Tiketi za ubingwa Liverpool ni milioni 11

Muktasari:
- Umuhimu wa mechi hii sio tu Liverpool kuchukua ubingwa, bali mashabiki kupata nafasi ya kuwa uwanjani wakati timu yao ikitafuta ubingwa huo, ambao wanaonekana kuwa na asilimia nyingi za kuupata.
LIVERPOOL, ENGLAND: LEO ni siku maalumu kwa mashabiki wa soka wa Liverpool. Licha ya ukweli huenda ikawa siku ya maumivu kwa majirani zao Everton na wapinzani wao Manchester United, lakini hii ni siku muhimu sana kwa majogoo.
Umuhimu wa mechi hii sio tu Liverpool kuchukua ubingwa, bali mashabiki kupata nafasi ya kuwa uwanjani wakati timu yao ikitafuta ubingwa huo, ambao wanaonekana kuwa na asilimia nyingi za kuupata.
Liverpool leo itacheza dhidi ya Tottenham na inahitaji alama moja tu ili kutawazwa kuwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu England msimu huu ikiwa ni taji lao la kwanza tangu mwaka 2020.

Awali wakati wanachukua EPL kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30, Liverpool haikupata nafasi ya kusheherekea na mashabiki wao kwa sababu ya janga la virusi vya Corona lililokuwa linaiandama dunia kwa wakati huo.
Raundi hii, mashabiki watapata nafasi hiyo ikiwa watachukua ubingwa lakini, bado kuna gharama kubwa ya kulipa ili kuingia Anfield leo.
Licha ya juhudi za kudhibiti madalali na tovuti za uuzaji wa tiketi kwa bei ya juu, tiketi zimeanza kuuzwa kwa karibu Pauni 700 (Sh2.5 milioni), kwa mujibu ya Daily Mail na hiyo ndiyo ilikuwa tiketi ya bei ya chini kabisa sokoni.
Tovuti ya uuzaji wa tiketi ya LiveFootballTickets inauza tiketi za mchezo huu kwa Pauni 3248 (Sh11 milioni) kutoka Pauni 61 ambayo ndio ilikuwa bei ya awali.
Pia tiketi zilizokuwa zikiuzwa Pauni 30, sasa zinauzwa Pauni 414 kupitia tovuti hiyo.
Liverpool ina mashabiki 28,000 ambao walinunua tiketi za msimu mzima, pia kuna mashabiki 11,000 ambao hununua tiketi maalumu kila mechi na timu za ugenini hupewa nafasi ya mashabiki 3000 na nafasi zilizobakia tiketi zake huuzwa kwa mashabiki ambao wamejisajili kupitia tovuti yao.
Akizungumza kuelekea mechi hiyo, Slot alisema: “Kila mtu anatazamia Jumapili, lakini tunajua bado kuna kazi ya kufanya, tunahitaji walau kupata pointi moja. Tunafahamu hilo.”
Liverpool walikuwa na matumaini ya kutwaa mataji mengi Machi mwaka huu, lakini vipigo kadhaa vilisababisha matumaini yote kuelekezwa kwenye Ligi Kuu.
Baadhi ya wachezaji wa kikosi cha sasa kama Cody Gakpo hawakuwepo wakati timu hiyo inatwaa ubingwa mwaka 2020.
Mbali ya mchezo huu utakaopigwa kuanzia saa 12:30 jioni, leo pia kutakuwa na mechi nyingine ya ligi kati ya Manchester United na Bournemouth itakayokuwa nyumbani itakayoanza saa 10:00 jioni.