Tanzania ina fursa ya kuongeza mapato kupitia utalii wa ndani

Mlima Kilimanjaro pamoja na Mbuga za Wanyama ni Moja ya vivutio vinavyovutia watalii wengi kuja nchini.

Muktasari:

Hali hii inatokana na utamaduni wa jamii nyingi za Kiafrika kutojenga utamaduni wa kutenga muda kwa ajili ya kutembelea vivutio vya kitalii.

Imekuwapo dhana kuwa unapozungumzia mtalii unamaanisha ni mtu kutoka nje ya nchi, hasa Ulaya, anayekuja nchini kuona maliasili ya taifa kama vile kutembelea mbuga za wanyama, mambo ya kale na kupanda mlima.

Hali hii inatokana na utamaduni wa jamii nyingi za Kiafrika kutojenga utamaduni wa kutenga muda kwa ajili ya kutembelea vivutio vya kitalii.

Wanauchumi mbalimbali wanaamini kuwa sekta ya utalii nchini inaweza kukua na kuongeza pato lake maradufu iwapo jamii itaelimishwa juu ya utalii wa ndani.

Sekta ya utalii nchini inachangia asilimia 17.5 ya pato la Taifa na inaaminika kwamba ingeweza kufikia asilimia 30 ya pato hilo kama kungekuwa na mkakati wa pamoja wa kutangaza fursa zilizopo na kuhimiza utalii wa ndani.

Utalii wa ndani uboreshwe

Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CBA Tanzania, Julius Mcharo anasema Tanzania ni nchi ambayo imejaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii na hata watalii mbalimbali duniani wamekuwa wakivutiwa na jinsi vivutio hivi ambavyo vinapatikana katika mikoa mbalimbali ya nchi.

Mcharo anasema yeye binafsi amepanda Mlima Kilimanjaro na kuona jinsi watalii wanavyofaidi vivutio hivyo ambavyo ni mali ya Tanzania lakini wenyeji hawafaidiki.

Ili kukuza utalii wa ndani na kuwafanya wenyeji wafaidike, anasema ni lazima kuwe na mikakati mizuri inayolenga pia kuongeza pato la taifa.

“Baadhi ya nchi barani Afrika, hivi sasa, zimeanza kuweka mikakati ya kukuza na kuweka vipaumbele katika utalii wa ndani badala ya kukazia tu utalii wa nje,” anasema Mcharo.

Anahimiza Watanzania kubadilika na kushiriki kwenye utalii badala ya kubakia nyuma wakati wageni wanafaidika.

Vilevile, anasema Watanzania wakibadilika ni mapinduzi ya sekta ya utalii kwa sababu itaachana na kutegemea wageni wa nje ambao wakati mwingine hupungua na kusababisha mtikisiko wa mapato kisekta.

Kwa sababu hiyo anaihamasisha Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha inaweka msisitizo katika kutangaza na kuhamasisha utalii wa ndani ili kupunguza utegemezi kwa watalii wa kigeni.

Kwa kutambua mchango mkubwa wa sekta ya utalii katika pato la taifa, Mcharo anasema CBA Tanzania tayari imeanza kukopesha wafanyabiashara wanaofanya biashara za utalii.

“CBA Tanzania itaendelea kubuni huduma mbalimbali za kukuza sekta ya utalii nchini kwa upande wa utalii wa na ule wa ndani,” anasema.

Anawataka Watanzania kuchangamkia fursa kwa kuibua miradi mbalimbali ya utalii na benki ya CBA Tanzania itafungua milango yake kwa kuwahudumia Watanzania wenye lengo la kukuza sekta hiyo.

Anasema lengo la CBA Tanzania ni kuona upungufu katika mambo ya kitalii nchini unaondoka na mambo yanaimarika ili kuvuta wageni wengi.

Anatoa mfano alipopanda Mlima Kilimanjaro alibaini kuwa bado kuna huduma hafifu hasa vituo vya kufikia watalii kama vile hoteli na isitoshe hakuna mipango mizuri ya huduma ya kwanza kwenye vituo na gharama za kupanda mlima bado ni kubwa kiasi kwamba Mtanzania wa kawaida hatazimudu.

