Kuhusianisha asili na jamii: Juhudi za JGI katika uhifadhi endelevu Magharibi mwa Tanzania

Tanzania inaelezwa kuwa na idadi ya sokwe wapatao 2200. Picha: Stephano Lihedule

Tanzania ambayo inajulikana kwa juhudi kubwa inazozifanya katika masuala ya uhifadhi, imetenga karibu theluthi moja ya eneo lake la kilomita za mraba 945,087 kwa ajili ya uhifadhi, ikijipambanua kuwa kinara wa kimataifa katika uhifadhi wa mazingira.

Licha ya dhamira hii, safari hii inakabiliwa na changamoto nyingi, kwani jamii nyingi bado ziko nyuma katika kuunga mkono juhudi za uhifadhi.

Mabaki ya mbinu za utawala wa kikoloni bado yanakuza hisia hasi juu ya mipango ya uhifadhi. Sambamba na kuongezeka kwa mahitaji ya ardhi na idadi ya watu, mambo haya yanachochea migogoro kati ya binadamu na wanyamapori, hivyo kusababisha baadhi ya jamii kuwapa changamoto wahifadhi kwa kutanguliza asili kuliko mahitaji ya binadamu.

Zaidi ya miongo mitatu iliyopita, Dk. Jane Goodall, mtafiti na mtetezi maarufu wa Sokwe, alikutana na changamoto mpya ya uhifadhi wa sokwe  kwa vile makazi ya Sokwe huko Gombe yalikuwa kwenye tishio kubwa.

Hili lilimsababisha kuanzisha Mradi wa Uhuishaji wa Misitu na Elimu ya Mazingira katika vijiji vinavyopakana na Ziwa Tanganyika (TACARE), akiweka taswira ya mustakabali endelevu ambapo uhifadhi wa Sokwe ulifungamanishwa na mbinu ya kuwawezesha wanajamii kuwa viongozi na wasimamizi wa mali asili zao.

Inakadiriwa Tanzania ina Sokwe takribani 2,200 wanaoishi katika maeneo yao ya asili, huku asilimia 60 kati yao wakikabiliwa na shinikizo ya kutoweka kutoka kwa watu walio katika wimbi la umaskini. Mgawanyiko wa makazi ya sokwe kutokana na ukataji miti ovyo, upanuzi wa makazi, malisho ya mifugo katika maeneo yasio rasmi, uchomaji mkaa na ubadilishaji wa msitu kuwa mashamba, unaleta tishio kubwa la kutoweka kwa Sokwe na wanyamapori wengine, huku pia kukichangia mabadiliko ya tabianchi.


Mbinu ya JGI: Uhifadhi unaozingatia jamii

Mwanzoni mwa miaka ya 1990, Taasisi ya Jane Goodall (JGI) ilianzisha mbinu ya uhifadhi shirikishi ya jamii. Mtazamo huu unaozingatia jamii, uliwafundisha wakulima wadogo mbinu za kilimo endelevu kama vile kilimo mseto, kilimo cha kontua na utumiaji wa mbolea vunde, ambapo JGI ililenga kuweka usawa kati ya mahitaji ya Sokwe na jamii za wenyeji katika shughuli zake za uhifadhi.

Dk. Shadrack Kamenya, Mkurugenzi wa Sayansi za Uhifadhi wa JGI Tanzania anabainiasha kwamba wakulima hapo awali walifyeka misitu ya mitoni kwa ajili ya kilimo cha muda mfupi na kusababisha upotevu wa rutuba ya udongo ambao ulisababisha ukataji zaidi ya miti kwa ajili ya kilimo.

Hata hivyo, afua kama vile Mradi wa Uhifadhi wa Maliasili wa USAID Magharibi mwa Tanzania, uliofadhiliwa kwa Dola milioni 20 kutoka USAID, umeonesha matokeo ya kutia moyo.

Mafunzo ya mbinu endelevu za kilimo yameongeza kwa kiasi kikubwa mazao ya kilimo. Wakulima waliongeza mavuno hadi asilimia 200 baada ya kuweka mbolea vunde ambayo inahifadhi unyevu hata wakati wa ukame.

