TUONGEE KIUME: Mwenzetu aliletewa watoto wake baa na mkewe

Kama una kawaida ya kwenda baa utakuwa unaelewa kuwa hiyo ndiyo sehemu hutokea mambo ya kushangaza zaidi ya sehemu yoyote ile. Nina uhakika ukiwa huko umewahi kushuhudia mzee mtu mzima akiwa amelewa chakari, amevua shati liko mabegani, anacheza wimbo wa ‘Komasava’ kama hana akili nzuri.

Lakini nakuhakikishia, katika mambo yote ya kushangaza niliyowahi kuyaona baa hakuna kitakachozidi siku nilipoona mwanamume ameletewa watoto wake baa na mke wake; nitakusimulia.

Mwanamume kuletewa mtoto sehemu isiyostahili siyo jambo jipya kwangu. Nimewahi kuona mwanamume amepelekewa mtoto wake ofisini. Yaani jamaa alikuwa na mtoto na mwanamke ambaye hawaishi pamoja. Kwa hiyo kumbe alikuwa na kawaida ya kupiga chenga kuhudumia.

Siku hiyo yuko ofisini hana hili wala lile, mara anakuja kuambiwa kuna mgeni wako. Anashangaa mgeni wangu? Nani? Anakwenda mapokezi anamkuta mwanamke, mtoto wake wa miaka mitano na begi lenye nguo za mtoto. Mwanamke akamwambia “kama umeshindwa kumuhudumia mtoto wako, nimekuletea umtafutie kazi ili ajihudumie.”

Lakini ya kuletewa mtoto baa sikuwahi kuifikiria. Jamaa tuko naye hapa kila siku, tunakunywa naye, tunatazama mpira pamoja na wakati mwingine hasa mwisho wa wiki tunamuacha hapa hapa.

Lakini kumbe jamaa nyumbani kwake ni kama sehemu ya kubadilishia nguo tu, yaani anarudi usiku mnene kutoka baa na anatoka majogoo kwenda kazini. Anarudi anakuta watoto wamelala, anaondoka anaacha watoto hawajaamka.

Kwa hiyo siku hiyo ilikuwa mwisho wa wiki, tulianza naye vizuri, tukanywa lakini mida mida tukaamua tubadilishe kijiwe, tukahamia baa nyingine. Basi mishale ya saa 6 usiku hivi, hatuna hili wala lile tunashangaa mwanamke anakuja kwenye meza yetu akiwa na watoto wawili, mmoja mdogo wa miaka mitatu kambeba mwingine wa miaka sita anatembea mwenyewe.

Aisee, sijawahi kuona mwanamke kauzu kama huyo. Alipofika katusalimia tu, za saa hizi shemeji, kisha akamshusha mtoto aliyembeba huku anamwambia nenda kwa baba. Sasa jamaa yetu kabaki kaduwaa tu, haelewi nini kinaendelea, wala hajui afanye nini, ikabidi ampokee mtoto.

Basi ‘waifu’ wake akamwambia neno moja tu, ukirudi nyumbani utakuja nao. Jamaa ikabidi aulize ‘kulikoni mama Junior? Kuna tatizo gani?’

Na jamaa wakati anauliza hivi alikuwa anaonekana kabisa haelewi kinachoendelea. Maana kama kuhudumia anahudumia, watoto wanakula vizuri, wanaishi vizuri, wanakwenda hospitali nzuri, wanasoma pazuri, sasa kulikoni?

Mkewe akamjibu, akamwambia “wewe kila siku unaporudi nyumbani unakuta watoto wamelala unaondoka hawajaamka, na sio kwamba upo bize na kazi, hapana, ni uko baa unapombeka. Muda kama huu ulitakiwa uwe nyumbani na familia yako. Mwisho watoto wakusahau, uje wakuite mjomba, kwa hiyo ili tusifike huko, nimekuletea watoto ukae nao hapa ili wasimsahau baba yao.”

Alivyomaliza hotuba yake, akageuka, akaondoka zake. Basi mwenzetu ikabidi ainuke na watoto wake amfuate mke wake, na usiku huo hakurudi tena baa.

Ninachoweza kukwambia ni kwamba ile ilikuwa njia ya ajabu sana, lakini ilifanya kazi na inafaa kuwanyoosha baba wote wanaodhani jukumu lao ni kutoa pesa tu, si kukaa karibu na familia zao.

Dunia imebadilika sana siku hizi, ni rahisi sana watoto kukengeuka kuwa na tabia zisizopendeza. Pengine hatuna uwezo kwa asilimia 100 wa kuzuia hilo kutokea, lakini kama tutajitahidi kuwa karibu zaidi na familia zetu, na watoto wetu pengine tunaweza kusaidia watoto wetu wasiishie huko.