Korea Kusini yaanza safari kujenga bandari ya uvuvi Zanzibar

Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Hamad Bakari  na Mwakilishi kutoka Wizara ya Bandari na Uvuvi wa Korea Kusini, Hee Kyung Kim wakisaini makubaliano kuanza upembuzi yakinifu kujenga Bandari ya Uvuvi kisiwani Zanzibar.

Muktasari:

  • Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar na Korea ya Kusini zimetiliana saini ya kufanya upembuzi yakinifu kujenga bandari za uvuvi kisiwani humo.

Unguja. Imeelezwa kuwa ujenzi wa bandari kubwa za uvuvi utaifungua Zanzibar kiuchumi na  kuwavutia wawekezaji kuwekeza kisiwani humo.

Hayo yamebainika leo Jumatatu Julai mosi, 2024 baada ya Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar kusaini makubaliano na Korea ya Kusini ya kufanya upembuzi yakinifu wa kujenga bandari za uvuvi kisiwani humo.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Kapteni Hamad Bakari amesema ujenzi wa bandari za uvuvi Zanzibar hivi sasa zinahitajika kwa vile  ni kisiwa na imezungukwa na bahari.


“Zipo meli nyingi kubwa za uvuvi zingependa kuja Zanzibar lakini changamoto  hatuna bandari maalumu ya uvuvi. Bandari hizi zitaifungua kiuchumi na kuwafanya wawekezaji kuja kwa wingi kisiwani hapa,” amesema. 


Kwa upande wake, mwakilishi kutoka Wizara inayoshughulikia masuala ya Bandari na Uvuvi ya Korea Kusini, Hee Kyung Kim amesema wamekuja Zanzibar kufanya upembuzi yakinifu kwa lengo la kujenga bandari kubwa za uvuvi ambazo zitakuwa za kisasa zaidi.


Amesema watafanya kazi hiyo kwa weledi mkubwa katika maeneo yaliyotengwa ili kuhakikisha lengo la kujengwa kwa bandari hizo linafikiwa kwa manufaa ya Wazanzibari na Taifa kwa ujumla.

Amesema Serikali ya Jamhuri ya Korea ipo tayari kutoa kila aina ya ushirikiano wa kimaendeleo ili kuiona Zanzibar inanufaika kiuchumi kupitia Wizara ya Uchumi wa Buluu na U.

Naye Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Shaaban Ali Othman amesema kujengwa kwa bandari kubwa za uvuvi, utasaidia kuongeza pato la mwananchi mmojammoja.

Amesema, kujengwa kwa bandari hizo kubwa kutazifanya meli za Afrika na kwingineko kuja Zanzibar na wananchi pamoja na vijana kupata nafasi za ajira.

Ameeleza, upembuzi huo utahusisha katika maeneo ya Mangapwani na Mkokotoni kwa upande wa Unguja na Micheweni na Shumba Viamboni kwa upande wa Pemba, ipatikane sehemu moja kwa kila upande ili kujengwa bandari hizo.

Kwa kipindi chote cha miezi sita wakati upembuzi ukiendelea, gharama zote zitagharamiwa na Serikali ya Korea kutokana na urafiki mkubwa uliopo kati mataifa hayo mawili.

Amesema mpaka sasa Zanzibar inaamini kujengwa kwa bandari hizo utakuwa mkombozi wa wavuvi wadogowadogo na wa kati ili kunufaika na wanachokivua katika kukuza kipato chao.

Amefafanua kuwa hivi sasa wavuvi wengi wa Zanzibar wamekua wakivua kisasa zaidi, lakini wanakabiliwa na changamoto ya kuvua uvuvi wa bahari kuu.

"Serikali inazungumza na wadau mbalimbali ili kupata vyombo vya uhakika katika kuhakikisha wavuvi wa Zanzibar wanavua uvuvi wa bahari kuu,” amesema.

Katika kuwalinda wavuvi na wanachokivua Wizara kupitia bajeti yake iliyopitishwa juzi na Baraza la Wawakilishi,  imeanza ujenzi wa viwanda viwili vya kuchakata samaki, majiko na masoko ya kisasa kwa Unguja na Pemba.