Baba adaiwa kumbaka maharimu wake mwenye miaka mitano

Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita Safia Jongo.

Muktasari:

  • Mtuhumiwa huyo anadaiwa kumlaghai mwanaye wa kike mwenye umri wa miaka mitano. Polisi wameshafanya upelelezi hivyo muda wowote mhusika atafikishwa mahakamani.

Geita. Jeshi la Polisi mkoani Geita limewakamata watuhumiwa 755 wa makosa mbalimbali ya kihalifu akiwemo Msauz Bakari (34), mchimbaji wa madini katika Kijiji cha Uyovu kilichopo wilayani Bukombe anayetuhumiwa kuzini na maharimu wake mwenye umri wa miaka mitano.

Katika taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi mkoa wa Geita inaeleza Juni 16, 2024 saa 4:30 usiku katika Zahanati ya Uyovu, zilipatikana taarifa za mtoto wa kike mwenye umri wa miaka mitano kuingiliwa kimwili na baba yake.

Mtuhumiwa huyo anadaiwa kumlaghai mwanaye kuwa atampa zawadi na kumfanyia ukatili huo. Upelelezi wa shauri hilo umekamilika na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa.

Katika taarifa hiyo ya polisi iliyosainiwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo, inasema kwa Mei pekee, jeshi hilo lilikamata watuhumiwa 754 kwa makosa 150 ya kihalifu yakiwemo ya kupatikana na mali za wizi.

Makosa mengine ni kukutwa na dawa za kulevyaĀ  kilo 16 na gramu 826 za banghi, kuingia nchini bila kibali, kukutwa na pombe moshi lita 103, wizi wa mafuta ya dizeli lita 195, wizi wa mifugo pamoja na makosa ya ukiukwaji wa maadili.

Jeshi hilo pia limefanya operesheni ya kukamata pikipiki zilizohusika na uhalifu na kufanikiwa kukamata watuhumiwa 41 wakiwa na pikipiki 44 zinazotumiwa katika matukio ya uhalifu.

Katika tukio jingine, mwanamke ambaye hajafahamika jina, anasakwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita kwa tuhuma za kumtelekeza mtoto mchanga anayekadiriwa kuwa na siku tatu katika Hospitali ya Mtakatifu Pio Maganzo iliyopo wilayani Bukombe mkoani humo.

Tukio hilo limetokea Juni 16, 2024 saa 6 usiku baada ya mwanamke huyo kufika hospitali na kuwaeleza walinzi kuwa anataka huduma za kitabibu na alipoingia alimuacha mtoto kwenye chumba cha ibada.

Inadaiwa baada ya muda mfupi, alirudi bila mtoto na kuwaeleza walinzi kuwa anakwenda kuchukua pesa kwa ndugu yake aliyeko nje ya hospitali na baada ya kutoka alipanda pikipiki na kuondoka.

Kwa mujibu wa polisi, mtoto huyo amehifadhiwa sehemu salama kwa matunzo na anendelea vizuri.