KMC yairudisha Simba mjini Tabora

Muktasari:
- Mechi hiyo imepangwa kupigwa Mei 11, huku KMC ikiwa wenyeji na imeombwa ukapigwe Ali Hassan Mwinyi, mjini Tabora kwa nia ya kutaka kuwapunguzia uchovu wa safari wachezaji ambao watakuwa na mechi siku tatu baadae mjini humo dhidi ya Tabora United.
KMC iliyopo nafasi ya 11 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara imetangaza kupeleka mechi yao ya marudiano dhidi ya Simba mjini Tabora, huku mabosi wa klabu huyo kupitia Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Daniel Mwakasungula wametoa ufafanuzi wa sababu ya kufanya hivyo.
Mechi hiyo imepangwa kupigwa Mei 11, huku KMC ikiwa wenyeji na imeombwa ukapigwe Ali Hassan Mwinyi, mjini Tabora kwa nia ya kutaka kuwapunguzia uchovu wa safari wachezaji ambao watakuwa na mechi siku tatu baadae mjini humo dhidi ya Tabora United.
Awali mechi hiyo ilipangwa kuchezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge, Dar es Salaam, ingawa viongozi wa KMC wametumia kanuni ya Ligi inayoruhusu kubadilisha viwanja vya mechi mbili za nyumbani kwa kuupeleka mjini Tabora kwa vile wana pambano jingine huko huko.
“Mei 11 tunacheza na Simba na baada ya hapo tuna mechi nyingine ugenini dhidi ya Tabora United siku ya Mei 14, kwa afya ya wachezaji tumeona ni vizuri kuchagua Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi ambao tutacheza mechi zote mbilii,” alisema Mwakasungula.
Kitendo cha KMC kuupeleka mchezo huo Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora, kinarudisha kumbukumbu ya Desemba 24, 2021 wakati miamba hiyo ilipokutana katika Ligi Kuu, huku kikosi cha Simba kikiibuka na ushindi mnono wa mabao 4-1.
Katika mechi hiyo mabao ya Simba yalifungwa na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ dk 10, Joash Onyango dk 12, huku Kibu Denis akifunga mawili dk 46 na 57, wakati lile la kufuatia machozi kwa KMC lilifungwa na Abdul Hassan dk 39.
Mechi ya duru la kwanza lililopigwa Novemba 6, mwaka jana kwenye Uwanja KMC Complex, Simba ikiwa wenyeji ilishinda kwa mabao 4-0 yaliyowekwa kimiani na Awesu Awesu na Edwin Balua waliofunga moja, huku Jean Charles Ahoua akitupia mawili.
Rekodi zinaonyesha tangu KMC ipande rasmi Ligi Kuu msimu wa 2018-2019, haijawahi kuifunga Simba kwani mara 13 zilipokutana zimetoka sare mechi mbili na kupoteza 11, huku ikifunga mabao tisa na yenyewe kuruhusu 30.