Mradi huu ulihusisha vijiji 74 vya mikoa ya Kigoma na Katavi ukigusa maeneo kama makazi ya Mishamo na Katumba mkoani Katavi, ukijikita na masuala ya utawala bora wa maliasili, uzazi wa mpango, elimu ya afya ya uzazi, usawa wa kijinsia na ushirikishwaji wa jamii, mipango ya matumizi bora ya ardhi, elimu ya uhifadhi wa mazingira kwa jamii  na watoto ikiwa na kampeni ya mabadiliko ya tabia za jamii iliyojikita katika matumizi ya mbolea vunde ili kupunguza athari za kilimo cha kuhamahama kuwalinda sokwe na makazi yao.

Mbinu shirikishi ya JGI sio tu imepunguza ukataji miti kwa asilimia 60 lakini pia imenufaisha watu 253,000 kupitia usimamizi endelevu wa maliasili.

Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na uhifadhi wa ardhi yenye ukubwa wa hekta milioni 1.8 za misitu, kusaidia halmashauri za wilaya za Uvinza na Tanganyika kuanzisha hifadhi mbili za misitu ya halmashauri za wilaya na uundaji wa Benki za Hifadhi ya Jamii (COCOBA) ambazo hadi mwishoni mwa mwaka 2023 zilikuwa na wanachama zaidi ya 9,000 ambao walikusanya kiasi cha Sh 1.2 bilioni kama chanzo cha mikopo nafuu kwa ajili ya kuendesha biashara ndogondogo ambazo ni rafiki kwa mazingira.


Wajibu wa TACARE katika uhifadhi na uwezeshaji wa jamii

Mradi wa TACARE, ulioanzishwa na Dk. Jane Goodall mwaka 1994, unaangazia umuhimu wa kuwawezesha wanajamii kuhifadhi maliasili zao. Mpango huu unaangazia kushirikisha jamii katika mbinu endelevu, kuhakikisha kuwa juhudi za uhifadhi zinakuwa jumuishi.

Pamoja na kukuza kilimo mseto na matumizi ya mbolea vunde, TACARE inasisitiza umuhimu wa usawa wa kijinsia na ushirikishwaji wa jamii, uzazi wa mpango na afya ya uzazi. Vipengele hivi ni muhimu kwa ajili ya kukuza usaidizi wa jamii na kuhakikisha kwamba wanajamii wote, bila kujali jinsia, wanaweza kushiriki na kufaidika na mipango ya uhifadhi wa maliasili.

Dk. Kamenya anaeleza kuwa “Wakulima wadogo walifyeka misitu mitoni ili kuzalisha mazao lakini baada ya muda wa miaka mitatu, rutuba ya udongo ilipotea na hivyo kuwalazimisha kufyeka maeneo mengine mapya ya misitu ili kuzalisha mazao.”

Mgawanyiko wa makazi kutokana na ukataji miti ovyo, upanuzi wa makazi, malisho ya mifugo kupita kiasi, uchomaji mkaa na ubadilishaji wa msitu kuwa mashamba, kunaleta tishio kubwa kwa Sokwe na wanyamapori wengine. Picha: Stephano Lihedule

Mpango wa USAID katika uhifadhi wa mazingira Magharibi mwa Tanzania

Novemba 2018, USAID na JGI walizindua   mradi wa USAID Uhifadhi wa Maliasili Magharibi mwa Tanzania kwa ufadhili wa takriban Dola milioni 20 kutoka Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID). Mpango huu ulilenga kuwalinda Sokwe na makazi yao katika mfumo wa ikolojia wa Gombe Masito Ugalla na kusaidia jamii kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kuboresha maisha yao.

Mradi USAID Uhifadhi wa Maliasili Magharibi mwa Tanzania umeziwezesha jamii, Halmashauri na wadau wengine wa uhifadhi kutekeleza hatua endelevu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, huku wakidumisha mbinu ya kutokomeza tishio la kutoweka kwa Sokwe na makazi yao.

