Mzigo wa talaka kwa wanawake-1

Sada Hamad.

Muktasari:

  • Katika mijadala mingi, wazazi na wataalamu wa malezi wanakubaliana kuwa talaka inaweza kuwa na athari kubwa kwa watoto. Watoto wanapitia mabadiliko makubwa katika mazingira yao ya nyumbani ambayo yanaweza kusababishia msongo wa mawazo, huzuni na wakati mwingine hata matatizo ya kiakili na kihisia

Kumekuwa na malalamiko, majadiliano na tafiti nyingi kuhusu ongezeko la talaka nchini.

Wengi wanaamini na inavyoonekana moja kwa moja, kwamba suala hili la talaka linaathiri watoto kwa kiasi kikubwa.

Katika mijadala mingi, wazazi na wataalamu wa malezi wanakubaliana kuwa talaka inaweza kuwa na athari kubwa kwa watoto.

Watoto wanapitia mabadiliko makubwa katika mazingira yao ya nyumbani yanayoweza kuwasababishia msongo wa mawazo, huzuni na wakati mwingine hata matatizo ya kiakili na kihisia.

Tafiti zinaonyesha watoto wa wazazi waliotalakiana mara nyingi hukumbwa na changamoto kadhaa, ikiwamo ya kupata matokeo duni shuleni ikilinganishwa na wenzao wa familia zisizo na talaka.

Pia, kuna ongezeko la hali ya mmomonyoko wa maadili, na talaka zinaweza kuongeza hatari ya watoto kupata matatizo ya afya ya akili.

Lakini yapo maoni yanayosema talaka wakati mwingine inaweza ikasaidia kuepusha madhira makubwa zaidi kwenye familia.

Katika hali ambayo wazazi wanagombana mara kwa mara, talaka inaweza kuwa na faida kwa watoto kwa kuwaondolea mazingira ya dhuluma na vurugu.

Hata hivyo, ni muhimu kwa wazazi na jamii kwa jumla kushirikiana ili kupunguza athari hizi kwa watoto.

Lakini utafiti uliofanywa na Mwananchi visiwani Zanzibar na Mkoa wa Mtwara, umeonyesha mbali ya watoto kuwa waathirika wa kwanza, talaka pia huchangia mama wa watoto na familia yake alikotoka kuathirika kwa sababu ndugu yao anakuwa ametelekezewa watoto.

Mwananchi baada ya kuzungumza na watu kadhaa imebaini kati ya 10 ni mmoja aliyesema aliondoka akawaacha watoto na baba yao, ingawa baadaye inaonekana mwanamume aliwapeleka watoto hao kwa mama yao ambaye anawalea kwa kushirikiana na familia ya upande wake.

Mbali ya wimbi hilo la talaka, imeonekana wasichana walio wengi huingia kwenye ndoa kwa lengo tofauti ikiwamo kutafuta uhuru.

Akizungumzia madhila ya talaka, Halima Hamad Kassim anasema ameshaolewa mara tatu.

Na kila mwanaume amezaa naye  watoto watatu na sasa wote anawalea mwenyewe akisaidiana na mama yake mzazi.

 “Kina mama hawamalizi kulea, talaka zinatuathiri wanawake na watoto kwa sababu tunaachiwa ulezi tunalea peke yetu kusema kweli tunateseka sana.

“Miaka hii tunaachika mara kwa mara kwa sababu wanaume wengi wanawaacha wanawake bila mpangilio, ukiwa peke yako wanakuacha mkiwa mmeolewa wake wenza, unaachwa hatujui hasa nini kimetokea mpaka wanatuacha kila wakati, “anasema.

Sada Ali Hamadi anasema ameolewa mara sita; “ndoa yangu ya kwanza niliolewa Chwale, nikapata watoto wanne.”

Lakini anasema hakuifurahia ndoa yake, kwa sababu alikuwa anatumikishwa sana na mwanamume huyo ambaye baadaye alimpa talaka na akamrejesha nyumbani kwao na watoto wake.

Hata hivyo, anasema alipofika nyumbani kwao, baba yake akamwambia amrejeshee watoto mumewe.

