Mambo sita ya kufanya kuimarisha afya ya ubongo

Dar es Salaam. Ikiwa wewe ni miongoni mwa watu wasiolala inavyopaswa, basi fahamu unauumiza ubongo wako na kuufanya ushindwe kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Wataalamu wa akili na ubongo, wanasema wapo watu wenye uwezo mkubwa wa akili, lakini kutokana na kutolala kwa saa sita mpaka nane mfululizo kwa siku, ubongo wao huishia kufanya kazi kwa asilimia 50 mpaka 60, ikilinganishwa na asilimia 100 iwapo wangelala inavyopasa.

Wakati dunia ikiadhimisha mwezi wa afya ya ubongo (Juni), wataalamu hao wanasema, ubongo ni muhimu sana kwa afya ya mwanadamu, hivyo ni lazima kuhakikisha kiungo hicho cha mwili kinapata virutubisho vifaavyo na kinapumzika vya kutosha.

Daktari bingwa mbobezi wa magonjwa ya ubongo na mfumo wa fahamu, Dk Edward Kija anasema mwili unahitaji kupumzika na ndipo ubongo hufanya kazi kubwa ya kurekebisha mfumo wa mwili.

Anasema ubongo unahitaji mapumziko ili utengeneze kumbukumbu vizuri na kupeleka taarifa vizuri kwenye maeneo yote yanayotakiwa, kulingana na ukubwa wa kihifadhi kumbukumbu, kama ilivyo ‘RAM’ katika simu.

“Inategemea upo katika hatua gani ya ukuaji, watoto wanapaswa kulala kati ya saa nane hadi 10 na watu wazima saa sita hadi nane mfululizo. Hii inahusisha pia kutoamka katikati kwenda chooni au kunywa maji au kucheza na simu.

“Kuna watu wanalala mapema lakini wanaamka mara mbili mpaka tatu. Binadamu anapolala mapema, ubongo wake hufanya kazi kwa kiwango chake bora cha asilimia 100, usipolala vizuri unafanya kazi chini ya hapo kwa asilimia 50 au 60. Kuna watu wangelala vizuri wangefanya zaidi wafanyavyo,” anasisitiza.

Dk Kija anasema kama mtu hapumziki vya kutosha muda mwingi, lazima ashindwe kufanya majukumu yake kama anavyopanga na muda mwingi atahisi amechokachoka.


Kazi za ubongo unapolala

Katika hili, wataalamu hawa wanasema kama ilivyo katika ofisi ambayo lazima mafaili mbalimbali yapangwe vizuri, ndivyo ubongo hurekebisha kila kitu binadamu anapolala.

Mkuu wa kitengo cha upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu ambaye pia ni daktari bingwa MOI, Lemery Mchome anasema ni muhimu kulala saa sita mpaka nane kwa mtu mzima, kwani licha ya ubongo kuwa na kazi ya kufikiri mchana, una kazi nyingine nyingi muhimu ambazo hufanyika usiku.

Ubongo una kazi nyingine mwilini ya kurekebisha vitu mbalimbali na kusimamia mifumo yote ya mwili.

“Mchana unapohangaika ubongo unafanya kazi, ikiwemo kupumua, kuhakikisha chumvi inakaa vizuri, presha iko vizuri na kinga ya mwili inafanya kazi vizuri. Kila kitu kinaendeshwa na ubongo.

“Unapofika muda wa kulala ubongo unaacha kufanya kazi za nje, unajibadilisha kuanza kushughulikia kazi za ndani, unaanza kuangalia viwango vya homoni kwenye mwili, kinga ya mwili kama iliharibiwa mchana na msongo wa mawazo unatengeneza viwango vinavyotakiwa,” anasema.

Anasema kuna kazi nyingi muhimu ubongo unafanya binadamu akiwa amelala, hivyo wanasayansi walipendekeza saa sita mpaka nane, utakuwa umefanya kazi zinazohitajika na mwili unakuwa salama kwa mujibu wa tafiti za kisayansi.

“Ukifuatilia sana unagundua ni kweli. Wanaume wanakufa mapema kuliko wanawake, mwanamume atapita baa, ataangalia mpira au filamu atalala kwa kuchelewa, lakini wanawake wengi hulala mapema, mwili wake unafanya kazi na kujirekebisha.

Hoja hiyo inaungwa mkono na Mtaalamu wa ubongo kutoka Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi Muhimbili (Muhas), Dk Mnacho Mohammed, anayesema usingizi ni muhimu ili ubongo uweze kufanya kazi na mwili uwe katika kiwango kizuri kiutendaji.

“Mtu anapolala, licha ya kwamba mwili unaendelea kuwa hai na shughuli nyingine za kupumua, mapigo ya moyo kuendelea na mifumo ya kusafisha taka, usingizi huurudisha ubongo katika mfumo na kujijenga upya, na ndiyo maana mtu asipolala anakuwa na msongo wa mawazo,” anasema Dk Mnacho.


Ufanye nini

Mbali na kulala, Dk Kija anafafanua njia nyingine za kuimarisha afya ya ubongo kuwa ni pamoja na kula matunda na mboga za majani, vyakula vya wanga na protini ili kusaidia chembe hai za kwenye ubongo kufanya kazi vizuri.

