Benki ya CRDB yakabidhi gawio la Sh51.7 bilioni kwa Serikali

Waziri wa Uwekezaji na Mipango, Profesa Kitila Mkumbo (katikati), Kaimu Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha (Usimamizi na Uchumi), Japhet Justine (wa pili kulia), Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge, Oran Manase Njeza (kulia), Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Dk Ally Laay (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (wa pili kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati ya Bajeti ya Bunge (waliosimama) katika hafla ya kukabidhi gawio kwa Serikali kwa mwaka 2023 katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Kambarage Hazina jijini Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita.

Dodoma. Waziri wa Uwekezaji na Mipango Profesa Kitila Mkumbo amepokea gawio kubwa zaidi kupata kutolewa na taasisi ya kifedha la Sh 51.7 bilioni linalotokana na uwekezaji wa Serikali ndani ya Benki ya CRDB kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dk. Ally Laay.

Akizungumza katika hafla hiyo ambayo alimwakilisha Waziri wa Fedha, Profesa Kitila Mkumbo aliipongeza Benki ya CRDB kwa kutoa gawio hilo ambalo ni sawa na ongezeko la asilimia 12.8 ya gawio lililotolewa kwa mwaka 2022 la Sh45.8 bilioni. Gawio hilo limetokana matokeo mazuri ya fedha mwaka ambayo Benki imeyapata kwa mwaka 2023.

“Ongezeko hili la gawio ni kiashiria tosha kwa Serikali kuwa Benki yetu ya CRDB inazidi kuimarika zaidi kutokana na mikakati madhubuti ya kibiashara iliyojiwekea na jambo linalowapa moyo Watanzania na wawekezaji kuwa benki inatoa huduma bora katika jamii,” alisema Profesa Mkumbo.

Waziri Mkumbo alisema Sh 27.4 bilioni kupitia Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja na Serikali ya Denmark (DIF) zitakwenda kusaidia kuboresha zaidi sekta ya afya.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi gawio kwa Serikali kuu na taasisi zake kutoka Benki ya CRDB kwa mwaka 2023 katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Kambarage Hazina jijini Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita.

“Makubalino yetu ni kuwa fedha hizi zinaelekezwa katika kuimarisha sekta ya afya, kwa maana ya kuimarisha miundombinu na kusaidia upatikanaji wa dawa na vifaatiba,” aliongezea Profesa Mkumbo.

Waziri Mkumbo amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dk Samia Suluhu Hassan, katika kipindi chake kifupi, tayari imeongeza vituo vya afya kutoka 8,549 mwaka 2021 hadi vituo 9,693 mwaka 2024.

“Fedha hizi zitakwenda kusaidia jitihada hizi ikiwa ni mpango wa Serikali wa kuhakisha wananchi wanapata huduma bora za afya.”

Akielezea namna ambavyo Serikali inaridhishwa na umahiri wa Benki ya CRDB katika kutanua wigo wa huduma zake ndani na nje ya nchi, Profesa Mkumbo ameipongeza Benki hiyo kwa kupanua wigo wake kwa kuanzisha kampuni tanzu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kampuni tanzu ya CRDB Insurance Co. Ltd, pamoja na taasisi ya CRDB Bank Foundation ambayo imeonyesha kuwa mstari wa mbele katika kuchochea ujumuishi wa kiuchumi kupitia programu ya IMBEJU.

Aidha, Profesa Mkumbo aliihakikishia Benki ya CRDB na wadau wengine wa maendeleo nchini kuwa Serikali itaendelea kuimarisha na kuweka mazingira rafiki na endelevu ya kufanya biashara katika sekta ya fedha na sekta nyinginezo ili kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje.

Naye Kaimu Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha (Usimamizi na Uchumi), Japhet S. Justine aliipongeza Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Benki ya CRDB kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kusimamia benki hiyo na kupelekea matokeo mazuri ya kifedha na kukua kwa gawio kwa wanahisa ikiwamo Serikali.

