Liverpool yabeba ubingwa EPL ikiisulubu Totenham

Muktasari:
- Mara ya mwisho Liverpool kutwaa taji hilo ilikuwa msimu wa mwaka 2019/2020, na kusherehekea bila mashambiki wao uwanjani kutokana na uwepo wa mlipuko wa Uviko-19. Msimu huu wanatwaa kombe hilo mbele ya mashambiki zaidi ya 61,276 waliofurika katika uwanja wa Anfield.
Mgongo Kaitira
Imeisha hiyo. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Liverpool kuibamiza Totenham Hotspur kwa mabao 5-1 katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Anfield na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England (EPL).
Liverpool ambao sasa wanakuwa mabingwa wa ligi ya juu England wakifikisha makombe 20 sawa na Manchester United, wametangaza ubingwa huo leo Jumapili.
Totenham ilianza kutangulia kupitia bao la kona lililofungwa na Dominic Solanke dakika ya 12, kisha Luiz Diaz ameweka sawa mzani kwa kumalizia pasi safi ya Dominic Szoboszlai dakika ya 16 na baadaye Alexis MacAllister dakika ya 24akapiga shuti kali lililomuacha kipa Guglielmo Vicario mdomo wazi alipogeuka na kukuta nyavu zikitikisika.
Furaha ya mashambiki wa Liverpool walioujaza Uwanja wa Anfield yalipomwagwa majivu ya lejendari Billy Shanky iliongezeka baada ya Mholanzi Cody Gakpo dakika ya 34 kupigilia msumari kisha kuvua fulana na kuonyesha iliyokuwa ndani iliyoandikwa ‘Welcome to Jesus’ (karibu kwa Yesu). Gakpo amepigwa kadi ya njano kutokana na tukio hilo.
Mohammed Salah hakubaki mbali na goli la Totenham baada ya kuifungia Liveepool bao la nne dakika ya 62 na kukikaribia kiatu cha mfungaji bora wa EPL msimu huu kwa kufikisha mabao 28 kisha kuibua shangwe kwa mashabiki aliopiga nao ‘selfie’.
Dakika ya 68’, mchezaji wa Totenham, Destiny Udogie amekoleza furaha kwa mashambiki wa Liverpool baada ya kujifunga.