Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga, Azam zahamisha vita ya Bara Gombani

YANGA Pict

Muktasari:

  • Mabao mawili ya kila kipindi yaliyowekwa kimiani na Stephane Aziz Ki na Denis Nkane yameifanya Yanga kutinga nusu fainali na kesho Jumanne itavaana na Zimamoto iliyoitoa Coastal Union kwa bao 1-0, huku Azam ikicheza mchezo wa kwanza wa nusu fainali leo dhidi ya JKU iliyong’oa Singida BS.

YANGA juzi usiku ilianza vyema michuano ya Kombe la Muungano kwa kuing’oa KVZ kwa mabao 2-0 na kuungana na Azam FC iliyofuzu mapema kwa kuiondosha KMKM na sasa wanaviziana kuhamishia vita ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba iwapo zitavuka mechi za nusu fainali.

Mabao mawili ya kila kipindi yaliyowekwa kimiani na Stephane Aziz Ki na Denis Nkane yameifanya Yanga kutinga nusu fainali na kesho Jumanne itavaana na Zimamoto iliyoitoa Coastal Union kwa bao 1-0, huku Azam ikicheza mchezo wa kwanza wa nusu fainali leo dhidi ya JKU iliyong’oa Singida BS.

Washindi wa mechi hizo za nusu fainali ndio wataokutana fainali itakayopigwa Mei Mosi na iwapo Yanga ambao ni mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo sambamba na Simba iliyoshindwa kushiriki msimu huu, itapenya dhidi ya Zimamoto na Azam kuitoa JKU zitakumbushia Dar es Salaam Derby.

Yanga iliyopo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara, ikiwa na pointi 70 baada ya mechi 26, wakati Azam ikiwa ya tatu na pointi 54 kwa mechi 27 na hivi karibuni zilivaana katika marudiano ya Ligi na Yanga ilishinda 2-1, pia msimu uliopita zilikutana katika fainali ya FA Zanzibar mechi ikipigwa New Amaan.

Ipo hivi. Baada ya Azam kuing’oa KMKM Ijumaa iliyopita kwa bao 1-0 leo kuanzia saa 1:15 usiku itashuka tena kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba kuvaana na watetezi wa Ligi Kuu Zanzibar, JKU katika mechi ya kwanza ya nusu fainali. JKU ilifika hatua hiyo kwa kuitoa Singida BS kwa mikwaju ya penalti 6-5, baada ya kikosi hicho kutoka nyuma kwa mabao 2-0 na kumaliza dakika 90 kwa sare ya 2-2.

Msimu uliopita michuano hiyo ya Muungano iliporudishwa tangu iliposimama 2003, Azam ilicheza fainali na kupoteza mbele ya Simba kwa bao 1-0 katika mchezo wa fainali uliopigwa New Amaan, mjini Unguja.

Kocha wa Azam, Rachid Taoussi baada ya mchezo wa hatua ya robo fainali dhidi ya KMKM, alisema wachezaji wanapaswa kuongeza umakini kutokana na ugumu wa mashindano uliopo, ili waweze kutimiza malengo ya kuchukua ubingwa huo mwaka huu bila kujali itakutana na timu gani.

Kesho Jumanne itakuwa ni zamu ya mechi ya pili ya nusu fainali kati ya Yanga itakapokuwa na kibarua kigumu cha kuvaana na Zimamoto inayoshika nafasi ya saba katika msimamo wa Ligi Kuu ya Zanzibar.

Yanga itashuka uwanjani kesho ikiwa inasaka rekodi ya kuchukua ubingwa huo mara nyingi zaidi ambapo endapo itauchukua itafikisha saba tangu michuano hiyo ilipoanza rasmi kuchezwa mwaka 1982 na kuwazidi mahasimu wao Simba waliochukua mara sita.

Katika mara sita ambazo Yanga imechukua ubingwa wa Kombe la Muungano yaani 1983, 1987, 1991, 1996, 1997 na 2000, ni mwaka 2000, ilikosa ubingwa wa Ligi Kuu uliochukuliwa na Mtibwa Sugar, ila miaka mitano ilichukua mataji hayo kotekote.

Mapema kocha wa kikosi hicho, Miloud Hamdi alisema, wanaenda Pemba kwa nia ya kuendeleza heshima ya klabu, licha ya kukiri ratiba inawabana ndio maana anawatumia wachezaji wengi ambao hawatumiki kikosi cha kwanza ili wengine wapate mapumziko kabla ya kurudi katika Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho, ikiwa imetinga nusu fainali na imepangwa kuvaana na JKT Tanzania siku ya Mei 16.

Mechi hiyo ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho itapigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga wakati nusu fainali ya pili itapigwa Tanzanite Kwaraa, Manyara kati ya Simba na Singida Black Stars.