Walioshtakiwa wakidaiwa kumuua Mawazo waachiwa huru

Marehemu Alphonce Mawazo enzi za uhai wake. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Washtakiwa katika kesi hiyo namba 56/2023 Alfan Apolnari, Epafra Zakaria, Hashim Sharifu na Kalulinda Bwire wameachiwa chini ya kifungu cha 91 cha makosa ya mwenendo wa jinai.

Geita. Mahakama Kuu Kanda ya Geita imewaachia huru washtakiwa wanne waliokuwa wakikabiliwa na shtaka la kumuua kwa kukusudia aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo.

Hukumu hiyo imetolewa juzi Juni 25, 2024 na Jaji wa Mahakama hiyo, Graffin Mwakapeje baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka kuona hana nia ya kuendelea na kesi hiyo.

Washtakiwa katika kesi hiyo namba 56/2023 Alfan Apolnari, Epafra Zakaria, Hashim Sharifu na Kalulinda Bwire wameachiwa chini ya kifungu cha 91 cha makosa ya mwenendo wa jinai.

Awali, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Wakili Musa Mlawa akisaidiana na Deodatha Dotto aliieleza Mahakama kuwa chini ya kifungu cha 91, Jamhuri haina nia ya kuendelea na kesi hiyo.

Kufuatia ombi hilo, Jaji Mwakapeje aliridhia na kuwaachia huru chini ya kifungu cha 91 na kueleza kuwa Jamhuri wanaweza kuwakamata tena watakapowahitaji.

Upande wa utetezi umeishukuru Mahakama kwa uamuzi huo kutokana na wateja wao kukaa ndani kwa miaka tisa tangu wakamatwe mwaka 2015 na kuishukuru Serikali kwa kuona haja ya kutenda haki.

Washtakiwa hao walitetewa na mawakili wa kujitegemea, Rukia Marandu, Siwale Siyambi, Costantine Ramadhan na Beatrice Amos.

Juni 18, 2024, kesi hiyo ilianza kusikilizwa upya baada ya Mahakama ya Rufani iliyoketi Mwanza mbele ya majaji watatu, Ferdinand Wambali, Issa Maigena Leila Mgonya kutengua hukumu ya kesi hiyo na kuamuru ianze kusikilizwa upya baada ya kubaini kasoro za kisheria katika mwenendo wa kesi hiyo Mahakama Kuu.

Mahakama ya Rufani katika hukumu hiyo, imesema imebaini mwenendo wa kesi hiyo ulikiuka masharti ya kifungu cha 246(2) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA).

Desemba 24, 2020, aliyekuwa Hakimu Mwandamizi Mkazi Geita, Frank Mahimbali, aliyepewa mamlaka ya ziada kwa ajili ya kusikiliza kesi hiyo iliyopaswa kusikilizwa na Jaji wa Mahakama Kuu, aliwahukumu kunyongwa hadi kufa washtakiwa wanne katika kesi hiyo.

Hata hivyo, washtakiwa hao walikata rufaa Mahakama ya Rufani wakipinga kutiwa hatiani na adhabu hiyo.

Mahakama ya rufani katika hukumu iliyotolewa Agosti 30, 2023 ilibaini kuwa kulikuwa na kasoro za kisheria katika hatua za kumpeleka mtuhumiwa mahakamani (Committal Proceedings).

Katika hatua hiyo, kwa mujibu wa kifungu 246(2) cha CPA, sura ya 20 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019, inataka idadi ya mashahidi watakaoitwa na Jamhuri watajwe pamoja na vielelezo vya ushahidi vitakavyotumika, visomwe kwa washtakiwa.

Hata hivyo, Mahakama ya Rufani ilibaini katika kesi hiyo baadhi ya mashahidi hawakuorodheshwa na Jamhuri na maelezo ya baadhi ya washtakiwa waliyoyatoa polisi hayakusomwa kwenye hatua hiyo lakini mashahidi walitoa ushahidi mahakamani.