DC, RPC watofautiana maagizo ya Makonda mtoto aliyelawitiwa Arusha

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda

Muktasari:

  • Mtoto huyo inadaiwa alikuwa anafanyiwa vitendo hivyo na watoto watatu wa  jirani zake huko kata ya Muriet jijini Arusha, ameanza kupata matibabu katika Hospitali ya Rufaa Mount Meru baada ya kubainika kuharibika vibaya sehemu za haja kubwa hadi kufikia hatua ya kujisaidia damu.

Arusha. Mkuu wa Wilaya ya Arusha Felician Mtahengerwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha wametofautiana kuhusu maelekezo ya kuwakamata na kuwachukulia  hatua kali za kisheria watuhumiwa wote wa tukio la ulawiti wa mtoto wa miaka mitatu.

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Felician Mtahengerwa

Wakati kamanda wa polisi mkoa huo akisema watuhumiwa hawajakamatwa kutokana na umri wao, mkuu wa wilaya alisema walishakamatwa na taratibu zinakamilishwa ili wafikishwe mahakamani.

Agizo hilo lilitolewa na  Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda.

Mtoto huyo inadaiwa alikuwa anafanyiwa vitendo hivyo na watoto watatu wa  jirani zake huko kata ya Muriet jijini Arusha, ameanza kupata matibabu katika Hospitali ya Rufaa Mount Meru baada ya kubainika kuharibika vibaya sehemu za haja kubwa hadi kufikia hatua ya kujisaidia damu.

Hali ya mtoto huyo iliyoibuliwa na mama yake mzazi, katika kliniki iliyokuwa ikiendeshwa na Makonda, Jeshi la Polisi walipewa maagizo ya kuwakamata watuhumiwa wote wanaohusika na tukio hilo.

Mbali na hilo Makonda pia alimtaka Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Felician Mtahengerwa kufuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa maagizo hayo ya wahusika kukamatwa ndani ya saa 24, lakini mtoto apewe matibabu.

Akizungumza leo Juni 6, 2024 Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Justine Masejo amesema, wameshindwa kuwakamata watuhumiwa kutokana na umri wao kuwalinda kwa mujibu wa sheria.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo

"Kulingana na sheria za nchi, watuhumiwa wale wako chini ya umri wa kushtakiwa makosa ya jinai, kwani mmoja ana tisa na mwingine miaka sita ila kuna namna wanashughulikiwa na ustawi wa jamii" amesema SACP Masejo.

Wiki iliyopita,  Mtahengerwa aliwaambia waandishi wa habari kuwa watuhumiwa wote wanaohusika na tukio hilo, wamekamatwa na wanasubiri upelelezi wa Jeshi la Polisi ukimamilika wapelekwe mahakamani.

"Katika tukio hilo tumefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wote waliohusika kumlawiti mtoto huyo na hatua za awali za kisheria zimeanza na watafikishwa mahakamani."alinukuliwa akisema Mtahengerwa.

Awali ilivyokuwa

Katika kliniki ya Makonda Aprili 10, 2024 iliyofanyika kwenye  viwanja ilipo ofisi yake, mama wa mtoto aliwatuhumu watoto wa jirani kuhusika na tukio hilo wenye umri kati ya miaka sita, tisa na 11.

Mbali na tuhuma hizo, mama huyo alisema kuwa alikwenda katika kituo cha Polisi Muriet kupata msaada wa watuhumiwa kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria bila mafanikio, zaidi ya kuambulia matusi na maneno ya kashfa na kejeli kutoka kwa askari Polisi.

Alisema mtoto wake alianza kufanyiwa vitendo hivyo Machi 22,2024 na watoto hao wote watatu.

"Baada ya kugundua kitendo hicho, nilienda Kituo cha Polisi Muriet kutoa taarifa na kupata hati ya matibabu (PF3) ambapo nilimpeleka mtoto Hospitali ya Muriet na baada ya majibu ya vipimo kuthibitisha kuwa ni kweli walinipa rufaa ya kwenda Hospitali ya Mount Meru" Alisema.

Alisema kuwa baada ya majibu alirudi Polisi kutaka hati ya kuwakamata watuhumiwa (RB) ambapo walikwenda kukamatwa na kulala kituoni kwa siku moja kabla ya kuachiwa kwa dhamana ya wazazi wao.

"Baada ya kuachiwa wazazi wao wakaja hadi nyumbani kwangu wakanza kunitishia maisha, nikarudi tena kituoni kuelezea wakatikia bila kuchukuliwa hatua zozote za kisheria, na nilirudi tena wakaanza kunitukana na kunifukuza kituoni hapo na maaskari wa Muriet, wakidai nasumbua tena nina kiherehere" alisema mama huyo na kuanza kulia.

Alisema kuwa hata hospitali alikokwenda kupata tiba ya mtoto hawataki tena kumsaidia zaidi ya kumpa dawa za uongo, huku wakimfukuza asirudi tena.

"Mtoto wangu ameharibika vibaya sehemu za haja kubwa, na inabidi sasa nirudi kumfunga pampasi kutokana na kujisaidia hovyo tena damu, na hospitali nao hawataki kunisaidia wananifukuza wanasema jambo hili ni siri ila mimi nitaenda kutangaza,"alisema mama huyo na kuongeza.

"Hata dawa za mtoto sijapewa naambiwa ni siri nisiseme mtoto amefanyiwa hivyo, hivi kweli mtoto wangu anaharibiwa kiasi hiki naambiwa nisiseme, wanabaki kunigombeza kila mahali, kwa sababu tu sina ndugu anayenifuata kituoni wala hospitali bali wananiona tu mimi,  wananionea mkuu" alisema mama huyo na kuangua kilio upya kwa nguvu.


Maagizo ya Makonda

Kutokana na tukio, Makonda alitoa maagizo matano ikiwemo kuhakikisha watuhumiwa wote wanakamatwa ndani ya saa 24.

"Sasa naomba nitoe maagizo, kwanza Muriet si iko hapa Jiji, tunaye Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) nawapa saa 24 tafuteni wahalifu na hatua kali za kisheria zianze kuchukuliwa dhidi yao" alisema Makonda.

Makonda pia alimtaka mama wa mtoto huyo kuhakikisha anapeleleza majina ya askari hao waliokuwa wanamkashifu na ampatie kwa njia ya simu ambayo alimpa namba yake.

"Pili nataka askari wote waliokuwa wanakupa kauli ambayo sio nzuri, fanya ufanyavyo unipe majina yao na nakupa namba yangu, na tatu OCD hakikisha ulinzi wa huyu dada"alisema Makonda.

Agizo la nne Makonda alimtaka Mganga Mkuu wa Mkoa kuhakikisha anawasilisha ripoti ya vipimo vyote alivyofanyiwa mtoto huyo.

"Agizo la nne RMO, kote alikopita na mtoto wake akapimwa nataka hiyo ripoti, na mwisho nataka dawa ya kumtibu mtoto mdogo wa miaka mitatu aliyelawitiwa na kuharibika apewe na mtoto apone"

Akizungumza leo Juni 6, 2024 na Mwananchi Digital, mama wa mtoto huyo amesema kuwa anamshukuru Mungu mtoto wake amepata dawa na anaendelea vizuri lakini bado watuhumiwa wa tukio hilo hawajakamatwa.