Kipaumbele kikuu katika mkakati wa miaka mitano kilikuwa kutoa mafunzo kwa wakulima wadogo kutumia mbolea vunde kupitia kampeni ya mabadiliko ya tabia ya jamii inayoendeshwa kwa kutumia mbinu za kijamii za masoko ikibeba kauli mbiu, 'Tunza Udongo, Tunza Familia, Tunza Mazingira' kuboresha urejeshwaji wa rutuba ili kupunguza athari za kilimo cha kuhamahama kutokomeza  sokwe na makazi yao. 

Tofauti na mbolea ya gharama na inayoharibu udongo, mbolea vunde  ina virutubisho vyote muhimu kwa ukuaji wa mazao, yaani Nitrojeni, Fosforasi na Potasiamu (NPK) na inadumu kwa muda mrefu shambani, ikiwekwa mara moja tu kwenye zao husaidia ukuaji wa mazao na wakulima wanaweza kuizalisha mbolea hiyo kwa kutumia malighafi zinapatikana katika maeneo yao.

Tafiti za JGI zinaonesha kuwa hadi sasa matumizi ya mbolea vunde  katika vijiji vya mradi yana matokeo mazuri, huku mbolea vunde  ikihifadhi maji hata nyakati za ukame katika mashamba yaliyopoteza rutuba, hivyo kuwawezesha wakulima kuvuna kati ya asilimia 100 na 200 zaidi ya walivyokuwa wakivuna kabla ya kuweka mbolea vunde.

Dk. Kamenya anaongeza: “Wahudumu wa vitalu vya miti vijijini   wamekuwa wakiweka malengo ya biashara yao katika miche wanayotesha kwa uangalizi kutoka kwa JGI na wataalam wa halmashauri ya wilaya.”

Mafanikio makubwa yaliyopatikana yameifanya USAID na JGI Tanzania kusaini mkataba wa ushirikiano wa mradi mpywa wa USAID Tumaini Kupitia Vitendo (Hope through SAction) wenye thamani ya Dola milioni 29.5 za marekani,  unaolenga kuimarisha na kukuza juhudi za uhifadhi katika vijiji 104 na kuimarisha mbinu za kilimo zinazohimili mabadiliko ya hali ya hewa na ushiriki wa wanawake kiuchumi.


Ushirikishwaji wa jamii na mbinu endelevu

Mradi huu unahusisha vijiji 74 katika halmashauri za Kigoma, Uvinza, Tanganyika na Nsimbo  katika mikoa ya Kigoma na Katavi na vijiji 30 vya makazi ya Mishamo na Katumba Halmashauri ya Tanganyika na Nsimbo mkoani Katavi na unahusisha maeneo mtambuka pamoja na kilimo hai, ikiwa ni pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, usawa wa kijinsia na ujumuishaji wa jamii, Sayansi ya Data na usimamizi wa maarifa na mawasiliano na simulizi.

Kipengele muhimu cha mradi huo ni matumizi bora ya ardhi, ambapo kila kijiji  kimetenga eneo lake kwa ajili ya kilimo ili kupunguza kilimo cha kuhamahama. Mpango wa kawaida wa matumizi bora ya ardhi ya kijiji unakisiwa kuwa na thamani ya Shillingi 19 milioni unaweka mipaka ya maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya makazi, kilimo, hifadhi  za misitu ya vijiji na kwa matumizi mengine kadri itakavyoamuliwa na jamii husika.

Wahifadhi wa JGI Tanzania wanawashauri wanakijiji si tu kupanda na kutunza miche mipya ya miti, bali pia kuacha visiki vya miti ya miombo iliyokatwa ichipue upya ili msitu huo wa asili uote tena. Wataalamu wa afya ya uzazi wa mpango na usawa wa jinsia kutoka halmashauri za wilaya katika eneo la mradi wanawashauri wanakijiji kuwa na ukubwa wa familia wanazoweza kuzihudumia na kuachana na dhana potofu zinazowazuia wanawake na vijana kuchangia ipasavyo ajenda ya uhifadhi wa maliasili katika vijiji vyao.

