Stumai, Shikangwa jino kwa jino kiatu Ligi Kuu

Muktasari:
- Stumai ndiye kinara wa ufungaji akiweka kambani mabao 26 nyuma yake yupo Shikangwa mwenye 19 katika mechi 14 walizocheza.
ACHANA na vita ya upachikaji mabao kwa nyota Jentrix Shikangwa wa Simba Queens na Stumai Abdallah (JKT Queens), kingine ni wanalingana kwa mabao ya ugenini.
Stumai ndiye kinara wa ufungaji akiweka kambani mabao 26 nyuma yake yupo Shikangwa mwenye 19 katika mechi 14 walizocheza.
Washambuliaji hao wanalingana kwa kufunga mechi za ugenini kila mmoja akiweka kambani 14, Winifrida Gerald wa JKT akifunga saba, Neema Paul wa Yanga Princess sita.
Kwenye mabao 26, mabao 12 amefunga Stumai akiwa kwenye uwanja wa nyumbani na 14 ugenini huku Shikangwa kwenye mabao 19 matano pekee amefunga nyumbani na 14 ugenini kiufupi ni washambuliaji hatari wanapokuwa ugenini.
Ukiachana na kufukuziana kwenye mbio za ufungaji, pia wanakimbizana kwenye hat-trick, Stumai akifunga tano na Shikangwa akiweka tatu.
Wengine ni Neema, Asha Djafar wa Simba, Ariet Udong wa Yanga Princess, Anastazia Shau wa Mashujaa Queens na Milembe John (Ceasiaa) wenye moja moja.