Wakulima wa ufuta Kilwa walalamikia mfumo wa TMX

Wakulima wa zao la ufuta wakiwa kwenye mnada wa pili ambao umefanyika katika kijiji cha Njinjo Amcos ya Matandu Wilayani Kilwa leo Juni 25, 2024. Picha na Bahati Mwatesa

Muktasari:

  • Jumla ya tani 4,400 zimeuzwa kwenye mnada wa pili wa Chama Kikuu cha Lindi Mwambao, katika AMCOS ya Matandu, Wilaya ya Kilwa kwa bei ya juu ya Sh3,490 na chini Sh3,340 kwa kilo moja

Kilwa. Wakulima wa ufuta kutoka Wilaya ya Kilwa wameiomba Serikali kuangalia upya mfumo wa TMX kwa kuwa umekuwa sio rafiki katika biashara ya zao hilo.

Akizungumza baada ya mnada wa ufuta uliofanyika leo Jumanne, Juni 25, 2024, mkulima kutoka Kijiji cha Njinjo, Abdulkarim Mkanile amesema bei ya ufuta imeshuka kutoka Sh3,640 mnada wa kwanza hadi kufikia Sh3,490 kwenye mnada wa pili.

Amesema mfumo wa TMX hauwanufaishi wakulima kwa sababu unashusha bei kwa haraka.

Mkanile amesema mfumo wa zamani ulikuwa mzuri zaidi kwa sababu mnunuzi hakuwa na uwezo wa kuona bei iliyowekwa na mnunuzi mwenzake.

"Mfumo wa boksi ulikuwa mzuri sana; mnunuzi anaweka bei ya kumzidi mwingine. Lakini sasa kila mnunuzi anaona bei iliyowekwa na mwingine kwenye mtandao, hivyo wanapunguza bei haraka sana. Hivi sasa tupo mnada wa pili na bei zimeshuka haraka sana," amelalamika Mkanile.

Wakulima wa zao la ufuta wakiwa kwenye mnada wa pili ambao umefanyika katika kijiji cha Njinjo Amcos ya Matandu Wilayani Kilwa leo Juni 25, 2024. Picha na Bahati Mwatesa

Mkulima Abdalah Hassan amesema hali ikiendelea hivyo, huenda baadhi ya wakulima wakazuia ufuta wao ndani na kutafuta masoko nje ya ushirika.

“Tunatumia gharama kubwa kulima haya mashamba tukitegemea kupata faida lakini kinachoonekana sasa, bei itaendelea kuporomoka, huu mfumo si rafiki,” amesema Hassan.

Hata hivyo, Ofisa Ushirika wa Mkoa wa Lindi,  Projestus Pascal amewataka wakulima kupeleka ufuta bora ili kuongeza uwezekano wa bei kupanda kwenye minada ijayo.

"Bei za ufuta zinashuka lakini niwaombe wakulima wajitahidi kupeleka ufuta bora ghalani ili mnunuzi aweze kuvutiwa nao na kuongeza bei kwenye mnada ujao," amesema Pascal.

Maonyesho Saidi amesema wanunuzi wameombwa kulipa fedha za wakulima kwa wakati na wasisubiri kulipa karibu na minada mingine.

"Sisi tunachotaka ni kulipwa kwa wakati ili tuweze kuwaandaa watoto wetu wanaofungua shule mapema. Malipo yakichelewa wanakuwa wanatuumiza sana," amesema Saidi.

Jumla ya tani 4,400 zimeuzwa kwenye mnada wa pili wa Chama Kikuu cha Lindi Mwambao, katika AMCOS ya Matandu, Wilaya ya Kilwa kwa bei ya juu ya Sh3,490 huku ya chini ikiwa Sh3,340 kwa kilo moja ya ufuta.