Mtaalamu wa Mawasiliano na simulizi wa Taasisi ya Jane Goodall Tanzania,  Robert Mkosamali anabainisha kuwa: “Tafiti zinaonyesha mradi na hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zimepunguza uharibifu wa makazi ya Sokwe, huku ukataji wa misitu katika meneo ya mito ukipungua kwa asilimia 60.” 

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi, Shabani Juma Juma akizungumza na wadau wa uhifadhi. Picha: Michael Pandisha

Matokeo chanya na matarajio ya baadaye

Kwa upande mwingine, takriban watu 253,000 wamefaidika na usimamizi endelevu wa maliasili na uhifadhi wa baianuwai katika mfumo wa ikolojia wa Gombe-Masito-Ugala.

Zaidi ya hekta milioni 1.8 zimehifadhiwa na hifadhi mbili za misitu ya Masito na Tongwe Magharibi zenye ukubwa wa hekta 521,000  mali ya halmashauri ya Wilaya ya Uvinza na Tanganyika zilitangazwa kwenye gazeti la Serikali kupitia uwezeshaji wa Taasisi ya Jane Goodall na ufadhili wa watu wa Marekani kupitia USAID.

Wakazi wa Mishamo na Katumba wameungana katika vikundi 172 vya Benki ya Hifadhi ya Jamii (COCOBA) vyenye wanachama 3,128, (wanaume 1,312 na wanawake 1,681).  Wahudumu wa afya wa jamii 250 wamepatiwa mafunzo katika kutoa huduma za uzazi wa mpango, zaidi ya wanafunzi 21,000 (wanaume 10,000, wanawake 11,000) wanajihusisha na elimu ya mazingira katika vilabu 244 vya Roots & Shoots katika maeneo ya mradi. 

Wahudumu vitalu vya miti ya vijiji na waangalizi wa misitu wa vijiji, wamewezeshwa kupata mafunzo ya vijiji ili kuhakikisha hifadhi za misitu zinaendelea kuhifadhiwa na wanaokiuka sheria ndogo wanashughulikiwa na mkono wa sheria. 

Vijiji vyote 74 katika eneo la mradi vinajivunia kuwa na mipango ya uhifadhi ya misitu na matumizi bora ya ardhi na misitu iliyotengwa na vijiji imerejesha shoroba uhuru kwa sokwe kwenye ukanda wa wanyamapori wa Gombe-Burundi. Kwa msaada wa mradi huo, mamlaka ya hali ya hewa Tanzania imefunga vituo vitatu vya hali ya hewa katika Shule ya Sekondari Kakoso iliyopo Mpanda ndogo, Mkoa wa Katavi, eneo la Lugufu wilayani Uvinza na eneo la Kalinzi wilayani Kigoma, Mkoani Kigoma ili kufuatilia hali ya hewa katika eneo lote la ukanda wa uhifadhi. Taarifa ya hali ya hewa zitatumika  katika kuimarisha mbinu za kilimo kinachozingatia hali mabadiliko ya hewa.


Kushughulikia changamoto na mipango ya baadaye

Mikakati ya utekelezaji  imedumisha udumisha idadi ya Sokwe tu, lakini imepunguza kiwango cha kutoweka kwa jamii ya wanyama hao. Mambo mengi yanachangia kutoweka kwa Sokwe duniani, yakiwemo magonjwa. Wakati mwindaji akiwa na mbwa anapoingia katika makazi ya Sokwe, kwa mfano, nafasi ya Sokwe kushika na kufa kutokana na mafua au magonjwa mengine yoyote ni kubwa.

Pia huzuia ukuaji wa idadi ya Sokwe na kiwango cha chini cha kuzaliwa kwao “Sokwe anapokufa, ni vigumu kupata mbadala wake, kwani ni mtoto mmoja tu huzaliwa katika kipindi cha miaka minne hadi mitano, na ni Sokwe wachache sana huzaa mapacha,” anaeleza Dk Kamenya.

