Majaliwa atoa maagizo udhibiti dawa za kulevya, aonya matumizi ya ‘cha Arusha’

Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa akizungumza wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya kupinga matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya yaliyofanyika kitaifa katika Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.

Muktasari:

  • Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameonya matumizi ya bangi hususani maarufu kama ‘cha Arusha’ aliyodai kuwa utafiti unaonyesha ndiyo bangi hatari zaidi nchini kutokana na tabia yake ya kusababisha kilevi kupindukia na mvutaji kupoteza fahamu.

Mwanza. Wakati matumizi ya dawa za kulevya yakiathiri vijana zaidi ya 14,874 nchini, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza uandaliwe mpango wa uwezeshaji wa waraibu wa dawa za kulevya waliohitimu matibabu ili kuingia kwenye shughuli za ujasiriamali.

Majaliwa ametoa maagizo hayo kwa Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) pamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuandaa mpango huo.

Hayo ameyasema leo Jumapili Juni 30, 2024 Jijini Mwanza wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kupinga matumizi ya dawa za kulevya.

Majaliwa amemuagiza pia Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kupambana na Kutokomeza Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo kuendeleza operesheni dhidi ya dawa za kulevya nchini ikiwemo kufika kwenye vituo vya mabasi, bandari, vituo vya treni, sokoni na maeneo yenye mikusanyiko ili kutokomeza biashara hiyo.

“Kaeni mtengeneze mpango unaoweka wazi kwamba hawa waraibu wa dawa za kulevya wakimaliza matibabu wanaelekea wapi. Mkutane mara moja mtoe taarifa kwa Wakuu wa Mikoa (Ma RC) na Wakuu wa Wilaya (Ma DC) kuhusu uwezeshwaji huo. Mpango huo ueleze kwamba wanaohitaji kilimo na ufundi watawezeshwa vipi baada ya kumaliza matibabu ya Methadone,” amesema Majaliwa.

Katika kilele hicho kilichoenda sambamba na uzinduzi wa sera ya Taifa ya mapambano dhidi ya matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya  ya mwaka 2024, Majaliwa amewataka wazazi na walezi kuendelea kupiga vita matumizi na biashara hiyo haramu ili kujenga jamii yenye vijana salama, akionya matumizi yake yanachangia Taifa kuwa na vijana wasiozalisha na wategemezi.

Pia, amezipongeza Asasi zisizo za Kiraia (NGO) ikiwemo Tanzania Health Promotion Support (THPS) kupitia mradi wake wa ‘Afya Hatua’ unaofadhiliwa na Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na Ukimwi (PEPFAR) kupitia Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (CDC), kwa jitihada za kuwasaidia waraibu wa dawa hizo na walioambukizwa Virusi Vya Ukimwi (VVU).


Aonya ‘Cha Arusha’

Katika hatua nyingine Majaliwa ameonya vijana kujiepusha na matumizi ya bangi hususani bangi maarufu kama ‘Cha Arusha’ aliyodai kuwa utafiti unaonyesha ndiyo hatari zaidi nchini kutokana na tabia yake ya kusababisha kilevi kupindukia na mvutaji kupoteza fahamu.

“Dawa za kulevya zimeathiri vijana zaidi ya 14,874, hasa bangi, mirungi, Metaseptrin na Skanka. Lakini pia nimeshangazwa kufahamishwa kwamba bangi kumbe zina madaraja yake. Tunaelezwa kuwa bangi kali iko pale Arusha inaitwa ‘Cha Arusha’ ukiila jiandae kurukwa na akili na ukiitumia unalala hapohapo, dawa hizi si nzuri inaonekana mbegu zimesambaa sambaa. Usikubali kupewa bangi popote unaweza kupewa Cha Arusha ukalala hapohapo,” amesema Majaliwa.


Hali ya dawa za kulevya nchini

Kwa mujibu wa Kamishna Jenerali wa DCEA Lyimo, kwa kipindi cha kuanzia Juni, 2023 hadi Mei, 2024 mamlaka hiyo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama nchini ilikamata zaidi ya kilogramu milioni 2 za dawa za kulevya, kiasi kinachotajwa kuwa kikubwa kukamatwa katika kipindi cha miaka 11 iliyopita tangu mwaka 2012 hadi 2022.

 “Ni mara tatu zaidi ya jumla ya dawa za kulevya zilizokamatwa kipindi cha miaka 11 kuanzia mwaka 2012 hadi 2022 ambazo kwa kipindi hicho zilikamatwa kilogramu 660,465.4 lakini kwa kipindi cha mwaka mmoja na miezi mitano imekamatwa kilogramu 200,050,000,”amesema.


Amesema kilogramu hizo zilihusisha watuhumiaji 14,874 kati yao wanaume wakiwa ni 13,685 na wanawake 1,189 huku, akitaja dawa za kulevya zilizokamatwa kwa kipindi hicho ni  bangi kilogramu zaidi ya 1.8 milioni, mirungi kilogramu 211,788.62, Metaseptrin kilogramu 2,936.49, Heroini kilogramu 1,549.78, Kokeini kilogramu 3.13 na bangi ya kusindikwa (skanka) kilogramu 425.66

Amesema mamlaka hiyo imefanikisha kuvunja na kudhoofisha mitandao mikubwa ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya kwa kuwakamata lakini pia kudhibiti na kuzuia kemikali bashirifu zaidi ya kilogramu 157,738.55 pamoja na lita 1,000 zilizokuwa ziingizwe nchini kinyume cha sheria.