“Nikamgomea nikamwambia mimi nimeishi kwa mateso sana, nikimuachia hawa wanangu si ndiyo atawaua,” anasema.

Hata hivyo, anasema baba yake akamwambia kama kaamua hivyo, basi hatampatia chakula cha kulisha wanawe.

Sada anasema alipoona hivyo, akaanza kufanya vibarua ili apate fedha za kuhudumia watoto wake na yeye mwenyewe.

Anasema maisha yake yalikuwa magumu sana, lakini mwisho wa siku alichukulia kawaida akaendelea kukomaa hivyo hivyo na wanawe.

Hata hivyo, anasema ilifikia mahali akaamua kuolewa tena na huko alibahatika kupata mtoto mmoja.

Bahati mbaya yule mumewe akafariki dunia, kwa kuwa mumewe alikuwa hana baba wala mama, akaamua kurudi nyumbani kwa wazazi wake.

“Nilikaa kwa miaka miwili pale nyumbani, nikaolewa tena na  nikabeba mimba nilipozaa tu nikaachika, nikaondoka na mwanangu. Nikaja nikaolewa tena, nikaachika kwa sababu mume alikuwa akinipiga sana, kuna siku akasema atanichinja baba yangu akasema nirudi nyumbani mwanaume asinifanye kama ng’ombe,” anasimulia mama huyo.

Bado anasema aliolewa tena hii ikiwa ni ndoa yake ya tano, huko nako amezaa watoto wawili lakini akaachika tena na mwanamume hakueleza sababu ya msingi kwa nini anamuacha.

Sada anasimulia (bila kukumbuka miaka kwa sababu hata mwaka wake wa kuzaliwa haujui) aliolewa  tena akakaa kwenye ndoa  miezi sita na kuachika.

 Anasema aliolewa tena mke mwenzake pia alimkataa akaachika. “Watoto wangu wengi hawakusoma, nami pia sikusoma wala sikumbuki nilizaliwa lini,” anasema Sada.

Anasema.  “Hizi talaka zinanifanya nijione sina bahati, ninahangaika tu tangu nimezaliwa mpaka sasa,”anasema Sada.

“Mtu akisema Serikali ishughulikie hili kwa uzoefu wangu naona itawafunga vijana wengi, hili suala la baadhi ya mabinti na wanawake kutaka kuolewa ili watoke kwenye mikono ya wazazi na kuwa huru linatuathiri wengi inaonekana sote tuliolewa kutaka huo uhuru ila si wote,” anasema.


Asikitika talaka zinavyowatesa

Akizungumza na Mwananchi kwenye mahojiano maalumu kuhusu wingi wa talaka, Saada Jumbe (36) mkazi wa Kusini Pemba anasema haelewi afanye nini na umri wake bado mdogo.

Anasema kuna siku aliamka asubuhi mumewe akamwambia hamtaki ajiandae amrudishe nyumbani kwao.

Na alipofika nyumbani kwa wazazi wake, mwanamume huyo akaishia nje na jioni akamtuma mdogo wake apeleke talaka mbili.

“Ndiyo alivyoniacha na watoto watatu mmoja akiwa na miezi minne,” anasema Saada na kuongeza:“Naiogopa ndoa, lakini siwezi kuzini, umri wangu mdogo kusema nitaachana kabisa na haya mambo, lakini sielewi nifanye nini,” anasema Saada.

Anasema ndoa ya  kwanza aliachika  kwa sababu za kifamilia, alikuwa haelewani na ndugu upande wa mumewe aliokuwa akiishi nao nyumba moja.

Anasema wakati anaachika alikuwa na mtoto mmoja na mume wake wa pili walikuwa hawaelewani.

“Alinioa mke wa pili, nilipozaa tu akaoa mke wa tatu kisha nikawa sina thamani tena, hanijali, haji zamu, hanihudumii wala kunijulia hali, nikamwambia aniache kwa sababu sikuona maana ya kuolewa tena,” anasema Saada.

Anasema wakati anaachika alikuwa ana mtoto wa miezi tisa na mwingine wa miaka mitatu kasoro.