Hata hivyo, mafanikio yaliyopatikana hadi sasa yamewafanya washiriki katika majaribio ya kuzindua USAID Hope through Action - mradi unaolenga kuongeza mafanikio ya uhifadhi wa mazingira wa USAID Magharibi mwa Tanzania na kupanua wigo wa uhifadhi katika vijiji 104 huku USAID ikitoa ufadhili wa msingi wa Dola 29.5 milioni katika mradi huo.

“Tuko katika mchakato wa kumtafuta mshirika wa kilimo ili kupata teknolojia zinazozingatia hali ya hewa kwa wanawake kwa lengo la kukuza uzalishaji katika kanda za kilimo za vijijini, kuwezesha uhusiano wa soko na kuwaunganisha wakulima na benki za biashara kwa ajili ya kupata mikopo midogo,” anaeleza Dk Kamenya.

Mzalishaji wa mbolea vunde wa Kijiji cha Sunuka Wilaya ya Uvinza, Mkoa wa Kigoma, Hilda Joel (kushoto) akimuelezea jambo Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye (kulia). Picha: Michael Pandisha

Vijiji vya Tanzania kuwa na ufanisi wa kukabiliana na uzalishaji wa hewa ukaa

Vijiji 27 Magharibi mwa Tanzania viko kwenye hatua za mwisho za kufaidika na juhudi za uhifadhi wa misitu kwa zaidi ya miongo miwili. Vijiji na halmashauri za wilaya ziko katika hatua za mwisho za kupata mkataba mnono wa kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa kutoka kampuni ya Carbon Tanzania.

Wataalamu kutoka halmashauri za wilaya za Uvinza na Tanganyika katika mikoa ya Kigoma na Katavi pamoja na wawakilishi kutoka Taasisi ya Jane Goodall (JGI) Tanzania na Carbon Tanzania wameandaa mpango wa usimamizi wa misitu ya hifadhi ya Masito na Tongwe Magharibi.

Katika eneo la hekta 521,000, hifadhi hizi za misitu zimefanyiwa tathmini ili kubaini hifadhi za hewa ukaa na kubainisha hatua za kuimarisha uwezo wao wa kupunguza uzalishaji wa gesi chafu.

Hewa ukaa inayochangia asilimia 76 ya uzalishaji wa gesi chafu duniani, husababisha joto katika angahewa na kusababisha mabadiliko ya halijoto, unyevunyevu na mifumo ya mvua.

Misitu ina jukumu muhimu katika kufyonza gesi hizo kupitia kitendo cha mme kukuwa kufuata mwanga (photosynthesis), kuzalisha nishati na kutoa oksijeni. Kuhifadhi misitu ni suluhisho la asili la kufikia malengo ya hali ya hewa, kwani miti inaweza kuondoa asilimia 37 ya gesi zinazoongeza joto katika angahewa.

Halmashauri za wilaya ya Uvinza na Tanganyika zinatarajia kuingia mkataba wa pamoja wa usimamizi wa misitu na halmashauri 27 za Serikali ya vijiji kwa ajili ya usimamizi wa misitu ya hifadhi ya mamlaka za vijiji vya Masito na Tongwe Magharibi, kabla ya mpango wa kukabiliana na hewa ukaa. Mkataba na Carbon Tanzania, biashara inayowekeza katika suluhu za asili kwa kulinda mazingira, mimea, wanyama, watu na hali ya hewa, utafuata.

Carbon Tanzania kwa sasa inatekeleza miradi kama vile; eneo la Yaeda-Eyasi, Makame Savannah na Mlima Ntakata, kulinda misitu kwa ajili ya wazawa, wafugaji, wakulima, wanyamapori na hali ya hewa. Katika hifadhi za misitu za mamlaka za vijiji vya Masito na Tongwe Magharibi, mwekezaji katika fidia ya hewa ukaa atatumia mfumo wa Kupunguza Uzalishaji kutoka katika Ukataji na Uharibifu wa Misitu (REDD) ili kuendeleza usimamizi endelevu wa misitu.

