Serukamba akomalia miradi ya Maendeleo, atoa agizo Mufindi

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Peter Serukamba akizungumza katika kikao cha baraza maalum la kupitia Taarifa ya Mdhibiti Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika halmashauri ya Wilaya ya Mufindi

Muktasari:

  • Asema halmashauri zihakikishe zinapeleka   fedha kumalizia miradi ambayo haijakamilika kwa wakati, ili  itoe huduma kwa wananchi.

Mufindi. Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba, ameiagiza Halmashauri ya Wilaya Mufindi kuongeza nguvu katika usimamizi wa miradi ya maendeleo, ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati.

Serukamba ametoa maagizo hayo leo Jumatano Juni 26, 2024 kwenye kikao cha Baraza la Madiwani lililojadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2022/2023 unaoishia Juni 30, kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi.

Pia, Serukamba amesema kuwa taarifa hiyo ya CAG, imebaini kuna ujenzi wa majengo mbalimbali yenye thamani ya Sh1.3 bilioni  katika halmashauri hiyo, bado haujakamilika.

"Naagiza halmashauri kuhakikisha mnapeleka fedha kwa ajili ya kumalizia miradi hii ambayo bado haijakamilika kwa wakati," amesema Serukamba.

Amesisitiza halmashauri hiyo haipaswi kuanzisha miradi mipya kabla ya kumaliza miradi iliyopo.

Aidha, Serukamba amesisitiza halmashauri hiyo kufanyia kazi haraka maagizo sita yaliyobaki na hoja 26 ambazo majibu yake yanapaswa kuwasilishwa ofisi ya CAG, ili hoja hizo zifungwe.

"Kwa mujibu wa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, kwa hesabu zinazoishia Juni 30, 2023, halmashauri ilikuwa na jumla ya hoja 51, lakini wamefanyia kazi agizo moja kati ya saba na hoja 25 kati ya 26, hivyo niwaombe mkamalizie hizo ambazo zimebakia, ili hoja hizo ziweze kufungwa," amesema Serukamba.

Awali, akisoma taarifa hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Mashaka Mfaume amesema taarifa hiyo imehusisha hoja za kipindi cha nyuma, lakini baadhi ya miradi imeshakamlika.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Festo Mgina amesema wamepokea maelekezo yote yaliyotolewa na mkuu huyo wa mkoa na watayafanyia kazi.