Japhet aliipongeza pia Benki Kuu kwa usimamizi mzuri wa sekta hiyo ambayo imechangia katika utendaji mzuri wa taasisi za kifedha, na uwepo wa huduma bora na nafuu kwa wananchi.

Akikabidhi gawio Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Dk Ally Laay alisema kuwa gawio hilo ni sehemu ya faida ya Sh423 bilioni baada ya kodi ambayo Benki hiyo imeipata katika mwaka wa fedha 2022.

 “Katika Mkutano wa Wanahisa uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC) mwezi Mei mwaka huu, Wanahisa wa Benki ya CRDB walipitisha kwa pamoja gawio la shilingi 50 kwa hisa ikiwa ni ongezeko la asilimia 11 na hivyo kufanya jumla ya gawio la mwaka huu kufikia Sh 130.6 bilioni sawa na asilimia 31.8 ya faida halisi iliyopatikana,” alisema Dk Laay.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema kukua kwa thamani ya uwekezaji wa wanahisa wa benki hiyo kutokana na mafanikio ambayo benki hiyo imeyapata katika utekelezaji wa mkakati wake wa biashara wa muda wa kati wa mwaka 2023 – 2027. Nsekela ameeleza mbali na gawio lililotolewa katika mwaka wa fedha 2023, Benki ya CRDB pia imelipa jumla ya kodi za Sh 403.2 bilioni.

Waziri wa Uwekezaji na Mipango, Profesa Kitila Mkumbo (wa pili kulia) akikabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya Sh27.4 bilioni kwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha (Uchumi), Japhet Justine (katikati) ikiwa ni gawio kwa Serikali kwa mwaka 2023 katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Kambarage Hazina jijini Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita. Wengine pichani ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge, Oran Manase Njeza (kulia), Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Dk Ally Laay (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (wa pili kushoto).

Pamoja na kukabidhi gawio kwa Serikali kuu kupitia mfuko wa uwekezaji wa DANIDA, Benki ya CRDB pia imekabidhi gawio kwa taasisi na mashirika mbalimbali ya Serikali ikiwamo PSSSF, NSSF, ZSSF, NHIF, Local Government Loans Board, Chama cha Ushirika cha Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (WETCU), Umoja Unit Trust Scheme, pamoja na halmashauri za Mbinga, Shinyanga, Mufindi, Chunya na Rungwe.


Kuhusu Benki ya CRDB

Benki ya CRDB ni moja benki zinazoongoza katika ukanda wa Afrika Mashariki, inatoa huduma kwa wateja wadogo, wakati na wakubwa ikiwamo huduma kwa wateja binafsi, huduma za hazina, huduma za bima, mikopo ya biashara, kilimo na uwezeshaji kwa wajasiriamali wadogo.

Benki ya CRDB ndio benki ya kwanza nchini Tanzania kutambuliwa na kampuni ya kimataifa ya utafiti ya Moody’s Investors Service kuwa moja kati ya benki 10 imara na salama Afrika katika uwekezaji.

Moody’s imeipa Benki ya CRDB daraja la uimara la B1 ambapo ni daraja la juu zaidi kupatikana kwa mabenki na taasisi za fedha katika ukanda wa jangwa la Sahara.

Benki ya CRDB imepata utambuzi wa Mfuko wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa (UN Green Climate Fund) tangu mwaka 2019 na pia imetambuliwa kama benki bora Tanzania na jarida la Global Finance kwa mwaka 2023.

Benki ya CRDB imekuwa kiungo muhimu cha biashara katika nchi za Tanzania, Burundi na DRC kwa kuwahudumia wateja zaidi ya milioni 4 na kupitia mtandao mpana wa matawi 268, wakala zaidi ya 34,000, ATMs zaidi ya 550, mashine za manunuzi zaidi ya 2,800 na Kituo cha Huduma kwa Wateja kinachotoa huduma saa 24/7.