Sane ajutia tattoo yake Man City

Muktasari:

  • Leroy Sare ambaye kwa sasa anakipiga kwenye klabu ya Bayern Munic alijiunga miamba hiyo akitokea Manchester City.

Munich, Ujerumani. Leroy Sare amekiri kujutia juu ya uamuzi wake wa kujichoro tattoo kubwa mgongoni inayoonyesha moja ya mabao yake aliyofunga wakati anakipiga kwenye kikosi cha Manchester City.

Winga huyo mwenye umri wa miaka 28 yupo kwenye kikosi cha Ujerumani kinachopambana kujaribu kushinda ubingwa wa Euro 2024 katika fainali zinazofanyika kwenye ardhi ya taifa hilo.

Ametokea benchini kwenye mechi zote tatu ilizocheza Ujerumani kwenye hatua ya makundi, ikiwamo ile ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Uswisi, ambapo ulikuwa mchezo wa mwisho wa hatua hiyo ya makundi.

Sane sasa anataka kuongeza mabao yake 13 aliyofunga akiwa na timu ya taifa ya Ujerumani wakati itakapokipiga na Denmark kwenye mtoano wa hatua ya 16 bora leo Jumamosi.

Sane anacheza kwenye klabu ya Bayern Munich, ambako amefunga mabao 29 katika mechi 123 alizocheza kwenye Bundesliga tangu alipojiunga na timu hiyo mwaka 2020. Lakini, kabla ya hapo alikuwa kwenye kikosi cha Man City, ambako alishinda mataji mawili ya Ligi Kuu England, moja la Kombe la FA na matatu ya Kombe la Ligi.

Moja ya nyakati zake bora huko Etihad, wakati alipofunga kwenye ushindi wa mabao 5-3 dhidi ya Monaco kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, licha ya kwamba Man City ilitupwa nje kwenye jumla ya mabao. Na baada ya hapo, mkali huyo wa zamani wa Schalke alikwenda kuchora tattoo ya bao lake alilofunga kwenye mechi hiyo, kitu ambacho kwa sasa anajutia.

Akizungumza na Der Spiegel, Sane alisema: “Kama nilivyosema, nilikuwa kijana mdogo. Ingekuwa leo ningefanya uamuzi tofauti.”

Sane aliingia kwenye gumzo kubwa baada ya kuonyesha tattoo hiyo mwaka 2017 na kushangaa kwa namna jambo hilo lilivyokuwa kwenye vyombo vya habari, alisema: “Nilishtushwa sana jinsi jambo lilivyofanywa kuwa kubwa. Nilikuwa bado mdogo.”

Tangu alipoondoka Man City, Sane ameshinda Bundesliga mara tatu, Klabu Bingwa Dunia, Uefa Super Cup na Kombe la Ujerumani mara tatu.