“Kemikali hizo endapo zingechepushwa zingeweza kutumika kutengeneza dawa za kulevya, vilevile mamlaka ilifanikisha uteketezaji wa ekari 2,666.3  za mashamba ya bangi na ekari 535 za mashamba ya mirungi. Pia kubaini viwanda viwili vidogo vya kuchakata na kufunga bangi mkoani Mara na viwanda vidogo viwili kimoja cha kutengeneza biskuti za bangi eneo la Kawe na kingine cha kuchakata bangi eneo la Mbezi Beach jijini Dar es Salaam vilibainika na kuchukuliwa hatua za kisheria,” amesema Lyimo.

Ameongeza pia kwa kipindi cha mwaka 2023 hadi Mei 2024 jumla ya mashauri mapya 1,417 yenye makosa mbalimbali ya dawa za kulevya yamefunguliwa mahakamani huku,  kati ya mashauri hayo 1,359 yametolewa maamuzi na Jamhuri kushinda mashauri 983 sawa na asilimia 72.3.

Amesema mikoa inayoongoza kwa kilimo na uzalishaji wa dawa za kulevya ni Morogoro, Mara, Arusha na mikoa ya Kilimanjaro na Tanga ikiwa ni vinara wa kilimo cha dawa ya kulevya aina ya mirungi.

“Kwa upande wa matumizi hadi sasa dawa ya kulevya aina ya bangi inaongoza kwa kutumiwa zaidi ikifuatiwa na heroine, mirungi na dawa tiba zenye asili ya kulevya. Matumizi ya bangi husababisha madhara zaidi duniani  kuliko dawa zingine za kulevya kwa kuwa mtumiaji anaweza kupata magonjwa ya akili, mapafu na  saratani,”amesema Lyimo


Kanda ya Ziwa

Lyimo amesema katika operesheni zilizofanywa na mamlaka hiyo kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ilifanikisha kuteketeza ekari 884 za mashamba ya bangi, zilihusisha ukamataji wa magunia 967 na kilo 102 za bangi, kilogramu 59.4 za mirungi, heroine na dawa tiba zenye asili ya kulevya gramu 602.9

“Ukamataji huu ulizalisha kesi 64 zilizohusisha jumla ya watuhumiwa 161. Operesheni zaidi zinaendelea katika ukanda huu ili kuhakikisha tunatokomeza uzalishaji, biashara na matumizi ya dawa za kulevya,” amesema.

Aidha Lyimo amesema kwenye dawa za kulevya kuna kemikali hatarishi zenye uwezo wa kusababisha kansa na magonjwa ya figo. Hivyo, amesema Mamlaka imeendelea kuimarisha udhibiti na kuchukua hatua za kisheria kwa wanaojihusisha na biashara hiyo.


Jitihada za Serikali na wadau

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama amesema Serikali imenunua mashine ya kisasa kwa zaidi ya Sh2 bilioni inayofanya uchunguzi wa haraka wa viashiria vyote vinavyotakiwa kutolewa sampuli zitakazothibitisha uwepo wa matumizi ya dawa za kulevya.

“Mashine hiyo ya kisasa ina uwezo wa kuchukua sampuli zaidi ya 250 kwa saa 24 na kutoa majibu na kupeleka ushahidi ili hatua ziweze kuchukuliwa katika mapambano haya, tumewekeza pia ujuzi wa watumiaji wa mashine hizo kwenye maabara yetu,”amesema.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa THPS, Dk Redempta Mbatia amesema kupitia mradi wa ‘Afya Hatua’ unaotekelezwa katika mikoa ya Pwani na Tanga wamefanikiwa kutoa huduma za kinga, tiba na matunzo kwa waraibu 2,442 wa dawa za kulevya katika mpango wa MAT, na kati yao 1,426 bado wanaendelea na matibabu.

“Pamoja na huduma za MAT, waraibu wote waliojiandikisha waliweza kupata ushauri nasaha na upimaji wa VVU. Kati ya hao, watumiaji dawa za kulevya 122 waligundulika kuwa na VVU na mara moja walianza kupata huduma za tiba na matunzo katika kliniki za tiba na matunzo (CTC) zilizopo maeneo yao. Huduma hizi zinasaidia sio tu kuokoa maisha bali pia kuboresha ustawi wa jamii tunazohudumia,” amesema Dk Redempta.

Wakati huo, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la ICAP Tanzania, Haruka Maruyama amesema shirika hilo litaendelea kutafuta miradi na fedha zitakazosaidia kufanikisha mapambano dhidi ya biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya nchini.

"Tumekuwa tukishirikiana na Serikali ya Tanzania kwa kipindi kirefu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, matibabu ya VVU na homa ya ini. Tutaendelea kutafuta fursa mbalimbali ili kuhakikisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini Tanzania yanafanikiwa," amesema Maruyama.