Anasema mwanawe alipokuwa, akaolewa tena, “lakini ukiniuliza sababu ya kuachana na huyu mume wangu wa mwisho hata sina, aliamka tu akasema miye na yeye basi na ikawa basi.”

Hata hivyo, anasema baadaye alikuja kusikia kumbe alikuwa kaoa mke mwingine kwa siri kwa sababu alishawahi kusikia ana mwanamke mwingine, alipomuuliza alimkatalia.

“Nilimwambia siku nikipata uhakika miye mwenyewe nakupa talaka, nahisi aliona bora aniache kuliko nijue kuwa ameoa,” anasema.

Khamisi Haji Mbarouk, mkazi wa Mtambile pia anasema talaka zina sababu nyingi ambazo wanandoa pengine hawazizungumzii.

Anasema pia, watu hawajui kuwa kuoa hasa visiwani ni pata potea, “wasichana na wanawake huku kama hawajaolewa hawaruhusiwi kutoka kwao, hivyo ukisema unamuona ili apate uhuru anakubali, akifika nyumbani kwao anaanza visa ili umuache awe huru.

“Na wakiachika wanakuwa huru kweli ndiyo maana wanaolewa mara nyingi baada ya ndoa ya mwanzo, kwani wakiachwa hawaulizwi tena wanafanya wanachokitaka,” anasema.

Shaweji Mbwana anasema, “sitaki kukumbuka wanawari niliowaposa na kuwaoa kwa mapenzi mara mbili tofauti walichonifanya, huku wakiulizwa mahari wanataka kitanda na godoro hilo la kwanza, kwa wote nilinunua ila mmoja alitaka na seti ya dhahabu nikafanikiwa kununua cheni tu,”

“Kilichotokea sikudumu nao hawa wanawake, niliwaoa kwa nyakati tofauti lakini niliishi nao kwa amani miezi mitatu tu kisha walianza kudai talaka.

“Kila mmoja alipoondoka alisomba vitu vyake nilivyomnunulia miye na kwao kisha akapanga nyumba, nilichobaini walikuwa wananitumia kama daraja la kuwatoa kwao ili waishi maisha ya anasa ambayo nyumbani kwao ilikuwa ngumu,” anasema Mbwana kwa jazba kidogo.

Huku akiungwa mkono na vijana wenzake waliokuwa maskani eneo la Kukuu Kangani, Kusini Pemba Abdallah Pandu anasema kuwa, “Uliza hata talaka wao ndiyo wa kwanza kudai tena wanalazimika na kizogo juu, kwa sababu umeshamtoa kwao na vitu anavyo anataka kuwa huru.

“Kuna vitu kuhusu hili ongezeko la talaka havisemwi, wanalaumiwa wanaume kwa sababu ndiyo wanazitoa, lakini wanawake wanachangia sana maana walio wengi hasa wanawari hawaolewi kwa mapenzi.

“Hata ukifuatilia walio wengi wapo radhi wajigomboe ilimradi tu waachike, kwani malengo yao yanakuwa yametimiza. Ukioa na ukakosana kidogo na mkeo unawaza ndiyo walewale kwa kujihami usifike naye mbali akakusumbua unaamua umuache mapema, wanaponzana sana,” anasema Pandu.

“Nimeshaacha wanawake watatu ndani ya miaka saba na niliwaoa kwa ndoa na gharama, lakini nilishindwana nao, ila huyu niliyenaye sasa huu ni mwaka wa 12 na sifikirii kumuacha,” anasema Mtambile.

Anasema miongoni mwa aliowaacha, wawili waliondoka na watoto wawili kila mmoja na mmoja alizaa naye mtoto mmoja na wake zake hao wote waligoma kuwaacha watoto.

Mbarouk anasema hapendi maneno maneno. “Kosa dogo, basi utajuta unakuwa kama umeua walikuwa wanaongea sana halafu kama wanasubiri ukosee tu waanze, nikashindwa kuvumilia, ila wakiulizwa hawasemi hayo, mbona huyu nimekaa naye miaka yote hiyo,”anasema Mbarouk.


Usikose sehemu ya pili ya simulizi hii kesho. 

        

Makala haya yameandikwa kwa ufadhili Bill & Melinda Gates Foundation.