado hatupo kwenye nmafasi nzuri kwasababu walio chini yetu tumeachana kwa pointi chache akishinda anapanda na sisi tunateremka,” alisema Maxime na kuongeza;
“Tutaingia kwa kuziheshimu timu ambazo tutacheza nazo mechi zilizobaki tunahitaji pointi zote sita kwenye makaratasi ni rahisi kuzungumza lakini dakika 180 ndio zitakazoamua.”