“Ukiwa na lishe nzuri, ubongo wako utaweza kufanya kazi vizuri, mwili unahitaji damu izunguke vizuri. Damu ndiyo inapeleka hewa ya oksijeni kwenye chembe hai za mwili wako, ili damu iweze kuzunguka vizuri,” anasema.

Anasema ili kuwe na mzunguko mzuri wa damu ni lazima mwili uwe na maji ya kutosha. Hivyo mzunguko mzuri wa damu mtu huupata iwapo anakunywa maji ya kutosha.

Pia Dk Kija anasema binadamu anahitajika aushughulishe mwili wake kwa kufanya mazoezi kwa angalau dakika 30 kwa siku.

“Unaweza kutembea, kukimbia, chochote kile angalau dakika 30 mwili wako utoke jasho, inasaidia kufungua mishipa ya hewa ili uweze kupumua hewa ya kambon dayoksaidi na kusaidia mwili wako upate oksijeni ya kutosha,” anasema.


Mambo ya kuepuka

Dk Kija anasema ili uwe na afya nzuri ya ubongo, unahitaji kuepuka matumizi ya pombe, kwa kuwa huenda kuathiri ufanyaji kazi wa chembe hai moja kwa moja, ambazo kwa hesabu zipo bilioni 10, ikiwa kila siku utakunywa pombe zitapungua na hivyo uwezo wa ubongo wako pia utapungua.

Pia anashauri kuepuka uvutaji wa sigara, akisema zinaenda kuathiri mishipa ya damu inayopeleka damu kwenye ubongo, na kuifanya ishindwe kutanuka na kusinyaa kuendana na presha ya moyo.

Anasema sigara huanza kutengeneza ukungu kwenye mishipa ya damu inayopeleka hewa ya oksijeni kwenye ubongo. Mishipa hiyo huhitaji kwa wingi lishe na hewa ya oksijeni, hivyo ukungu huo huifanya ikose hewa ya kutosha.


Magonjwa yanayoathiri ubongo

Mtaalamu huyo pia anataja baadhi ya maradhi kama presha, kisukari, uzito kupita kiasi kuwa ni vitu vinavyoathiri kiwango cha damu kinachokwenda kwenye ubongo na kuufanya ushindwe kufanya kazi.

“Maradhi yanayoathiri moja kwa moja akili na chembe hai za ubongo ni yale ya maambukizi na minyoo ambayo huathiri chembe hai kwenye ubongo, lakini kuna magonjwa ya kurithi nayo huenda kuua chembe hai za ubongo na kusababisha ushindwe kufanya kazi vizuri,” anasema Dk Kija.

Daktari bingwa wa magonjwa ya akili katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Said Kuganda anasema akili huwa inaugua, akimaanisha inaumwa yenyewe tu.

Dk Kuganda anasema licha ya akili kuugua, pia yapo magonjwa ambayo yakijitokeza yanaweza kuathiri akili, kwani huingilia mfumo wa fahamu kama Ukimwi, magonjwa ya kifafa na kaswende.

“Kaswende ina nafasi kubwa na ni maarufu na inawezekana kabisa dalili pekee ya ugonjwa huo ikawa ni upungufu kwenye akili. Watu wanaweza kuona dalili nyingi na wakapima wakaona kweli ni kaswende.

“Inaweza ikaja mwanzoni kabisa, ikawa ni usumbufu kwenye akili, watu wakahangaika kutibu akili kumbe wakawa wamesahau kupima hiyo kaswende, kwani ina uwezo wa kuleta athari kwenye akili, wadudu wale wanavamia ubongo,” anasema Dk Kuganda.

Anataja magonjwa mengine yanayoshambulia mfumo wa fahamu yanayoweza kuathiri utendaji kazi kuwa ni saratani, malaria na maambukizi mengine ya bakteria yanayoingia kwenye damu na kuingia kwenye ubongo.

“Watu wanaweza kupata hitilafu sababu wana magonjwa mengine ambayo yenyewe yanaweza kuingilia mfumo wa fahamu, akili ikachanganyikiwa au ikapata madhara, mfanohoma ya mapafu, Uviko19, mtu mwenye upungufu mkubwa wa virutubisho au madini yakipungua sana mwilini, anaweza kupata changamoto ya akili au akaugua akili,” anasema.

Dk Kuganda anasema hayo ni tofauti na magonjwa ya akili ambayo yanasababishwa na tatizo la afya ya akili, ikiwemo hofu, wasiwasi, huzuni na sonona ambayo husababisha akili kuchanganyikiwa.

“Ukiona mtu aliyechanganyikiwa kuna mambo kadhaa muhimu, ili useme huyu mtu amechanganyikiwa, huenda ana changamoto kidogo ya magonjwa ya akili.”

Dk Kuganda anasema hata magonjwa ya watoto yanaweza kujitokeza ambayo yanaweza kuathiri ukuaji wa akili.

“Mfano wanazaliwa na kupata hitilafu, lakini ubongo wao unakua na unatakiwa ubebe makuzi. Hapa akili haikui vizuri kutokana na hiyo shida, mfano kwenye utindio wa ubongo, usonji au kifafa au watoto wanazaliwa wanapata degedege za utotoni wanaathirika.

Anasema ikiwa hivyo, utakuta mwili unakua lakini akili inabaki nyuma.