Mfumo wa REDD, ulioanzishwa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC), unaidhinisha miradi ya hiari ya asili inayopunguza au kuondoa uzalishaji wa gesi chafu. “Mfumo huu unaruhusu halmashauri za wilaya na Serikali za vijiji kupata mapato kwa ajili ya shughuli za ulinzi wa misitu zinazopimika na zinazoweza kuthibitishwa zinazosimamiwa na Carbon Tanzania,” anasema Aristides Kashula, Ofisa Misitu Mwandamizi wa JGI.

Ofisi ya Makamu wa Rais, inayohusika na masuala ya mazingira, itaamua uwiano wa mgawanyo wa mapato kati ya halmashauri za wilaya na Serikali za vijiji. Halmashauri zinatarajiwa kuingiza mapato mengi zaidi kuliko ilivyo sasa, lakini hii inakuja na uwajibikijai.

Kila kijiji lazima kiunde kamati imara ya usimamizi wa misitu ya asili itakayosimamia hifadhi za misitu, ikiwa ni pamoja na kufanya doria kuzuia moto, mifugo, walowezi na wawindaji haramu. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, halmashauri za wilaya na vijiji zimetekeleza majukumu sawa wakati wa kutekeleza mradi wa Uhifadhi wa Mazingira wa USAID Magharibi mwa Tanzania na JGI Tanzania na wadau wengine wa uhifadhi.

Tangu mwaka 2018, JGI, chini ya ufadhili wa USAID, imetoa mafunzo kwa halmashauri za wilaya na vijiji kuhusu usimamizi wa maliasili. “Tulifanya doria za pamoja za misitu kila robo mwaka, huku JGI ikilipa gharama za magari, mafuta na posho,” anakiri Bruno Mwaisaka, Afisa Maliasili wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika.

Utafiti wa pamoja uliofanywa na halmashauri na JGI ulibaini vitisho kwa Sokwe na kupitia upya mipango ya matumizi ya ardhi ya kijiji. “Tumeshirikiana na JGI kutoa elimu kwa wanavijiji kuhusu afya ya uzazi, kilimo hai, utawala bora, haki na usawa na utawala wa sheria,” anasema Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Sigunga, Arfonsina Tambo.

Mikutano tofauti ilifanyika kwa ajili ya vijana, wanawake, wanaume na makundi yenye mahitaji maalum kueleza matatizo yao na ripoti ziliwasilishwa kwenye mikusanyiko ya vijiji ili kupata ufumbuzi wa kudumu. Hata hivyo, changamoto za kisiasa ziliibuka wakati wa uchaguzi, kwani viongozi walihofia kutekeleza sheria ndogo za vijiji kunaweza kugharimu kura hizo. Wafugaji kutoka mikoa jirani waliwahonga viongozi ili walishe katika maeneo ya hifadhi na wakimbizi kutoka nchi zilizokumbwa na vita wakafyeka misitu.

Licha ya changamoto hizo, wanajamii wanatambua manufaa ya mradi wa USAID wa Uhifadhi wa Mazingira Magharibi mwa Tanzania. Maarifa ya kilimo-hai yamepunguza utegemezi wa wanawake katika uvuvi kutoka Ziwa Tanganyika. “Mboji ya mbolea imeongeza mavuno ya mahindi kwa kiasi kikubwa, hivyo kupunguza utegemezi wa wanawake ziwani,” anasema Tambo.

Vikundi viwili vya Benki ya Ushirika ya Jamii (COCOBA) vyenye wanachama 55 vimejipatia kipato kwa kukusanya na kuuza uyoga kutoka kwenye hifadhi za misitu. JGI ilitoa ruzuku ya asilimia 80 kwa ajili ya kununua mashine ya kukaushia uyoga inayotumia umeme jua yenye thamani ya Sh680, 000 ili kusaidia kufungasha uyoga kwa ajili ya kuuza.

Kiongozi wa kikundi cha COCOBA katika eneo la Katumba mkoani Katavi Neema Elias anasema. “Vikundi vitaendelea kukusanya uyoga mwitu ili kukidhi mahitaji ya wateja.”

