Muelemishe Mwafrika Atakayeimudu Karne ya 21

Ni jambo lililopo katika kumbukumbu kuwa kichocheo cha ghasia za kihistoria za Soweto dhidi ya serikali ya kibaguzi ya Afrika Kusini, zilizoleta msukumo kwa harakati za uhuru nchini humo, ilikuwa ni kiu ya watoto wa Afrika Kusini kupata elimu bora na inayofaa.

Walitambua kwamba wakipewa elimu ya daraja la pili kungepelekea wao kuwa raia wa daraja la pili katika nchi yao na duniani kiujumla. Hivyo, ikachochea uamuzi wa Umoja wa Afrika kuichagua tarehe 16 Juni kuwa Siku ya Mtoto wa Afrika. 

Mada ya mwaka huu isemayo, “Jinsi gani tunajenga mifumo imara ya elimu kwa madhumuni ya dhati katika kujifunza, huku tukitngeneza mapenzi ya kujisomea?” imefaa zaidi kwa sababu inaangazia ni elimu ipi tunatakiwa kuwapa Watoto wa Afrika kuendana na mahitaji ya karne ya 21.

Kwanza kabisa, tunahitaji kuanza na wanafunzi wenyewe, kama Ken Robinson alivyosema hapo zamani, ‘Watoto wote wanaanza maisha yao ya shule wakiwa na mawazo yanayong'aa, akili changa na utayari wa kuhimili hatari kwa kile wanachofikiria’.

Hivyo, kutegemeana na mazingira ya nyumbani, vituo vya chekechea na vituo vya kulelea watoto wadogo (Day Care), shule za awali na shule za msingi wanazopitia: Hawawi wabunifu, wengi wanakuwa nje ya ubunifu huo.

Ni katika maeneo haya ambapo ubunifu wa watoto, uwezo wao wa kutafuta, kuchunguza, kujifunza na kujieleza wenyewe hujengwa au kuharibiwa. Ndiyo hapo ambapo pia upendo wa kusoma na kujifunza katika maisha yao yote huchochewa au kuharibiwa.

Je watoto wetu wanaona shule zao za awali kama ni sehemu za furaha za kucheza, kuleta muingiliano na urafiki, za hadithi na sanaa, au kama vikao visivyo na maana ambapo wanakaa kimya na kuadhibiwa wasipo tii?

Tunapaswa kuondoa dhana kwamba ni vizuri watoto wanavyoanza masomo mapema. Nchi zinazofanya vizuri katika elimu, kama Ufini (Finland) au Japan, zinazingatia kucheza, kufurahia hadithi, kujifunza kuishi pamoja na kadhalika. Na wana vitabu vya kusisimua, vyenye rangi, na vinavyovutia watoto hao kusoma.

Hivyo ndivyo mtu anavyojenga tabia ya kusoma na akili ya ubunifu. Lakini inaonekana tumebadilisha shule zetu za awali na chekechea kuwa vyuo vikuu vidogo na kisha tunalalamika wanafunzi wanapochoka shuleni au hawapendi kusoma vitabu. Je, ni wazazi wangapi wanafurahia kununua vitabu vya hadithi, si vitabu vya kiada, kuchochea mawazo ambayo yalionekana hata na wanasayansi wakubwa kama Einstein, kuwa ni ufunguo wa maendeleo kwa watoto wetu?

Watoto wetu wanapoendelea kukua, natambua kwamba Wizara ya Elimu imechukua hatua muhimu katika kuandaa mtaala mpya. Kwa mara ya kwanza, tumeweka kipaumbele kwamba watoto ni tofauti na wana vipaji tofauti mbali na masomo. Kwa matumaini, kama inahitaji rasilimali kubwa, kila shule itaweza kushughulikia utofauti wa vipaji walivyonavyo watoto wetu.

Pia natambua kwamba sera mpya inatoa kipaumbele kwa ujuzi wa karne ya 21, hasa ubunifu na fikra pevu, kazi ya pamoja, inayoendana na mazingira ya wakati huu, sio tu kwa maendeleo ya watoto wetu bali pia 'kuajirika’ ambayo nadhani ni mojawapo ya malengo ya mtaala mpya ambalo pia ni lengo kuu la wazazi wengi.

Tofauti na imani ya sasa kwamba kufaulu mitihani na kupata vyeti vinavyohitaji uwezo wa kukariri (ambayo ni ustadi ambao umekuwa sio wa lazima katika zama hizi za Google na akili mnemba), kinachotafutwa sasa na waajiri ni ujuzi wa karne ya 21.

Ili kuunda mifumo ya elimu inayofaa, tunahitaji kubadili mfumo mzima wa tathmini, si kile unachojua bali jinsi unavyoweza kutumia ubunifu, fikra pamoja na kushirikisha wengine katika kile unachojifunza na kuendelea kujifunza.

Hii inapaswa pia kujumuisha maarifa ya kompyuta, haitoshi tu kujua jinsi ya kutumia kompyuta, kuweka programu, kutumia akili mnemba, nk. Tunahitaji kujua jinsi wengine wanaotumia mtandao wanavyotutumia sisi pia.

Tunahitaji kuwa na uwezo wa kutambua utofauti kati ya ukweli na uongo, nusu-kweli, kukuza, nadharia, nk. Hii itatuwezesha kufanya maamuzi yenye taarifa sahihi katika maisha yetu.

Teknolojia ni muhimu kwa maisha ya watoto wetu, hivyo badala ya kupiga marufuku simu janja shuleni, tunapaswa kuwafundisha watoto wetu jinsi ya kuzitumia kwa ufanisi na kwa manufaa yao.

Mwisho, katika muktadha wa Tanzania, elimu inayodumu, yenye ubora na inayoleta maana, hutegemea uwezo wa watoto wetu kuelewa kile wanachofundishwa. Haina maana kuwawekea wanafunzi wote lugha ya kufundishia ambayo hawana ufasaha nayo.

Ikiwa tunataka kweli kuunda ubunifu na fikra tunduizi kwa watoto wetu, tunapaswa kutumia lugha wanayoielewa ili kuwafundishia, huku wakijenga umahiri wao katika lugha nyingine. Vinginevyo, tutaishia kuwalaumu watoto wetu wengi kwa kuchanganywa na masomo badala ya kujifunza.