Malisa adakwa na Polisi mahakamani Kisutu, kesi yaahirishwa

Meya wa zamani wa Manispaa ya Ubungo Boniface Jacob aka 'Boni yai' akiwa na wafuasi wa Chadema katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kesi yake kuahirishwa. Picha na Hadija Jumanne

Muktasari:

  • Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa yao kati ya Machi 19 na Aprili 22, 2024 katika jiji la Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Ofisa Afya ya Jamii, Godlisten Malisa (38) anashikiliwa na Jeshi la Polisi baada ya kukamatwa kwenye viunga vya Mahakama ya Kisutu.

Malisa na Meya wa zamani wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob( 42) wanakabiliwa na kesi ya  jinai namba  11805/2024  yenye mashitaka matatu ya kuchapisha taarifa za uongo katika mtandao wa kijamii wa X (Twitter )na Instagram, kinyume cha sheria.

Malisa alikamatwa baada ya kutoka katika chumba cha mahakama, kwenye Mahakama ya Kisutu ambapo leo Juni 6, 2024 kesi hiyo ilipangwa kwa ajili washtakiwa wote kusomewa hoja za awali, baada ya upelelezi wa shauri hilo kukamilika.

Hata hivyo  Serikali  imeshindwa kuwasomea hoja za awali( PH), kutokana na mmoja wa washtakiwa kuchelewa kufika mahakamani hapo.

Awali, wakili wa Serikali Happy Mwakanyamale amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo, kuwa kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya washtakiwa kusomewa hoja za awali, lakini mshtakiwa mmoja hayupo mahakamani.

"Mheshimiwa hakimu, mshtakiwa wa pili katika kesi hii hayupo hapa mahakamani na shauri lilikuja kwa ajili ya kusomewa hoja za awali, hivyo kutokana na sababu hii, tunaomba upande mahakama upange tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea hoja za awali" amedai Wakili Mwakanyamale.

Mwakanyamale baada ya kueleza hayo, hakimu Swallo aliwauliza mawakili wa mshtakiwa huyo, Peter Kibatala na Hekima Mwasipu, alipo mteja wao, ambapo walidai kuwa yupo njiani anakwenda mahakamani hapo.

Kutokana na hali hiyo, Hakimu Swallo alisema kesi zinaanza kusikilizwa saa tatu asubuhi hivyo kitendo cha mshtakiwa kuchelewa kufika mahakamani hapo kitapelekea afutiwe dhamana.

Hakimu Swallo baada ya kutoa maelezo hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 4, 2024.

Muda mfupi baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, Malisa alifika mahakamani hapo na kuhojiwa na hakimu sababu ya yeye kuchelewa kufika mahakamani na maswali yalikuwa kama ifuatavyo.

Hakimu : Ulikuwa wapi mshtakiwa mpaka wakili wako Kibatala alikupigia simu ukasema umeshafika mahakamani?

Malisa: Mheshimiwa hakimu naomba unisamehe kwa kuchelewa.

Hakimu: Ulikuwa wapi?

Malisa : Nilianzia Hospitali ya Taifa ya Muhimbili( MNH) nina mgonjwa kule.

Malisa: Naomba unisamehe sana Mheshimiwa.

Hakimu: Siku nyingine ukirudia nakufutia dhamana, kwa sababu utaratibu unajulikana, kesi zinaanza kusikilizwa mahakamani kuanzia saa tatu kamili.

Malisa: Naomba unisamehe mheshimiwa.

Nje ya Mahakama

Washtakiwa baada ya kutoka ndani ya chumba cha mahakama, mshtakiwa Malisa alikamatwa na askari Polisi waliokuwa katika viunga vya mahakama na kumpeleka mahabusu.

Akizungumza na Mwananchi, Wakili wa utetezi, Hekima Mwasipu amedai kuwa mteja wao amekamatwa na kwa taarifa alizopata  anatakiwa kusafirishwa kwenda Kilimanjaro kwa madai kuwa ana mashitaka mengine huko.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, washtakiwa wameshtakiwa makosa yao, chini ya kifungu cha 16 cha sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 14 ya mwaka 2015.