Athumani Makana aliyeanza ufugaji nyuki mwaka 2005 amenufaika na mradi huo wa uhifadhi. Alipopata habari kwamba mbolea na dawa za kuulia wadudu zinachafua asali, sasa anatumia mizinga 2,000 ya nyuki ya kisasa na 300 inayomilikiwa na mke wake katika hifadhi za misitu, akizalisha angalau lita 6,000 za asali safi kila msimu. Upendo Honey hununua asali hii ambayo haijachafuliwa kwa Sh3, 500 kwa kilo na hivyo kuongeza mapato.

“Ufugaji wa nyuki unalipa na kubadilisha maisha,” anasema Makana ambaye sasa ana nyumba, pikipiki, mashine za kusaga na ana mpango wa kununua gari na kujenga nyumba za kupanga. Soko la ufugaji nyuki linahudumia vikundi 43 vya wafugaji nyuki vyenye jumla ya wanachama 597 (wanaume 476, wanawake 121) ambapo 125 ni wanachama vijana wa kiume.

Ofisa Misitu wa Jamii (wa nne kulia) akieleza jambo kuhusu matumizi sahihi ya ardhi kwa Naibu Mkuu wa Miradi ya USAID, Robert A. Rcelues (wa tano kulia) na wanakijiji. Picha: Michael Pandisha

Je, inawezekana kutoa maoni ni watu wangapi wanafaidika na asali?

Hapa inaonekana mtu mmoja anafanya vizuri (vizuri) lakini msisitizo wa uhifadhi wa jamii ni kwamba wanajamii wengi wanafaidika. (Hii imetatuliwa tazama hapo juu).

Juhudi hizi shirikishi za uhifadhi huahidi mustakabali mwema kwa vijiji vinavyohusika, ikionyesha athari chanya ya usimamizi endelevu wa maliasili kwa jamii za wenyeji.



Ushirikiano wa USAID na JGI katika uhifadhi unaozingatia jamii

Ni nini lengo la ushirikiano kati ya USAID na JGI?

Jason: Kulinda wanyamapori na kuwawezesha watu. Mwaka 2018, tulianza mradi wa miaka mitano wa Uhifadhi wa Mazingira wa USAID Magharibi mwa Tanzania wenye thamani ya Dola milioni 20. Umesaidia kulinda idadi ya sokwe na makazi yao na kuziwezesha jamii za wenyeji. Mwaka 2023, Marekani ilizindua mpango wa Dola milioni 30 na JGI/Tanzania, USAID Tumaini Kupitia Vitendo (Hope Through Action).

Robin: Ninataka kueleza kuwa hii ni ahadi ya muda mrefu. USAID ilianza mpango wa usimamizi wa rasilimali za mazingira katika miaka ya 1990, wakati huo huo Jane Goodall aliona kasi ya ukataji miti Gombe.

Namaanisha, hii ilitokea kabla hata Fei Toto hajazaliwa. Muda mrefu. Mwaka 2003, tulishirikiana na kuanzisha mbinu endelevu za kilimon za jamii. Kisha tukapanua wigo. Tuliwafundisha watoto mbinu za ikolojia. Tuliongeza kiwango cha ardhi chini ya uhifadhi kupitia upangaji wa matumizi ya ardhi unaoongozwa na jamii. Tulirejesha makazi ya sokwe.


Kwa nini ushirikiano wa USAID na JGI unasisitiza kufanya kazi na vijiji badala ya kujikita katika maeneo ya Hifadhi ya Gombe pekee yaliyotengwa kwa ajili ya sokwe?

Jason: Sokwe wanaishi katika misitu nje ya Gombe. Tunafanya kazi na jamii zinazoishi karibu na maeneo hayo, ili waweze kulinda wanyamapori huku wakinufaika na asili zilizopo.

Robin: Zaidi ya hayo, jamii karibu na Gombe hupata mapato kutokana na juhudi za uhifadhi. Kama Mkurugenzi wetu wa Misheni ya USAID, Craig Hart anavyosema, utawala wa wazawa ndio kiini cha ushirikiano huu.


