Fountain , KenGold ukilenga tu imooo

Muktasari:
- Fountain Gate iliyopo nafasi ya 14 ndiyo inayoongoza kwa kufungwa mabao mengi, ikiruhusu 54 katika mechi 28 ikifuatiwa na vibonde Wachimba Dhahabu wa Mbeya, KenGold iliyofungwa 52 kwa idadi ya mechi kama hizo.
ACHANA na taarifa za kushuka daraja kwa KenGold na Kagera Sugar kuna timu ambazo Ligi Kuu Bara msimu huu, kila lango lao likilengwa huwa imoo, kwa kuruhusu mabao mengi hadi sasa ligi ikisaliwa na mechi za raundi mbili kufungia msimu mbali na kiporo cha Kariakoo Dabi.
Fountain Gate iliyopo nafasi ya 14 ndiyo inayoongoza kwa kufungwa mabao mengi, ikiruhusu 54 katika mechi 28 ikifuatiwa na vibonde Wachimba Dhahabu wa Mbeya, KenGold iliyofungwa 52 kwa idadi ya mechi kama hizo.
Nyingine ambazo ukilenda lango lao tu imooo, ni Dodoma Jiji iiliyofungwa mabao 42, huku ikifuatiwa na KMC iliyoruhusu 41 ikiwa ni ya nne na Kagera ya tano ikifungwa 40.
Timu yenye ukuta mgumu hadi sasa ni Yanga iliyofungwa mabao 10, ikifuatiwa na Simba yenye 11, huku zenyewe zikiwa ndizo zenye safu kali ya ufungaji kwani Yanga imefunga 71 wakati Simba ina 62.
Kaimu Kocha Mkuu wa Fountain Gate, Khalid Adam alisema anatambua changamoto hiyo na anaifanyia kazi kwa kupunguza makosa na sio kusajili wachezaji bora kwa sasa wakiwa na mechi mbili mkononi ili kumaliza msimu.
“Ni kweli safu ya ulinzi ya timu yetu ina changamoto ya kuruhusu mabao kilichopo ni kupunguza makosa ili kujinasua kwenye nafasi mbaya tuliyopo hilo ndio naendelea kulifanyia kazi kwa sasa na naamini kabla ya kurejea kwa ligi mabadiliko yataonekana kwenye mechi mbili zilizobaki,” alisema Adam na kuongeza;
“Sio rahisi lakini matamanio ni kuona tunashinda mechi zilizobaki bila kuruhusu bao na ikitokea basi isiwe kwa idadi kubwa kwa sababu siyo rekodi nzuri kuwa timu inayoongoza kwa kufungwa mabao mengi.”
Kocha wa KenGold, Omary Kapilima alisema kilicho waangusha ni kuto kufanya tathjimini sahihi mwanzo wa msimu baada ya kupanda daraja kwa kusajili wachezaji wazoefu hana sababu ya kujitetea anarudi kujipanga upya.
“Tumeshapoteza hatuwezi kurudi tulipotoka bila ya kufanya mipango sahihi nafikiri tunazingatia mechi zilizobaki kwa kuhakikisha tunamaliza vizuri na kurudi Championship kusawazisha makosa tukipambana kurudi tena.”