Wanachama CCM, Chadema wapishana kauli Msigwa kuhamia CCM

Mkazi wa manisapaa ya Mpanda Katavi, Leonard Mayunga

Muktasari:

  • Mjadala wa Mchungaji Peter Msigwa kuhamia CCM umeendelea kuleta gumzo katika kila kona ya Tanzania.

Katavi. Siku moja baada ya aliyekuwa Mbunge wa Iringa Mjini kwa tiketi ya Chadema na Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa kuhamia Chama cha Mapinduzi (CCM), wanachama wa vyama hivyo wamepishana kauli kuhusu uamuzi huo.

Wakizungumza na Mwananchi Digital kwa nyakati tofauti leo Jumatatu Julai mosi, 2024, Amos Mgomelo, mwanachama wa Chadema amesema Chadema ni chuo cha kukuza viongozi na Msigwa si kiongozi wa kwanza kuondoka Chadema.

Anasema walikuwepo wengi na waliondoka, lakini bado chama hicho kinaendelea kuimarika.

"Kipindi cha nyuma Chadema tumeishi maisha magumu sana kwa kutokufanya siasa, lakini tumekivuka na sasa tupo tunaimarisha chama. Japo kuondoka kwake kutakuwa na pengo kubwa kwa sababu tumepunguza wanachama, lakini majukumu yake watu wapo watayafanya vizuri zaidi yake. Hilo hatuna wasiwasi nalo,” amesema Mgomelo.

Amedai kwa kipndi kirefu sasa CCM imeshindwa kukuza vipaji vya viongozi, ndiyo maana kinaelekeza nguvu kwenye kuwashawishi ambao wametengenezwa na Chadema wajiunge na chama hicho.

"Lakini nina jambo moja tu ambalo nataka nimwambie Mchungaji Msigwa, kama ameondoka kwa sababu alishindwa kwenye uchaguzi wa kanda, basi atakuwa ni mroho wa madaraka, ameongoza Kanda ya Nyasa miaka kumi kama mwenyekiti. Sasa kipindi hicho yupo madarakani hakukuwa na demokrasia kwenye chama, au baada ya kushindwa uchaguzi ndiyo kumeonekana hakuna demokrasia? Alitafakari hili akiwa huko huko CCM,” amesema.


CCM wafunguka

George Kizo, mwanachama wa CCM, Manispaa ya Mpanda amesema amefurahi kitendo cha Msigwa kujiunga na chama chao.

“Waache Chadema walolome, sisi tunachojua tumeongeza mwanachama makini na mwenye ushawishi mkubwa kwenye siasa zetu hapa nchini,” amesema Kizo.

Hata hivyo, Kizo amesema atamshangaa Msigwa kama atakuwa amejiunga na CCM kwa lengo la kutafuta maslahi binafsi.

“Nasema hivi kwa sababu tungemuelewa zaidi kama angekuja CCM miaka miwili iliyopita,  lakini amekuja baada ya kushindwa uchaguzi Chadema, lakini atambue tu kwamba chama chetu kina miongozo yake mizuri inayotuongoza hilo alizingatie,” amesema Kizo.

Amesema CCM ina watu wengi waliokipambania hadi hapa kilipo na ambao walijenga misingi imara inayokifanya kiendelee kuaminiwa na wananchi mpaka sasa.

Naye Leonard Mayunga, amesema Mchungaji Msigwa kilichomuondoa Chadema ameshakisema.

“Baadhi ya viongozi wa ngazi ya juu ndani ya Chadema wako kimaslahi zaidi, ndiyo maana wanawafanyia figisi kama alivyofanyiwa Msigwa, sasa mwanachama mwenye akili hawezi kudumu nacho ataona anapotezewa muda tu kama alivyoona Mchungaji Msigwa,” amesema Mayunga.