Ni mafanikio gani ambayo USAID na JGI wanajivunia zaidi ushirikiano wao uliodumu kwa miongo miwili?

Robin: Jinsi tunavyonufaisha watu na mazingira na kuwaonyesha watu jinsi wanavyonufaika na mfumo mzuri wa ikolojia. Baadhi ya takwimu: Karibu watu 253,000 waliboresha vipato vyao. Misitu ya hifadhi mbili za mamlaka za vijiji sasa zipo, vijiji 74 vilitengeneza na kutekeleza mipango ya matumizi bora ya ardhi. Tuliwafikia vijana kwa kuanzisha vilabu 244 vya shule za mazingira.

Jason: Na data zilizokusanywa na JGI zinaonyesha uwekezaji wa USAID ulisaidia kupunguza kiwango cha ukataji miti kwa asilimia 55 hadi 60.


Je, mamlaka za vijiji zina jukumu gani katika ushirikiano huu na zinafanya vizuri kwa kiasi gani?

Jason: Mamlaka za vijiji ni muhimu. Nje ya Hifadhi ya Taifa ya Gombe inayosimamiwa kitaifa, wilaya na vijiji vinasimamia ardhi. Vijiji vinatengeneza mipango ya matumizi ya ardhi kwa kushirikiana na mamlaka za wilaya na kitaifa ili kuhakikisha uratibu unafuatwa.

Robin: USAID pia ilifadhili moja kwa moja JGI tawi la Tanzania ikionyesha kujitolea kwa maendeleo yanayoongozwa na wazawa.


Je, mradi wa Hope through Action utaanzisha mipango gani mipya ambayo haikuwa sehemu ya mpango wa Hifadhi ya Mazingira Magharibi mwa Tanzania?

Jason: Mradi unajumuisha mambo kuhusu jinsia, kilimo na mabadiliko ya tabianchi. Mradi pia unaunga mkono juhudi za kukusanya na kutumia vyema data.

Je, ‘mtazamo kijinsia’ umesaidia vipi kushinda dhana potofu na vizuizi katika uhifadhi unaozingatia jamii?

Robin: Wanawake wanakabiliwa na vikwazo ili kushiriki katika kufanya maamuzi. Kwa kuunga mkono ufanyaji maamuzi jumuishi, wanawake wana nafasi kubwa zaidi na matumaini sawa katika kufanya maamuzi. Upatikanaji wa usawa ni muhimu kwa maendeleo endelevu ya Tanzania.

Jason: Kwa kuwajumuisha wanawake na vijana katika michakato ya kufanya maamuzi, viongozi hushughulikia matatizo ya vikundi kutokana na mawazo ambayo huboresha hali ya kiuchumi ya jamii nzima. Wakati wanawake hawawezi kushiriki, tunaacha nyuma utaalamu wa asilimia 50 ya watu.

Je, kuna mipango ya kutumia mbinu ya JGI inayozingatia jamii katika mifumo mingine ya ikolojia inayokabiliwa na changamoto kama hizi?

Jason: JGI ilianzisha mbinu ya uhifadhi inayozingatia jamii nchini Tanzania na programu yake ya Upandaji Misitu na Elimu kwenye maeneo ya Ziwa Tanganyika. Programu za uhifadhi za USAID Tanzania ni pamoja na kufanya maamuzi ya kijamii kama dhana ya msingi.

Robin: Kwa mfano, mradi wa USAID Heshimu Bahari unaimarisha usimamizi unaoongozwa na jamii wa makazi muhimu ya samaki na Mradi wa Utawala Bora wa Jamii wa USAID unajenga uwezo wa jamii kuwajibika kwa mahitaji ya jamii na mazingira. Wamarekani na Watanzania wanashiriki kwenye programu katika jamii zao. USAID inakuza mchango wa ndani nchini Tanzania.


Jason Ko anafanya kazi kama Mshauri Mkuu wa Mazingira wa USAID/Tanzania.

Robin Holzhauer ni Naibu Mshauri wa Maendeleo na Mawasiliano wa USAID/Tanzania.