Shule 117 zamwagiwa mipira ya Sh 35 Milioni

Muktasari:
- Msaada kwa shule hizo umetolewa na Shirika la Sports Development Aid ikiwamo 170 ya mpira wa miguu, 200 ya netiboli, 80 ya mpira wa wavu na 113 ya mpira wa mikono.
SHULE 117 za Sekondari mkoani Lindi, zimemwagiwa msaada wa mipira 585 ya michezo mbalimbali yenye thamani ya Sh35 milioni kwa ajili ya kukuza vipaji vya netiboli, soka, wavu na mpira wa mikono katika shule hizo na mkoa mzima.
Msaada kwa shule hizo umetolewa na Shirika la Sports Development Aid ikiwamo 170 ya mpira wa miguu, 200 ya netiboli, 80 ya mpira wa wavu na 113 ya mpira wa mikono.
Akizungumza juzi mara baada ya kukabidhiwa mipira hiyo Katibu Tawala Msaidizi Sekta ya Elimu, Joseph Mobeyo amewataka viongozi wa Halmashauri pamoja na Maofisa Elimu na Maofisa michezo kusimamia michezo shuleni ili kuweza kukuza vipaji vya wanafunzi.
“Katika kuimarisha elimu kupitia michezo kwa vijana niwaombe sana viongozi wenzangu kwenda kusimamia michezo kwa watoto wetu, tunalishukuru hili shirika la Sports Development Aid kwa kutupatia hii mipira 585 kwa ajili ya watoto wetu waliopo sekondari na mipira hii itasaidia sehemu ya maandalizi ya UMISSETA shuleni,” alisema Mobeyo.
Mkurugenzi wa Lindi Sport Development Aid, Ramson Lucas alisema lengo la kutoa mipira hiyo ni kuhamasisha ushiriki wa vijana katika michezo kama njia ya kuboresha afya, kuendeleza vipaji na kupunguza utoro shuleni.
“Tumeona tutoe mipira hiyo kwa shule 117 zilizopo mkoa wa Lindi ili kupunguza utoro shuleni, pia michezo husaidia kuboresha afya pamoja na kukuza vipaji vya wanafunzi,” alisema Lucas.
Mariam Shaaban, mwanafunzi wa Lindi Sekondari aliliambia Mwanaspoti kuwa, mipira hiyo itawasaidia sana kuimarisha afya na kujijenga kiakili.
“Unapokuwa unacheza unajenga akili pamoja na kuimarisha afya ya mwili, awali tulikuwa tunapata sana shida ya kucheza kutokana na mipira kuwa michache shuleni, ujio wa hii mipira umesaidia kuondoa changamoto kwani tutacheza kwa wakati na hatutagombaniana mipira na wavulana,” alisema Mariam.mipira ya Sh 35 Milioni