“Kuna jambo pia la hatari hasa panapokosekana chupa za hewa ya oksijeni hasa mtalii anapokaribia kilele cha mlima ambako mzunguko wa hewa siyo mkubwa na hivyo huathiri watalii katika kupumua,” anabainisha Mcharo.

Kudorora utalii wa ndani

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania, Devota Mdachi anasema kuwa kuna changamoto nyingi zinachangia utalii wa ndani kudorora.

Anataja miongoni mwa changamoto hizo kuwa ni bajeti ndogo ya utangazaji inayotolewa kwa Bodi ya Utalii Tanzania. “Sekta hiyo ingefanya vizuri iwapo Serikali ingekuwa inatenga fedha nyingi kwa ajili ya matangazo kama ilivyo kwa nchi zingine zinazotuzunguka,” anasema Mdachi.

Anatoa mfano: “Kwa mwaka huu wa fedha, Tanzania imetenga Dola 2.7 milioni za Marekani sawa na Sh6.2 bilioni kwa ajili ya kutangaza utalii, Kenya wametenga Dola za Marekani 36 milioni sawa na Sh82.9 bilioni za Tanzania, Uganda Dola 3.9 milioni sawa na Sh9 bilioni za Tanzania.”

Anasema Tanzania yenye vivutio vingi duniani ndiyo nchi inayotenga bajeti ndogo kwa ajili ya kutangaza fursa ilizonazo, matokeo yake bodi haitekelezi mikakati yake ili kufikia lengo ili kukuza utalii wa ndani.

Pamoja na sekta hiyo kuchangia pato kubwa la Taifa, anasema haipo kwenye Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) na siyo kipaumbele cha taifa.

Anasema changamoto nyingine ni pamoja na utamaduni uliojengeka kwa muda mrefu kwa Watanzania kutotembelea vivutio vilivyopo, wakiamini kuwa utalii unawahusu wageni kutoka nje na gharama kubwa za malazi katika hoteli, hasa zilizoko kwenye hifadhi.

Kampeni utalii wa ndani

Mkurugenzi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Allan Kijazi anasema shirika hilo limezindua kampeni ya miezi sita ya kuhamasisha utalii wa ndani kwa kuwa unachangia ongezeko la pato la taifa. “Kwa upande wa wageni wa nje wanakuja wengi na utalii endelevu ni ule ambao wazawa wanashiriki kikamilifu,” anasema akibainisha kuwa si vizuri kutegemea tu watalii wa nje.

Mcharo anasema Watanzania wanapaswa kufahamu pia kupanda mlima kilimanjaro ni sehemu ya ukakamavu wa mwili licha ya kunufaika na mambo utakayoshuhudia.

“Upandaji mlima ni mazoezi ya kujenga afya ya mwili na ni kivutio kinachoburudisha na kufanya akili na mwili vitulie baada ya uchovu wa kazi za muda mrefu,” anabainisha Mcharo.

Anasema yeye binafsi amekuwa akihamasisha utalii wa ndani ambapo yeye na wenzake waliunda kundi Victoria Group na kutenga muda wao ili kupanda mlima huo mrefu kuliko yote Afrika. Anasema upandaji wa Mlima Kilimanjaro ulikuwa na changamoto nyingi zikiwamo za hali mbaya ya hewa. Hata hivyo, anahimiza Watanzania kutembelea vivutio hivi ili waweze kufurahia nchi yao ambayo ina raslimali nyingi za kustajabisha na zinazowavutia wageni.

Nini kifanyike ili kukuza utalii wa ndani? Jibu ni kwamba Serikali haina budi kutenga bajeti za kukuza utalii, nguvu ielekezwe katika kukuza utalii wa ndani, somo la utalii liongezwe katika mitalaa ya shule za msingi na tozo za kuingia kwenye hifadhi zipungue.