Sura mpya zinaitaka Man United

Muktasari:
- Man United iko nafasi ya 14 na wanakaribia kuwa na msimu wao mbaya zaidi katika historia ya EPL lakini hiyo haijazuia mastaa kutamani kutua kwenye kikosi chao.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim amefichua kuna kundi kubwa la wachezaji bora ambao wako tayari kujiunga nao licha ya timu yao kutofanya vizuri kwenye Ligi Kuu England msimu huu.
Man United iko nafasi ya 14 na wanakaribia kuwa na msimu wao mbaya zaidi katika historia ya EPL lakini hiyo haijazuia mastaa kutamani kutua kwenye kikosi chao.
Mashetani hawa wekundu kwa sasa wanapambana kuhakikisha wanashinda taji la Europa League ili kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao baada ya kutokuwa na msimu mzuri katika EPL.
“Ni Manchester United, Kile ninachohisi, kuna wachezaji wengi wanaotaka kucheza kwenye timu yetu. Najua ukiiangalia timu kwa sasa ina matatizo mengi, kuanzia wafanyakazi na watu kuondoka, kubadilisha kocha na matokeo, lakini bado wachezaji wanatamani kuwa hapa kwa sababu tuna mpango madhubuti juu ya nini tunahitaji. Mbali ya mipango yetu, ukweli pia hii ni Manchester United. Kila mtu anataka kuichezea.”
Man United wanapambana kufikia makubaliano na Wolves kwa ajili ya kumsajili staa wao Matheus Cunha dirisha lijalo la majira ya kiangazi, pia Liam Delap kutoka Ipswich na Victor Osimhen wa Napoli ni miongoni mwa washambuliaji wengine inaohitaji kuwasajili.
Amorim alikataa kujibu kuhusu uvumi mkubwa unaomhusu Cunha, ingawa hakukanusha ikiwa hana mpango naye kabisa.
Wengine ambao wamekuwa wakitajwa huenda wakatua Man United msimu ujao ni kipa wa Lille ya Ufaransa, Lucas Chavalier, Rayan Cherki anayekipiga Lyon na Viktor Gyökeres anayekipiga Sporting Lisbon ya Ureno alikotokea kocha Amorim.
Licha ya kusajili, kocha huyu pia ana majina ya wachezaji ambao watatakiwa kuuzwa lakini amesisitiza mambo yanaweza kubadilika kabla ya msimu kumalizika, hivyo hawezi kusema nani ataondoka na nani atabaki.
“Nimeshafikiria hilo kwa sababu tunahitaji kufanya mambo mapema, lakini mambo yanaweza kubadilika kabla ya kumalizika kwa msimu.”
Amorim anasema bado kuna wakati kwa wachezaji kumuonyesha utofauti akitolea mfano kwa Casemiro ambaye hivi karibuni amekuwa na kiwango bora.