Kaseja ana kibarua cha 2015-2016

Muktasari:
- Kagera kwa sasa inashika nafasi ya 15 ikiwa na pointi 22, baada ya kucheza mechi 27, nyuma ya Tanzania Prisons na Pamba Jiji zilizopo nafasi ya 13 na 14 zikiwa na pointi 27, ikisakwa timu moja itakayoungana moja kwa moja na KenGold iliyoshuka mapema ikiwa na mkiani na pointi 16 tu.
KOCHA wa Kagera Sugar, Juma Kaseja kwa sasa presha inazidi kupanda kutokana na nafasi iliyopo timu hiyo inayopambana na kutoshuka daraja, ingawa ikiwa atainusuru kupitia mechi tatu zilizobakia inaweza kujirudia rekodi ya msimu wa 2015-2016.
Kagera kwa sasa inashika nafasi ya 15 ikiwa na pointi 22, baada ya kucheza mechi 27, nyuma ya Tanzania Prisons na Pamba Jiji zilizopo nafasi ya 13 na 14 zikiwa na pointi 27, ikisakwa timu moja itakayoungana moja kwa moja na KenGold iliyoshuka mapema ikiwa na mkiani na pointi 16 tu.
Pointi 22 ilizonazo Kagera, kama itashinda mechi hizo tatu ilizonazo mkononi, itafikisha pointi 31, ambazo ni sawa na zile za msimu wa 2015-2016 na kikosi hicho kiliponea chupuchupu ya kushuka daraja, ingawa itategemea na wapinzani wanaochuana katika kukwepa playoff kubaki Ligi Kuu.
Msimu huo wa 2015-2016, Kagera ilikuwa nafasi ya 12 na pointi hizo 31 baada ya kucheza mechi 30, nyuma ya Coastal Union iliyokuwa na pointi 22, African Sports (26) na Mgambo Shooting (28) zote za Tanga zilizoshuka daraja kwa pamoja, ikiwa ni rekodi ya aina yake kwa timu za mkoa mmoja kushuka.
Kwa msimu huo, Kagera ilishinda mechi nane, sare saba na kupoteza 15 kati ya 30 ilizocheza, huku msimu huu wa 2024-2025 katika mechi 27 ilizocheza imeshinda tano, sare saba na kupoteza 15, jambo linalosubiriwa kama rekodi hiyo itajirudia tena au la, safari hii kocha akiwa ni Kaseja.
Katika mechi hizo tatu zilizobakia, Kagera itakuwa na kibarua dhidi ya Mashujaa Mei 12 kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, huku duru la kwanza zilipokutana Novemba 30 mwaka jana mjini Kigoma zilitoka sare ya bao 1-1, kisha itaenda hadi Ruangwa Lindi kuifuata Namungo siku ya Mei 21.
Mechi ya kwanza kwa timu hizo kukutana msimu huu ilipigwa Desemba 11, 2024 mjini Bukoba na kumalizika kwa sare ya 1-1 na Kagera itamaliza msimu kwenye Uwanja wa KMC, kuvaana na Simba siku ya Mei 25, ikirejea mechi ya Mei 19, 2018 ambapo Simba ilitibuliwa rekodi kwa kufungwa bao 1-0, huku Juma Kaseja enzi hizo akiichezea Kagera, alipangua penalti ya Emmanuel Okwi dakika za jiooni.
Katika mechi ya kwnza iliyopigwa DEsemba 21, 2024, Simba iliifumua Kagera kwa mabao 5-2 na kocha Kaseja aliyepewa timu hivi karibuni alisema, mechi zote ni ngumu ila watahakikisha wanapambana hadi tone la mwisho, huku akiwataka wachezaji kutocheza kwa hofu ya aina yoyote, kwani kwa kufanya hivyo itawaondolea hali ya kujiamini mapema.
Kaseja aliyewahi kuzichezea Yanga, Simba na timu ya taifa ‘Taifa Stars’, alijiunga na kikosi hicho kama kocha mkuu Machi 4, 2025, baada ya kuondoka kwa Mmarekani Melis Medo Februari 25, 2025, kutokana na mwenendo mbovu wa matokeo kikosini.
Tangu atangazwe rasmi Machi 4, Kaseja amekiongoza kikosi hicho katika michezo mitano ya Ligi Kuu ambapo kati ya hiyo, ameshinda miwili mfululizo, akianza na 2-1, dhidi ya Pamba Jiji, Machi 7, kisha pia (2-1) v Coastal Union FC, Aprili 3.
Baada ya hapo, akapoteza michezo mitatu mfululizo akianza na kichapo cha 1-0, dhidi ya Tanzania Prisons Aprili 6, (2-0) v Dodoma Jiji, Aprili 9, kisha 4-2 mbele ya Azam FC, Aprili 19 na kuzidi kuongeza presha ya kikosi hicho kama kitabakia.